Monday, June 27, 2011

je unajua?

mwaka huu, mwezi wa julai utakuwa na ijumaa tano, jumamosi tano, jumapili tano, jambo hili hutokea mara moja kila baada ya miaka 823. Pia mwaka huu utashudia tarehe nne za ajabu ambazo ni 1/1/11, 11/1/11, 1/11/11, 11/11/11

Friday, June 17, 2011

HOTUBA YA BAJETI YA WAZIRI KIVULI WA FEDHA

1
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA FEDHA MHE.KABWE ZUBERI ZITTO (MB) KUHUSU MPANGO
NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA
WA FEDHA 2011/2012
______________________
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunipa afya njema na kuweza kusimama hapa mbele ya Bunge hili,
kuwasilisha Maoni na Mapendekezo ya Kambi ya Upinzani kuhusu
hali ya uchumi ya nchi yetu na bajeti kwa mwaka 2011/2012 kwa
mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 96(6).
Mheshimiwa Spika, Naomba kwa niaba ya waheshimwa wabunge
wote wa Kambi ya Upinzani ambao hawakupata nafasi ya kushiriki
au kutoa rambirambi zao kwako kwa msiba mkubwa uliokupata wa
kuondokewa na Mama yako mpenzi, nifanye hivyo kwa niaba yao.
Mheshimiwa Spika, Kabla ya kuanza kutoa mtazamo wetu naomba
nikishukuru chama changu cha Demokrasia na Maendeleo –
CHADEMA, viongozi wangu wakuu wote, kwa juhudi kubwa
tunazozifanya ili kuhakikisha Watanzania wanaelewa maana halisi
ya “wananchi kuwa na mamlaka kwa Serikali waliyoiweka
madarakani kwa njia ya kura”. Vile vile na kwa umuhimu wa
kipekee namshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mhe. Freeman
2
Aikael Mbowe (Mb) kwa kuniteua kuwa Waziri Kivuli wa Wizara hii
nyeti katika uchumi na maendeleo ya nchi. Kama ilivyo ada yangu,
nitaifanya kazi hii kwa uaminifu, uadilifu na umakini mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Aidha, namshukuru Mheshimiwa Christina
Mughwai (Mb) Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi – Wizara ya Fedha
kwa ushirikiano wake pamoja na timu nzima ya Kambi ya Upinzani
kwa kazi yao kubwa waliyoifanya katika maandalizi ya hotuba hii.
Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa Watanzania waliotupatia
maoni mbalimbali kupitia ‘social media’ kama facebook, twitter na
hata wengine kwa kupitia ujumbe mfupi wa sms. Maoni yao
yamesaidia kuboresha Hotuba hii na pia kuimarisha ushiriki wa
wananchi katika kutengeneza Sera za nchi.
Mheshimiwa Spika, Nitakuwa sijatenda haki kwa wananchi wa
Jimbo la Kigoma Kaskazini kama sitawashukuru kwa imani kubwa
waliyonayo kwangu, nami nawaahidi kuwa nitaitunza na kuiheshimu
imani yao kwangu, kuendelea kushirikiana nao kuleta maendeleo
katika Jimbo na Mkoa wetu na mwisho kukifanya CHADEMA kuwa
chama tawala hapo mwaka 2015. Asanteni sana.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Nchi ni nyenzo (instrument) ya
maendeleo. Sio suala la Urari tu wa Mapato na Matumizi. Ni namna
ya kutumia rasilimali chache tulizo nazo kwa ajili ya kutengeneza
3
rasilimali nyingi zaidi na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi na
kujenga Taifa Imara.
Hivyo basi, Bajeti inahusu namna ya kukusanya na kutumia pesa za
wananchi kwa manufaa yao ya pamoja. Kwa bahati mbaya,
mchakato wa kuamua namna ya kuzitumia, kuzisimamia na
kuhakikisha kuwa pesa hizo zinaenda zinakotakiwa kwenda ni
mgumu kwa wananchi wa kawaida kuweza kushiriki. Hii inatokana
na ukweli kuwa sehemu kubwa ya taarifa zinazohusiana na bajeti
huwa haziwekwi wazi kwa umma, na hata zile zinazopatikana huwa
katika namna iliyo ngumu kueleweka. Hivyo, wananchi wengi huwa
hawana fursa ya kushiriki katika michakato ya bajeti. Kwa ujumla,
michakato mingi rasmi huwa haiko wazi kwa wananchi. Hata hivyo,
juhudi zilizoanza sasa za kutaka kuanzisha Ofisi ya Bajeti ya Bunge
zitasaidia sana kuweka uwazi katika Bajeti ya Nchi na hivyo kuweka
urahisi wa wananchi kushiriki katika mchakato.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imekuwa ikiitaka Serikali
kuweka vitabu vya bajeti katika mfumo rahisi unaoweza kueleweka
na kufuatiliwa na wananchi wengi, lakini suala hilo limekuwa gumu
kufanyika. Nina matumaini kuwa kwa miaka ijayo na hasa baada ya
kuanzisha Ofisi ya Bajeti ya Bunge, vitabu vya Bajeti vitakuwa
vinapatikana mapema na kwa njia rahisi.
Mheshimiwa Spika, Tunaamini kuwa ushiriki mkubwa zaidi wa umma
na uchunguzaji wa utungaji na utekelezaji wa Bajeti utaboresha
4
uwajibikaji na kuziba mianya zaidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya
rasilimali za nchi.
Mheshimiwa Spika, Mahatma Gandhi aliwahi kusema “Mabadiliko
ya kidemokrasia hayawezekani iwapo hatupo tayari kusikiliza
upande mwingine. Tunafunga milango ya kufikiri wakati
tunapokataa kuwasikiliza wapinzani wetu, au baada ya kuwasikiliza
tunawafanyia mzaha. Kutokuvumiliana kunapokuwa ndio mazoea,
tunajiweka katika hatari ya kutokujua ukweli”.
Kambi ya Upinzani ilitoa maoni yake ya mwelekeo wa Bajeti na
kuainisha mambo kadhaa itakayoyapendekeza katika Bajeti yake
Mbadala. Mambo hayo ni pamoja na;
i. Kupunguza misamaha ya Kodi ili isizidi 1% ya Pato la Taifa.
ii. Kupunguza kodi na tozo kwenye Mafuta ya Petroli na Dizeli ili
kupunguza mfumuko wa Bei na ukali wa maisha kwa
wananchi.
iii. Kufanya Marekebisho makubwa katika mfumo wa malipo
Serikalini hususan kuondoa Posho za vikao (sitting allowances)
kwa watumishi na viongozi wote wa Umma
iv. Kuelekeza sehemu ya tozo ya kuendeleza ujuzi (Skills
Development levy) kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu.
5
Mheshimiwa Spika, Katika Hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi,
baadhi ya mambo haya yalizingatiwa na kupewa kipaumbele.
Ninachukua fursa hii kumpongeza Waziri mwenzangu kwa kusikiliza
maoni yetu kwenye baadhi ya mambo hayo na hivyo kuonyesha
kwa umma moja ya faida ya mfumo wa vyama vingi. Tunataraji
kuwa Serikali itaendelea kusikiliza maoni yetu na kuyafanyia kazi.
Changamoto hii na kwa uzito ule ule pia ipo kwetu sisi wa Kambi ya
Upinzani kusikiliza pia maoni ya Serikali. Ni kwa namna hii ndio
tutajenga Taifa la watu walio huru, lenye demokrasia, usawa na
haki, na lenye kutoa fursa kwa wananchi wake.
TATHIMINI YA HALI YA UCHUMI.
Mheshimiwa Spika, Ninapopitia Hali ya Uchumi ili kutoa maoni ya
Kambi ya Upinzani Bungeni ni vema tulijue Taifa letu kwa Takwimu
Chache.
Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa limefikia shilingi 32 trilioni na hivyo
Pato la wastani la kila mtu kuwa shilingi 770,000. Tanzania ina
takribani wananchi 42 milioni na kati ya hao 11 milioni wapo kwenye
taasisi za Elimu kwa maana ya Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya
Ufundi na Vyuo vya Elimu ya Juu! Kwa hiyo Robo ya Watanzania
wanasoma hivi sasa na wakimaliza wanataraji kupata ajira kwa
kuajiriwa au kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2010 Watanzania 19 milioni walikuwa
wanatumia simu za mkononi na hivyo kufanya asilimia 45 ya
6
Watanzania kuwa na simu na kuliweka Taifa katika nafasi ya juu
kabisa duniani ya matumizi ya simu. Asilimia 64 ya Watanzania
wanapata maji safi na salama mijini na asilimia 57.8 hupata huduma
hii vijijini. Asilimia 14 ya Watanzania wanapata huduma ya umeme
na kwa vijijini ni asilimia 2 tu.
Mheshimiwa Spika, Asilimia 33.4 ya Watanzania wanaishi chini ya
mstari wa umasikini na kwa waishio vijijini ni asilimia 37.4 wakati
asilimia 16.2 tu ya Watanzania waishio Dar es Salaam wanaishi chini
ya mstari wa Umasikini. Wakati tofauti ya kipato kwa Watanzania ni
asilimia 35, matajiri wa juu asilimia 20 wanamiliki asilimia 42 ya Pato
la Taifa (consumption expenditure) na masikini wa chini kabisa
asilimia 20 wanamiliki asilimi 7 tu ya Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika
mwaka 2010/11 iliyosomwa hapa Bungeni inaonyesha kuwa katika
mwaka 2010/11 Pato halisi la Taifa lilikuwa kwa kiwango cha asilimia
7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.0 mwaka 2009/10. Taarifa
inaonyesha kuwa ukuaji huu wa uchumi ulitokana na kuchangiwa
zaidi na kuongezeka kwa viwango vya ukuaji katika shughuli za
kiuchumi zenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa na hasa
Kilimo, Biashara na matengenezo na ujenzi.
Mheshimiwa Spika , pamoja na taarifa hiyo ukweli ni kuwa ukuaji wa
viwango vya juu ulionekana zaidi kwenye sekta za Mawasiliano
(22.1%), ujenzi (10.2%), umeme na gesi (10.2%), fedha (10.1%) na
7
uzalishaji viwandani (7.9%). Hata hivyo, pamoja na ukuaji wa sekta
hizi, mchango wake katika pato la Taifa ni mdogo kulingana na
kiwango cha ukuaji wa sekta husika kwa mwaka 2010/11.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Hali ya uchumi inaonyesha kuwa
pamoja na sekta kadhaa kukua lakini bado hazijaongeza mchango
wake katika ukuaji wa pato la taifa ukilinganisha na ukuaji wa sekta
husika. Kwa mfano, sekta ya mawasiliano imekuwa kwa asilimia 22.1
ila mchango wake katika pato la Taifa ni asilimia 2.1 tu, shughuli
ndogo za hoteli na migahawa ukuaji wake ulikuwa 6.1 lakini
mchango wake katika ukuaji wa pato la taifa ni 2.3% tu. Hii ina
maana kuwa sekta hizi hazina uhusiano wa moja kwa moja (strong
linkages) katika ukuaji wa uchumi na katika kukuza pato la taifa na
hivyo kushindwa kupunguza hali ngumu ya maisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya hali ya uchumi inaonyesha kuwa
mchango wa shughuli za kiuchumi za kilimo umeendelea kushuka,
hii ni pamoja na ukweli kuwa Serikali katika mwaka husika ilijikita
kwenye “Kilimo Kwanza” jambo ambalo halionyeshi kama ni kilimo
kwa kauli tu ama ni kweli tunawekeza kwenye kilimo katika kukuza
uchumi wa wananchi takribani asilimia 71 ambao wanategemea
kilimo kama msingi mkuu wa maisha yao. Pia mauzo ya mazao nje
ya Nchi yalipungua kama ifuatavyo: kahawa (36.4), Pamba (24.3),
Chai (39.0), Karafuu (47.0); hii ni pamoja na ukweli kuwa bei za
mazao husika iliongezeka ukilinganisha na mwaka 2009/10, ila sisi
8
tulishindwa kuitumia fursa hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi
wetu ambao ni wakulima wa mazao haya kwa kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika ,
Ukisoma taarifa ya hali ya uchumi utaona kuwa ni sekta mbili za
utoaji huduma na viwanda na ujenzi ndizo zinachangia pato la Taifa
kwa asilimia 66.3. Hii maana yake ni kuwa sekta mama ya kilimo
ambayo ndiyo inaweza kuwaondolea watanzania umasikini kwa
sasa ina mchango mdogo katika Pato la Taifa. Mabadiliko haya ya
kimuundo wa uchumi wetu ndio sababu kubwa tunakuwa na
uchumi unaokua bila kupunguza umasikini. Narejea kusema kuwa
kwa sasa, ukilinganisha na tulipotoka, licha ya kwamba tunahitaji
ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi, ukuaji sio changamoto kubwa.
Changamoto sasa ni namna gani ukuaji huu wa uchumi unawafikia
wananchi. Sekta zinazokuwa kwa kasi ni zile zinazoshawishi uwekezaji
wa sekta binafsi kwa urahisi. Sekta ya Kilimo inahitaji uwekezaji
mkubwa wa kimiundombinu wa Serikali. Nchi yetu itaendelea na
changamoto ya kupunguza umasikini hadi hapo tutakapoamua
kwa dhati kuwekeza katika kukuza uchumi wa vijijini. Kambi ya
Upinzani inapendekeza katika Bajeti hii mbadala mikakati maalumu
ya kukuza uchumi wa vijijini kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya
vijijini, umeme vijijini na maji vijijini.
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2010/11 ukuaji katika shughuli za kiuchumi za Madini
9
na uchimbaji mawe uliongezeka na kufikia asilimia 2.7. Ukuaji huu
ulichangiwa zaidi na kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu na
kuongezeka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia. Hata hivyo,
mchango wa sekta hii pamoja na kuongezeka uzalishaji na bei kuwa
kubwa zaidi ya mwaka 2009/10 bado uliendelea kuwa ule ule wa
mwaka 2009/10 wa asilimia 3.3 pamoja na kuuza nje dhahabu
yenye thamani ya dola za kimarekani 1,516.6 milioni mwaka 2010/11.
Mauzo haya ya Dhahabu nje kwa mwaka 2010/11 ni sawa na
asilimia 7.1 ya Pato la Taifa kwa hesabu za mwaka husika. Ukiangalia
mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, mchango
kwenye Mapato ya Serikali na Mchango wa Sekta katika Mauzo ya
nje unaona dhahiri kabisa kuwa bado tunahitaji kufanya kazi ya
ziada kuhakikisha sekta ya Madini inakuwa na mahusiano na Sekta
nyingine za uchumi (linkages). Masuala haya yanahitaji kusimika sera
madhubuti (policy interventions) ili kulifanya Taifa lifaidike na utajiri
wa Madini. Kuboresha sera za Kikodi ikiwemo kujenga uwezo wa
Wakandarasi wa ndani katika sekta ya Madini na kuhusisha sekta
ndogo ya Umeme na sekta ya Madini ni masuala ambayo
tunapaswa kuyaamulia wenyewe.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya hali ya uchumi inaonyesha kuwa mwenendo wa
mfumuko wa bei umekuwa ukiongezeka tangu mwezi Oktoba 2010
kutoka asilimia 4.2 na kufikia asilimia 5.6 mwezi Disemba 2010 , mwezi
Januari 2011 ulikuwa asilimia 6.4 na hadi kufikia mwezi Aprili 2011
10
mfumuko wa bei ulikuwa umefikia asilimia 8.6. Hii ina maana yake
kuwa mfumuko wa bei unaongezeka kwa wastani wa asilimia 0.8
kila mwezi . Hali hii inaelezwa kuwa ni kutokana na ongezeko la bei
za umeme , gesi na chakula , jambo hili ni la hatari katika ukuaji wa
uchumi kama hatua za haraka na dharura hazitachukuliwa ili
kuweza kukabiliana na jambo hili kwani kama hali itaendelea kuwa
hivyo kwa miezi mitano tu ijayo, mfumuko wa bei utakuwa umefikia
asilimia 12.6. Serikali imekubaliana na hoja ya Kambi ya Upinzani
kwamba itaangalia tozo katika bei za mafuta ili kudhibiti hali hii.
Hata hivyo, suluhisho la muda mrefu la kudhibiti mfumuko wa Bei ni
kuzalisha chakula cha kutosha kwani chakula ni sehemu kubwa ya
kikapu cha bidhaa na huduma ambazo Mtanzania anatumia.
Ikitokea kuwa Bei za Mafuta katika soko la Dunia zikapanda tena na
kuyafanya maamuzi yetu ya kikodi hayana maana kuna haja ya
Serikali kuangalia jinsi ya kufidia kupanda kwa Bei za Umeme kwa
asilimia 18 ili kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Thamani ya Shilingi ya Tanzania imeendelea kushuka ukilinganisha
na fedha za kigeni na hii inatokana na kukosekana kwa mikakati
thabiti ya kuhakikisha kuwa shilingi inaimarika kwenye soko na hasa
kutokana na sera mbovu za kiuchumi na usimamizi usio makini.
Kushuka kwa thamani ya Shilingi licha ya kupanda kwa mauzo yetu
nje kwa sekta zote mbili tunazotegemea sana (Madini na Utalii)
kunaacha maswali mengi kuhusiana na chaguo letu kuhusu Hifadhi
11
ya Fedha za kigeni. Kambi ya Upinzani inaunga mkono ushauri
uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
kwamba sasa Benki Kuu ya Tanzania ianze kutunza sehemu ya
Hifadhi ya nchi katika Dhahabu. Benki Kuu inunue dhahabu kutoka
kwa wachimbaji wadogo na pia tuangalie uwezekano wa kutoza
sehemu ya mrahaba katika madini kama ‘dhahabu safi’ (‘pure
gold’).
Mheshimiwa Spika,
Deni la taifa linaonekana kuongezeka kwa kasi ya ajabu sana na
hivyo kupelekea Taifa kuwa na mzigo mkubwa sana wa Madeni.
Kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 38 kutoka Tshs 7.6 trilioni
mwaka 2008 mpaka Tshs 10.5 trilioni mwaka 2009 na sasa kwa mujibu
wa Hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi Deni limefikia Dola za
Kimarekani 11. 4 Bilioni ambazo ni sawa na Tshs 17.1 Trilioni kwa bei
ya Dola ya Kimarekani ya Disemba 2010. Jedwali hapa chini
linaonyesha Deni la Taifa na Malipo ya Deni hilo.
12
Mheshimiwa Spika, Mataifa yote Duniani hukopa sembuse sisi Taifa
linaloendelea. Hata hivyo, kasi ya ukopaji wetu sio endelevu hata
kidogo na kwa kweli ni mzigo mkubwa kwa kizazi kijacho. Kwa
mfano, tunapoangalia Bajeti ya mwaka huu utaona kuwa asilimia 50
Ya Bajeti itagharamiwa na Kodi zetu, lakini asilimia 30 itagharamiwa
na Mikopo ya ndani, ya nje na ya kibiashara, asilimia 17 Misaada na
asilimia 3 Makusanyo ya Halmashauri. Hii maana yake ni kwamba
asilimia 30 ya gharama za sasa za Serikali itabebwa na kizazi kijacho
kwani madeni haya yatalipwa na kizazi hicho.
13
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza ufanyike uchunguzi
Maalumu kwenye Deni la Taifa ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali atuambie madeni haya tunayokopa kwa kasi ya
namna hii tunayapeleka kweye miradi gani (Matumizi ya Madeni)
na namna gani tunaweza kudhibiti Deni la Taifa.
UDHAIFU KATIKA MATUMIZI YA FEDHA ZA UMMA.
Ripoti ta CAG katika Mwaka wa Fedha 2009/10
Mheshimiwa Spika,
Matumizi mabaya ya fedha za umma yameendelea kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.
Uchambuzi wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2009/2010 pekee, umebaini
takribani jumla ya Tsh trilioni 2.4 za fedha za umma zilitumika vibaya,
ambazo ni sawa na asilimia 25% ya bajeti yote ya mwaka huo
ambayo ilikuwa na jumla ya Sh 9.5 trilioni. Hii inaonyesha kuwa
katika kila Shilingi 100 tunayopitisha hapa Bungeni katika Bajeti
Shilingi 25 zinaingia kwenye mifuko ya wezi na wabadhirifu wa fedha
za Umma. Hali hii lazima ikomeshwe mara moja.
Mheshimiwa Spika,
Mifano ya fedha zilizopotea au kutumiwa vibaya katika mwaka wa
fedha wa 2009/10 ni manunuzi yaliyofanywa nje ya mpango wa
mwaka ya jumla ya Tsh bilioni 50.6, malipo yenye shaka ya jumla ya
14
Tsh bilioni 15.5, upotevu wa fedha na mali za serikali wa jumla ya Tsh
bilioni 11.1 na malipo ya mishahara kwa watumishi waliostaafu,
waliokufa na watoro kazini ya jumla ya Tsh bilioni 1.8.
Aidha, Mkaguzi hakukabidhiwa nyaraka na orodha ya walionufaika
na kiasi cha jumla ya Sh. bilioni 48 (Stimulus package) kilichotolewa
kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi toka Benki Kuu ya Tanzania
katika juhudi za kukabiliana na msukosuko wa uchumi ulioikumba
dunia.
Katika mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi nilimwuliza Mheshimiwa
Waziri Mkuu kuhusu suala la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kunyimwa nyaraka ili kukagua jumla ya Tshs 48 bilioni
zilizotajwa hapo juu. Natumai sasa Serikali itakuwa na majibu juu ya
suala hili. Kambi inaendelea kusisitiza ombi lililotolewa na aliyekuwa
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Mheshimiwa Hamad Rashid
Mohammed kwamba Fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya Stimulus
Package zikaguliwe na CAG na kuwasilisha Taarifa hiyo maalumu
Bungeni. Serikali ilikubaliana na ombi hili hivyo tunaomba taarifa hiyo
mara moja.
Mheshimiwa Spika,
Tunalisema hili la Stimulus Package kwa kuwa kuna ushahidi wa
barua kutoka kwa Katibu Mkuu Hazina akiwaandikia Mameneja wa
vyama vya ushirika vya mikoa ya Kilimanjaro na Kagera akiwaeleza
kuwa Serikali pamoja na kuidhinisha kulipwa kwa vyama hivyo, kwa
sasa hakuna fedha kwa ajili ya kufanya malipo hayo.
Barua iliyoandikwa kwa Meneja Kagera Cooperative Union (1990)
ltd ya tarehe 16 Septemba 2010 yenye kumb. Na TYC/B/40/143
ilikuwa ikimweleza Meneja kuhusiana na serikali kulipa kiasi cha
shilingi 734,369,379.49 . Ila ilipofika tarehe 27 Aprili 2011 Katibu Mkuu
wa Hazina aliandika barua nyingine kwa Meneja husika yenye
kumb.Na.TYC/B/40/143/45 kwa ajili ya kusitisha Malipo ya fidia
15
kutokana na mdororo wa uchumi kwa kuwa Serikali haina fedha na
pia muda wa kulipa fidia hizo ulikwisha tangu mwaka 2010.
Kuhusiana na chama cha ushirika cha Mkoa wa Kilimanjaro
(Kilimanjaro Native Cooperation Union (1984), Katibu Mkuu Hazina,
Ndugu Ramadhan Kijjah mnamo tarehe 16 Septemba aliandika
barua yenye kumb.Na TYC/B/40/143 iliyowajulisha kuwa Serikali
imeridhika kuwa wanastahili kupewa fidia ya shilingi 255,107,570.17
waliyopata kutokana na mdororo wa uchumi duniani. Ila ilipofika
tarehe 27 Aprili 2011 Katibu Mkuu huyo huyo aliandika barua
nyingine yenye kumb.Na.TYC/B/40/143/43 akiwajulisha kuwa Serikali
haina fedha kwa ajili ya kulipa fidia hiyo na kuwa muda wa kulipa
fidia ulikuwa umekwisha tangu mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika,
Kupatikana kwa barua hizi ni uthibitisho wa wazi kuwa kuna tatizo
kubwa kuhusiana na fedha zilizotolewa na Serikali kwani wakati
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Omar Yusuph Mzee akiwa anajibu swali
la msingi la Mhe. Mhonga Saidi Ruhanywa wakati wa Bunge la Bajeti
la mwaka 2010/11 alisema kuwa mpango ulikuwa unaenda vizuri.
Pia wakati Waziri wa Fedha Mhe. Mkullo akiwa anahitimisha hotuba
ya bajeti ya mwaka 2010/11 alilieleza bunge hili kuwa mpango
ulikuwa unaenda vizuri.
Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa tunaitaka Serikali ifanye ukaguzi
maalum kwenye mfuko huu.
JEDWALI 1.
JUMLA YA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA YALIYOAINISHWA KATIKA TAARIFA YA MDHIBITI NA MKAGUZI
MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2009/2010
MAELEZO KIASI
Manunuzi yaliyofanywa nje ya mpango wa mwaka 50,685,371,565.58
Matengenezo ya magari ambayo hayakupitia TEMESA 176,722,089.00
Malipo ya mishahara kwa watumishi waliostaafu, waliokufa na watoro kazini 1,842,607,565.29
Malipo ya posho ya samani kwa maafisa wasiostahili 770,087,895.00
Malipo yenye nyaraka pungufu 4,303,339,515.00
16
Vifaa vilivyolipiwa bado havijapokelewa 13,865,874,762.00
Malipo yaliyofanyika katika kasma isiyosahihi 4,953,226,683.00
Malipo yenye shaka 15,595,054,755.00
Madeni na mihadi ya serikali 254,616,874,180
Misamaha ya kodi 680,667,900,000.00
Maduhuli yasiyokusanywa kwa wakati 116,320,437,345.00
Madeni ya dharura ambayo hayakutarajiwa 26,276,785,317.00
Kutoa udhamini kinyume na kiwango kilichowekwa na sheria 711,804,989,096.00
Madai na amana za serikali ambazo hazikutolewa taarifa 134,046,000,000.00
Madeni ya vifaa na huduma ambayo hayakulipwa 160,756,067,190.00
Upotevu wa fedha na mali za serikali 11,152,048,065.00
Kutokuwepo uwazi katika mifuko maalumu ya fedha 78,014,807,604.00
Bakaa ambayo haikurejeshwa kwa mlipaji mkuu 31,821,562,811.00
Kukosekana kwa orodha ya waliolipwa kuchochea ukuaji wa uchumi 48,000,270,000.00
Malipo kwa Benki ya Rasilimali bila nyaraka za muhimu kutolewa 70,000,000,000.00
Jumla ya fedha zilizotumika vibaya katika mwaka husika wa fedha 2,415,670,026,437.87
Bajeti ya mwaka husika ilikuwa 11,000,000,000,000.00
Kwa hiyo, Jumla ya fedha zilizotumika vibaya ni sawa na 20% ya bajeti nzima 2,415,670,026,437.87
MAMBO MENGINE YA KUTILIWA MAANANI
Deni la taifa limekua kwa 38% na kufikia T rilioni 10
Jumla ya mali za serikali ambazo hazipo katika rejista Trilioni 7.9
Jumla ya fedha zisizoonekana kutokana na dosari za kibenki kwa muda mrefu Bilioni 747.1
Fedha nyingi zilizotumiwa na serikali zaidi ya amana iliyopo benki Trilioni 1.3
Jumla ya vitega uchumi vya serikali ambavyo hesabu hazikurekodiwa Trilioni 8.7
BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2011/2012.
Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2011/2012 inapendekezwa kufikia
shilingi 13.5 trillioni kutoka shilingi 11.2 trillioni ya Mwaka wa Fedha
unaokwisha wa 2010/2011. Kwa maana ya Shilingi za Kitanzania
Bajeti inaonekana kukua hata hivyo ukiondoa mfumuko wa Bei kwa
wastani wa asilimia 7%, ambao unapunguza uwezo wa kimanunuzi,
utaona thamani halisi ya Bajeti ni kama Shilingi 12.5 trillioni hivi.
Ukiibadilisha Bajeti kwa dola za Kimarekani ambapo mwaka 2010
17
ilikuwa ni wastani wa Shilingi takribani 1400 kwa dola moja ya
kimarekani na sasa siku Waziri anasoma Bajeti thamani ya Shilingi
ilikuwa na thamani ya shilingi 1581 kwa dola moja ya Kimarekani
utaona kuwa kwa uhalisia (in real terms) hakuna nyongeza ya Bajeti.
Hivyo kuna haja kubwa ya kuimarisha sarafu yetu na kudhibiti
mfumuko wa Bei.
Mheshimiwa Spika ,
Mnamo tarehe 08/06/2011 Waziri wa Fedha Mhe. Mustafa Mkullo
aliwasilisha Bungeni Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya
Mapato na Matumizi kwa mwaka 2011/12. Na aliwaeleza
Watanzania kuwa bajeti ya mwaka huu ni mahususi kwa ajili ya
masuala yalioyoorodheshwa hapa chini. Nanukuu, “Bajeti ya
mwaka 2011/12 itazingatia vipaumbele vifuatavyo:
i) Umeme;
ii) Maji;
iii) Miundombinu ya usafiri na usafirishaji (reli, bandari, barabara,
viwanja vya ndege, Mkongo wa Taifa);
iv) Kilimo na umwagiliaji; na
v) Kupanua ajira kwa sekta binafsi na ya umma.
Mheshimiwa Spika,
Wakati waziri akitaja kuwa kipaumbele cha kwanza ni Umeme
ukiangalia kwenye vitabu vya Bajeti vya serikali, Wizara ya Nishati na
Madini imetengewa jumla ya shilingi 402.4 bilioni kwa mujibu wa
fungu la 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi
shilingi 76,953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya Maendeleo
zimetengwa shilingi 325,448,137,000. Katika hali hii tunaona kuwa
umeme hauwezi kuwa kipaumbele katika bajeti hii kwa kuwa
18
haujapewa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Wizara ya Nishati na Madini inatengewa kiasi hicho cha
fedha, ukiangalia fungu lililotengwa kwa ajili ya Hazina (“the
treasury”) fungu 21 zimetengwa jumla ya shilingi 1,054,411,138,000.
Fedha zilizotengwa kwa Hazina fungu 21 ni sawa na asilimia 8% ya
bajeti yote ya serikali. Wakati Wizara ya Nishati na Madini, vote 58
yote imepangiwa fedha za Maendeleo Tshs 325.4 Bilioni, Hazina
imepangiwa Tshs 129 Bilioni kwa ajili ya matumizi mengine ya
kiutendaji (‘other operating expenses’) na Tshs 314 bilioni kwa ajili ya
matumizi mengine ila yasiyo ya dharura (‘contingencies-non
emergence’). Nimemsikia Mheshimiwa Mkulo anasema kuwa Fedha
nyingine ya Umeme ipo Wizara ya Fedha kupitia MCC. Hata hivyo,
ukiangalia fungu 50 fedha za Maendeleo MCC zimetengwa shilingi
111 bilioni ambazo hazifikii jumla anayosema Waziri. Zaidi ya hapo
fedha za MCC sio za miradi ya Umeme peke yake, ni pamoja na
Barabara nk. Ningependa kupata ufafanuzi zaidi ambao
unathibitishwa na vitabu vya Bajeti na sio maneno matupu katika
Hotuba.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Waziri akisema Bungeni kuwa bajeti ya mwaka 2011/12
itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuthibiti
matumizi, nanukuu “kupunguza malipo ya posho mbalimbali
19
yasiyokuwa na tija (uk.53) “ , ukweli ni kuwa Bajeti ya serikali ya
mwaka 2011/12 imetenga jumla ya shilingi 0.987 trilioni ambazo ni
sawa na asilimia 13 % ya bajeti yote ya matumizi ya kawaida ya
serikali na asilimia 6% ya Bajeti yote kwa ajili ya kulipa posho. Kambi
ya Upinzani inahoji, je, Waziri atapunguza posho zipi na kwa kiasi
gani wakati tayari ametenga kiasi cha sh. Trilioni 0.987 kwa ajili ya
posho.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Waziri wa Fedha akisema kuwa ili kudhibiti matumizi
watapunguza posho mbalimbali, wakati huo huo katika hotuba
yake uk. 66, anapendekeza kufanywa kwa marekebisho ya sheria
ya kodi ya mapato SURA 332 na anasema kwenye (i) “kusamehe
kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa
serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku
kutoka kwenye bajeti ya serikali”. Sasa tumeanza kusikia vilio kutoka
sekta binafsi kwamba na wao wapate unafuu huu wa kodi. Kambi
ya upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za
vikao (sitting allowances) uondoke katika utumishi wa umma.
Ninaomba ieleweke kuwa hatupingi posho za kujikimu ambazo
viongozi au maafisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo
vyao vya kazi. Posho hizi zirekebishwe kuendana na gharama za
maisha za sasa. Lakini Posho za vikao zifutwe mara moja. Ili
kuonyesha kuwa Viongozi wa kisiasa tunaelewa kilio cha wananchi
kuhusiana na gharama za maisha na kupunguza matumizi ya
20
serikali, waheshimiwa Wabunge tunaanza na posho za vikao vya
Bunge. Iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na
kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa
Serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuwahoji
na kuwawajibisha. Mfumo wa Posho za Vikao ni rushwa ya kitaasisi
wanaojipa watu wenye mamlaka. Wakati kiongozi wa umma
anapolipwa posho kwa kikao cha kufanya maamuzi yanayohusiana
na majukumu yake ya kazi ambayo kwayo analipwa mshahara,
Polisi halipwi posho kwa kulinda, Mwalimu halipwi posho kwa kuingia
darasani na wala Nesi halipwi posho kwa kusafisha vidonda vya
wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kufanya marejeo ya
mfumo wa posho na mfumo wa mishahara kwa watumishi wa
umma. Suala hili ni lazima tulianze sasa na katika Bajeti hii
tunayoijadili. Lazima kuwaonyesha Watanzania kuwa tunajali hali
zao ili kurejesha imani ya Umma kwa Wanasiasa na viongozi wao.
Mheshimiwa Spika, vipaumbele sita vilivyotolewa katika hotuba ya
Mheshimiwa Waziri ni:
Fedha zimewekwa katika Tshs. Billioni
Miundombinu-Barabara,reli, bandari na mkongo wa Taifa 2,781.40
Nishati na
Madini 539.3
Maji 621.6
Kilimo na Umwagiliaji 926.2
Elimu 2,283.00
Afya 1,209.10
21
JUMLA KWA SEKTA SITA 8,360.60
Mheshimiwa Spika, Tshs 8.361 Trilioni ni kwa ajili ya
Sekta sita tu ambayo ni sawa na asilimia 62% ya
bajeti nzima.
Katika kufanya uchambuzi katika vitabu vya bajeti imeonyesha kuwa
hizo sekta sita zimo kati ya mafungu 15 ambayo yamepangiwa fedha
nyingi ambayo ni pamoja na deni la taifa ambalo ni sh. 1.9 trilioni.
Hivyo basi, ukiongeza mafungu mengine sita ambayo ni fungu (21,
28,30,37,38 na 57) unapata jumla ya Tshs.12,586.11Trilioni.
Mheshimiwa Spika, Jumla ya bajeti nzima kwa mwaka huu ni Tshs.13,
525.90 Trilioni. Kwa mahesabu ya kawaida ni kwamba kuna tofauti ya
Tshs.939.8 bilioni kati ya matumizi kwa sekta za vipaumbele pamoja na
idara zingine zilizopewa fedha nyingi na Bajeti kuu. Mgawo wa fedha
za serikali kwa mafungu 15 ya juu ni kama ifuatavyo.
SUMMARY OF PUBLIC EXPENDITURE AND DEVELOPMENT FUNDS FOR MINISTRY/ DEPARTMENTS AND AGENCIES - 2011/12
S/N VOTE DESCRIPTION PUBLIC EXPENDITURE
AMOUNT PERCENTAGE
1 22 Public Debt and General Services 1,901,850,995,000 30.30%
2 98 Ministry of Works 245,440,294,000 4.00%
3 21 The Treasury 1,000,073,144,000 16%
4 46 Ministry of Education and V. Training 523,778,766,000 8.30%
5 52 Ministry of Health and Social Welfare 219,367,376,000 4%
6 50 Ministry of Finance 85,794,616,000 1.37%
7 49 Ministry of Water 17,455,673,000 0.28%
8 38 Defence 415,416,165,000 6.60%
9 58 Ministry of Energy and Minerals 76,953,934,000 1.23%
10 28 Ministry of Home Affairs - Police Force 276,144,464,000 4.40%
11 30 President's Office and Carbinet Secretariat 200,519,723,000 3.20%
12 43 Ministry of Agriculture, Food and Cooperation 152,406,152,000 2.40%
13 62 Ministry of Transport 69,585,672,000 1.11%
14 57 Defence and National Service 14,973,547,000 0.24%
22
15 37 Prime Minister's Office 32,291,737,000 0.51%
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaona kuwa bajeti hii ni ya nadharia zaidi kwani
kwa hali ya kawaida Wizara na idara za serikali zilizobakia haziwezi
kutumia Tshs.939.8 bilioni tu! Hapa inaonyesha bajeti iliyosomwa na
Mhe Waziri ilikuwa na lengo la kuwafumba macho watanzania na
kuwapa matumaini tu. Hili ni jambo la hatari kwani mara zote ukweli
uliofichwa pindi utakapofichuliwa kwa njia yeyote madhara yake
yanakuwa ni makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, licha ya uchambuzi hapo juu utagundua kirahisi
kabisa kuwa Waziri wa Fedha amerundika Fedha za Miundombinu
kwa pamoja ili kuhadaa Umma. Ukiangalia vitabu vya Bajeti utaona
kuwa katika Tsh 2.8 trilioni zilizotengwa kwa miundombinu, Tsh 1.5 trilioni
ni kwa Wizara ya Ujenzi peke yake na kuacha fedha nyingine kwa
Wizara zilizobakia. Utaona kuwa Wizara ya Uchukuzi inayosimamia
sekta nyeti kama Reli, Bandari, usafiri wa majini na Shirika la Ndege la
Taifa imetengewa fedha kidogo sana ambazo ni Tsh 69 bilioni kwa
matumizi ya kawaida na Tshs 167 bilioni kwa Maendeleo. Shirika la
Ndege, Shirika la Reli na Shirika la Usafiri majini (MSCL) hazijatengewa
fedha za kuweza kuyafanya mashirika haya yaanze kazi mara moja,
kwa ufanisi na kutengeneza faida miaka ya usoni.
Mheshimiwa Spika,
23
Bajeti ya serikali ya mwaka 2011/12 imewaongezea mzigo mkubwa
sana wananchi na hasa wajasiriamali wadogo na vijana ambao
wamejiajiri ama kuajiriwa kwenye biashara ya usafiri na usafirishaji.
Kwani serikali inapendekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria
ya usalama barabarani sura 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango
cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati akiwa
anaendesha gari yaani (Traffic Notification Fee) kutoka shilingi 20,000
hadi shilingi 300,000. Ingawa Waziri alitamka kwa maneno kuwa
faini itakuwa Tshs 50,00 kwenye kitabu cha hotuba yake ni Tshs
300,000. Kambi ya Upinzani haipingi adhabu kwa wakosaji wa
makosa barabarani isipokuwa tuna wasiwasi kuwa adhabu hii
itasababasha rushwa kuongezeka. Ila ikisimamiwa vizuri itapelekea
kupunguza ajali barabarani.
Mheshimiwa spika,
Ongezeko hili la faini ni kubwa sana na litawaangamiza kabisa
kibiashara vijana ambao wamejiajiri kwenye biashara ya usafirishaji
kama vile daladala, taxi, bajaji na pikipiki .
Kambi ya Upinzani inapinga marekebisho haya ya sheria kwani
yataathiri maisha ya watanzania wengi ambao watakuwa sasa kila
mara wanafanya kazi kwa ajili ya kulipia faini polisi badala ya
kuweza kukuza uchumi wao. Kwa mfano, kama dereva wa pikipiki
atakutwa na makosa matatu, mathalani la kusahau leseni, kutovaa
helmenti na kutovaa vazi maalum kwa ajili ya kuendesha pikipiki
atapaswa kutozwa faini ya shilingi 900,000 ambazo ni sawa na
24
gaharama ya kununua pikipiki nyingine mpya.
Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12 haijalenga katika kuimarisha
uchumi kwani fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ni kiasi cha
shilingi 4,925 trilioni tu na kati ya fedha hizo shilingi 1,871 trilioni ni
fedha za ndani na nyingine zilizobakia kiasi cha shilingi 3,054 trilioni ni
fedha za nje. Hivyo basi, kama wahisani hawatatoa fedha kama
ambavyo hali hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara ni kuwa
maendeleo hayataweza kupatikana kwani hakuna fedha kwa ajili
ya kuendesha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kambi ya Upinzani, inaona kuwa serikali bado haijaamua kuliondoa
taifa hili katika lindi la umaskini kwani hatutengi fedha zetu za ndani
kwa ajili ya maendeleo badala yake fedha za ndani tunatenga kwa
ajili ya shughuli za kawaida ambazo si za maendeleo.
BAJETI MBADALA YA KAMBI YA UPINZANI
Mheshimiwa Spika, zifuatazo ni dondoo za Bajeti Kivuli inayotolewa
na Kambi ya Upinzani Bungeni.
Dondoo za Bajeti Mbadala
• Kuongeza mapato hadi kufikia Shilingi trilioni 14.160 kutoka
trilioni 13.525 za Serikali.
25
• Tumeongeza mapato ya ndani hadi trilion 8.68 kutoka 6.7 za
serikali.
• Tumeondoa kukopa mikopo ya kibiashara na hii inatokana na
ukweli kwamba kufanya hivyo ni kuliongezea taifa gharama za
kulipa madeni yenye riba kubwa na pia hili linafanya uchumi
kuathirika kwani serikali inakuwa ikishindana na sekta binafsi
katika kuchukua mikopo kwenye taasisi za fedha na hivyo
kuathiri uchumi.
• Tumeondoa posho mbalimbali ambazo ni 0.987 trilioni na
kuzipeleka kwenye kuboresha Mishahara ya Watumishi wa
Umma na katika bajeti ya maendeleo.
• Tumepunguza matumizi ya kawaida ya serikali kutoka trilioni
8,600,286 na kuwa 7.913.
• Tunapendekeza kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya
umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme.
Vilevile kuchochea matumizi ya Gesi majumbani.
• Tutakusanya mapato ya ndani kwa 22.84% ya pato la Taifa
ukilinganisha na serikali ambao watakusanya 17%.
• Tumepunguza misaada na mikopo kutoka nje na kuwa 27.54 %
ya bajeti wakati ya serikali ni 29%.
• Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tumeongeza 1.905 trilioni
ambavyo ni vyanzo havikusanywi na serikali na kupanua wigo
wa kodi na kurekebisha sheria za kuzuia ukwepaji wa kodi (anti
tax avoidance measures) na kuboresha mfumo wa Kodi.
• Tunapendekeza kurahisisha mfumo wa kodi ya Mapato
(Personal Income Tax) na kwamba sasa kila Mtanzania ajaze
fomu za kodi (tax returns) kwa mujibu wa sheria hata kama
hana kipato.
SERA YA MAPATO .
Kuongeza mapato ya nchi kutoka katika bidhaa za misitu .
26
Mheshimiwa Spika ,
Katika kuhakikisha kuwa bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu
kama vile mbao , madawa, magogo na asali zinatumia kikamilifu
katika kuliongezea taifa kipato hatua zifuatazo zitachukuliwa ;
(i) Kuhakikisha kuwa Magogo yote yanayosafirishwa nje ya
nchi yanalipiwa kodi . Tunashauri kuimarisha usimamizi
bora wa uvunaji wa bidhaa hizi za misitu na kuifanya
idara ya Misitu na Nyuki kuwa Wakala wa Serikali. Juhudi
zitawekwa katika kuhakikisha kwamba Bidhaa nyingi za
Misitu zinatumika hapa nchini kuzalisha Fenicha kufuatia
amri ya kutonunua Fenicha kutoka ughaibuni.
(ii) Kutafuta soko la uhakika la asali kwa ajili ya kupata fedha
za kigeni kwenye masoko ya Ulaya na Marekani kwani
yametawaliwa na asali kutoka nchi za Amerika ya Kusini
kama Brazili na Argentina . Lengo la kuongeza juhudi
katika eneo hili ni kusaidia jamii za warina asali kupata
soko na nchi kufaidika na kodi na pia mauzo nje na hivyo
kupata fedha za kigeni.
kupunguza misamaha ya kodi.
Mheshimiwa Spika ,
Kiwango cha misamaha ya kodi zinazotolewa na Tanzania ni
kikubwa mno. Hii inaonekana wazi kwa kulinganisha kiwango cha
misamaha ya kodi kinachotolewa Tanzania na kile kinachotolewa
katika nchi za Uganda na Kenya. Nchini Tanzania kati ya miaka ya
2005/06 na 2007/08 misamaha ya kodi ilikadiriwa kuwa wastani wa
asilimia 3.9 ya pato la taifa. Mwaka 2008/09 misamaha ya kodi
ilikuwa asilimia 2.8 ya pato la taifa na mwaka 2009/10 asilimia 2.3.
Ukilinganisha na Kenya na Uganda misamaha ilifikia asilimia 1 na 0.4
ya pato la taifa la kila nchi husika kwa mtiririko huo.
27
Mheshimiwa Spika ,
Kama Tanzania ingerekebisha viwango vya misamaha ya kodi ili
kulingana na kiwango kilichofikiwa na Kenya, zaidi ya TZS 600 bilioni
zingeokolewa kwa mwaka 2007/08 peke yake. Ukubwa wa kiwango
cha misamaha inayotolewa unaweza kuelezewa kwa kukilinganisha
na malengo ya ukusanyaji wa mapato ya kodi ambayo Tanzania
inashindwa kuyafikia. Katika mwaka 2008/09 na 2009/10 Serikali
haikutimiza lengo lake la mapato kwa wastani wa TZS 453 bilioni kila
mwaka. Katika kipindi hicho hicho, misamaha ya kodi iliyotolewa
ilifikia wastani wa TZS 724 bilioni kwa mwaka. Mpaka mwaka 2011
mwezi Juni Msamaha wa Kodi unakadiriwa kuwa TZS 930 bilioni kwa
mujibu wa Taarifa ya TRA kwa kamati ya Fedha na Uchumi.
Kama misamaha ya kodi ingetolewa katika kiwango kinachofanana
na kiwango cha misamaha ya kodi inayotolewa Kenya, TZS bilioni
484 zingeokolewa mwaka 2008/09 na TZS bilioni 302 mwaka 2009/10.
Kwa maneno mengine, upungufu katika ukusanyaji wa mapato
ungepunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Kambi ya Upinzani inaipongeza Serikali kwa kukubali wazo la
kupunguza misamaha ya Kodi mpaka kufikia Asilimia moja ya Pato
la Taifa.
Mheshimiwa Spika hata hivyo Kambi ya Upinzani inapendekeza
kupitia upya vivutio vinavyotolewa na TIC kwa wawekezaji kwa
kupiga marufuku msamaha wowote wa kodi kwa bidhaa
zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.
Sekta ya madini na makampuni ya kimataifa (multinationals)
Mheshimiwa Spika ,
Katika tathmini ya Hali ya Uchumi 2010 tumeonyesha ni namna gani
ambavyo sekta ya Madini imekuwa haichangi mapato ya ndani.
28
Katika Mwaka huu wa Fedha Taifa letu litakusanya Tshs 99.5 Bilioni
kutoka katika Mrahaba kwenye Madini yanayochimbwa nchini
kwetu. Mapato haya ya Mrahaba kwa mwaka ujao ujao wa Fedha
ni aslimia 4.5 tu ya Mauzo ya Dhahabu peke yake nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Kwa Upande wa kodi nyingine zinazokusanywa
kutoka katika sekta ya Madini inakuwa ni vigumu kuweza kujua kiasi
gani twakusanya kwani Kampuni zote zalundikwa katika kapu moja
la Idara ya Walipa Kodi Wakubwa. Kwa takwimu za Mwaka
2009/2010 mapato yote ya kikodi pamoja na mrahaba na malipo
kwa mifuko ya Pensheni (ambayo sio kodi) katika sekta ya ya Madini
yalikuwa takribani shilingi 256 bilioni ambazo zilikuwa sawa na
asilimia 16 ya thamani ya mauzo ya Madini nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuna haja ya kuhakikisha Taifa linakusanya
mapato ya kutosha katika sekta ya Madini ili kuleta maendeleo ya
Wananchi wetu. Katika kuhakikisha kuwa tunaongeza ukusanyaji wa
Mapato ya kutosha kutokana na sekta ya Madini na makampuni ya
kimataifa tutachukua hatua kadhaa.
Mheshimiwa Spika,
Makampuni makubwa ya kimataifa (MNC) hutumia mbinu
mbalimbali kupunguza kodi wanazolipa kwenye nchi zinazoendelea.
Nchi yetu imekuwa ikikaribisha wawekezaji wakubwa kwenye
maeneo mbalimbali hasa sekta za Madini na Mawasiliano, hata
hivyo, kwa muda mrefu wa uwekezaji wao wamekuwa wakipata
misamaha ya kodi na pia kutolipa kodi ya makampuni ama kodi ya
“capital gains” wanapouziana makampuni hayo.
Mheshimiwa Spika,
Mfano mzuri ni wa kampuni za Madini ambazo hutumia sehemu
kubwa ya uwekezaji wao kama mkopo (debt financing), njia hii
29
huwezesha wawekezaji (shareholders) kupata faida (return)
mapema zaidi kuliko kuweka mtaji (share holders equity). Hii
inatokana na ukweli kwamba riba huondolewa katika kukokotoa
kodi ambayo kampuni hulipa. Katika kipindi cha kati ya mwaka
2001-2009 kiwango cha kodi ambacho kingelipwa serikalini iwapo
makampuni ya madini yangewekeza mtaji wa angalau 30% ya
uwekezaji kwenye migodi yao kingelikuwa takribani dola za
Kimarekani 830 milioni.
Mheshimiwa Spika,
Mifano ya asilimia ya mikopo katika Mitaji ya makampuni ya madini
hapa nchini ni kama ifuatavyo (Chanzo Masha Mining Review
Report);
(i) Geita Gold mine – 12,597,000 %
(ii) Bulyanhulu Gold mine – 791 %
(iii) Resolute Gold mine – 5088%
Mheshimiwa Spika,
Utaona kuwa kwa muundo huo wa mitaji ya Makampuni haya
matatu tu ni namna gani ambavyo sehemu kubwa ya Fedha
zinazotokana na faida wanayopata kwenye mauzo ya dhahabu
huishia kulipia Madeni na Riba na hivyo kukosesha Serikali mapato.
Hii kwa wataalamu wa kodi inaitwa ‘tax planning measures’.
Muundo huu wa mitaji ya uwekezaji itapelekea makampuni haya
kutangaza hasara kila mwaka.
Mheshimiwa Spika,
Vilevile kwenye sekta ya Mawasiliano, kampuni ya Celtel
International ilifungua kampuni huko Netherlands (Celtel Tanzania
BV) ambayo ndio inamiliki Celtel Tanzania limited. Hivyo uuzaji wa
Celtel kwenda Zain na baadaye kwenda Airtel haukulazimisha
kubadilishwa kwa mmiliki wa celtel Tanzania limited na hivyo kwa
30
kutumia mikakati ya kiumiliki (ownership structure) kila mara kampuni
hii ilipouzwa serikali haikuweza kukusanya kodi yake. Kwa mfano,
kwenye mauzo ya Zain kwenda Airtel serikali ingeweza kukusanya
dola za Kimarekani 312 milioni.
Mheshimiwa Spika,
Kwenye sekta ya Viwanda, Kampuni ya Bia Tanzania ambayo
inamilikiwa na SABMILLER nayo pia imeripotiwa kutumia njia ya
kimkakati kukwepa kodi ikiwemo kusajili hatimiliki na hivyo kupata
mrahaba ambao hautozwi kodi , mfano ni kwenye pombe aina ya
CHIBUKU ambapo jina hilo limesajiliwa huko Netherlands na
kampuni tanzu ya TBL. Inasemekana Tanzania imepoteza karibu dola
milioni 2 kila mwaka kutokana na mpango huo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani Bungeni tunapendekeza hatua zifuatazo ili
kuweza kukabiliana na ukwepaji huu wa kodi na hatimaye
kuliongezea taifa mapato;
(i) Kutunga sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya
Mapato ya mwaka 2004 kwamba, mikopo ya makampuni
kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi, isizidi asilimia 70
ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja bila
kujali mikataba iliyopo.
(ii) Kutunga sheria kuhakikisha kwamba Riba kwenye mikopo
kutoka Makampuni yanayohusiana haitaondolewa
kwenye kutoza kodi.
(iii) Kuhakikisha kwamba mauziano ya Kampuni yeyote
ambayo mali zake zipo Tanzania tunakusanya kodi ya
asilimia 30 % kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital gains’).
Kurekebisha Kodi za Mafuta
31
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapongeza hatua ya
Serikali kuchukua wazo la Kambi ya Upinzani la kupunguza
Kodi na tozo kwenye Bidhaa za mafuta ili kupunguza Bei ya
Bidhaa hizi na hivyo kupunguza ukali wa maisha kwa
wananchi. Ingawa Serikali haijasema kiwango cha kodi
kitakachoondolewa, tunapendekeza kuwa ushuru wa
barabara (road toll) usipunguzwe ili kubakia na Fedha za
kutosha kukarabati barabara ambazo tunazijenga kwa kasi.
Tunapendekeza Ushuru wa Bidhaa kwenye biadhaa za
Mafuta upunguzwe kwa asilimia 40 na tozo nyingine zote
kwenye mafuta zipunguzwe kwa asilimia 40 pia.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza pia kufuta kabisa
msamaha wa Kodi kwenye Mafuta kwa Kampuni za Madini
na Kampuni za Ujenzi kwani imethibitika kuwa msamaha huu
unapelekea upotevu mkubwa wa fedha za Umma. Takwimu
zinaonyesha kuwa kupitia misamaha hii jumla ya lita 133m za
Dizeli ambazo ni sawa na asilimia 20 ya Dizeli yote
iliyoingizwa nchini, ziliingizwa nchini na Kampuni 5 za Migodi
ya Dhahabu. na zililipa kampuni hizi zililipa dola laki mbili tu
kama ushuru. Mafuta mengi yanayoingia kupitia msamaha
huu hurudi kwenye sokona kuuzwa rejareja. Misamaha hii
ifutwe bila kujali mikataba iliyopo.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upizani Bungeni inapinga
pendekezo la sasa la kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta
kwa kampuni za utafutaji ya mafuta na Gesi. Msamaha huu
hauna mantiki kwani Kampuni za utafutaji mafuta na Gesi
kwa Mujibu wa Mikataba yao (Production Sharing
Agreements) wataweza kurejeshewa gharama hizi bara
baada ya mafuta na Gesi kupatikana (Cost Oil).
32
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema hapo juu hatua hii ya
kikodi ni ya dharura tu kwani bado inaweza kufanywa haina
maana yeyote kwa kitendo cha bei za mafuta kupanda
katika soko la Dunia. Hivyo tunahitaji njia endelevu nayo ni
kuhakikisha Mafuta yanaagizwa kwa wingi na hivyo
kupunguza gharama za usafirishaji. Mpango wa Bulk
Procurement umekuwa ukisemwa bila kutekelezwa kwa
muda mrefu kutokana na nguvu kubwa ya rushwa
waliyonayo matajiri katika sekta ya Mafuta. Ni lazima
tuishinde nguvu hii hata kama itakuwa ni kwa baadhi yetu
kupoteza maisha.
Mheshimiwa Spika Kambi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza Serikali kupitia Shirika la Umma la Mafuta
(baada ya kurekebisha TPDC na kuwa na Mamlaka ya
Udhibiti katika kutafuta na kuchimba mafuta na Gesi na
Shirika la Kibiashara la Mafuta na Gesi), inunue hisa asilimia
50 zilizobakia za BP (T) Limited, kuweka mtaji wa kutosha na
kufanya biashara ya Mafuta. Nchi nyingi Duniani hutumia
Mashirika yake ya Umma kwenye sekta ya Mafuta kudhibiti
Bei. Ukienda Dubai Leo vituo vingi vya Mafuta vinamilikiwa
na Shirika la Umma. Vilevile Malaysia licha ya Petronas
kushirika katika kuchimba Mafuta lakini pia inamiliki vituo vya
mafuta vya rejareja. Hii ndio hatua mwafaka ya kuchukua,
ipo ndani ya uwezo wetu na itaongeza Ushindani katika
soko na hivyo kudhibiti upandaji wa bei holela wa bidhaa za
mafuta. Kwa ufupi tunashauri BP (T) Limited imilikiwe na
Serikali kupitia Shirika la Umma kwa asilimia 100 badala ya
asilimia 50 ya sasa.
33
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza pia kuwianisha viwango vya bei ya Mafuta
ya Taa na bei ya Mafuta ya Diseli na Petroli ili kudhibiti
uchakachuaji wa mafuta ambao unaligharimu Taifa fedha
nyingi sana na kuleta uharibifu mkubwa sana.
Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa Spika, kupanda kwa gharama za maisha kwa
Wananchi kumepunguza uwezo wa matumizi wa wananchi
walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa kodi
(PAYE). Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha
Mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha
kinatarajiwa kuingiza takribani shilingi 450 bilioni kutoka idara
ya Kodi za Ndani na Idara ya Walipa kodi wakubwa. Hata
hivyo kuna haja ya kuangalia upya (tax brackets) na
kuzirahisisha kwa kuzipunguza na hata kuanza kufikiria kama
kuna haja ya kuwa na flat tax.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa Fedha
tunapendekeza Sheria ya Kodi ya Mapato ifanyiwe
marekebisho na kushusha kiwango cha chini kabisa cha
PAYE mpaka asilimia 9 na kiwango cha juu mpaka asilimia
27. Uamuzi huu utawezesha wananchi kubakia na fedha na
hivyo kutumia katika uchumi na kukuza uzalishaji. Uamuzi
huu utapunguza mapato ya Serikali kwa takribani shilingi
bilioni 23 (asilimia 4 ya matarajio ya makusanyo ya kodi hii).
Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi ya Upinzani
inapendekeza kuwa mchakato uanze ili kila Mtanzania awe
34
anajaza fomu za kodi (tax returns) kila mwaka. Kuna watu
wengi sana ambao wanapata mapato makubwa lakini
hawalipi kodi. Mfano, watu wenye nyumba za kupangisha
mijini wanapata fedha nyingi sana na wengine hutoza kodi
kwa kutumia dola za Marekani lakini hawalipi kodi ya
Mapato. Watu hawa hutumia Barabara na huduma
nyingine za Umma ambazo gharama zake zatokana na kodi
ilhali hawalipi kodi. Kambi ya Upinzani inapendekeza
kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority na
kwamba kila mwenye Nyumba ya kupangisha lazima
atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili.
Mheshimiwa Spika, ninataka kila Mtanzania mwenye kipato
alipie kodi ya kipato chake. Kulipa kodi ndio ishara ya
Uzalendo na ili raia aweze kuinyooshea kidole serikali yake
lazima awe na uchungu na uchungu unapatikana kwa
kulipa kodi.
Kurasimisha Biashara ndogo ndogo
Mheshimiwa Spika, moja ya hatua ambayo imekuwa ikizungumzwa
siku zote ni kupanua wigo wa kodi. Waheshimiwa wabunge wa
kambi zote mbili na hata wataalamu mbali mbali wanarejea sana
jambo hili. Imefikia wakati sasa kutekeleza jambo hili kwa vitendo
kwa kuondoa vikwazo vinavyofanya Biashara ndogo na za kati
(SMEs) zisiandikishwe. Biashara ndogo na za kati zinaunda sehemu
kubwa ya shughuli za kiuchumi nchini na hivyo kuwa moja ya
chanzo kikubwa cha Mapato ya Serikali. Katika utafiti uliofanywa na
Shirika la Serengeti Advisers Limited imeonekana kuwa licha ya
maboresho yanayofanywa na TRA bado wafanyabiashara wadogo
na wa kati wanakutana na vikwazo vingi sana. Baadhi ya vikwazo ni
35
pamoja na vitisho kutoka kwa maafisa wa TRA, urasimu na hata
Rushwa. Pamoja na vikwazo hivyo bado SMEs zimekuwa zikichangia
kwa kiasi kikubwa kupitia kodi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza
kwamba ushauri wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi (Tax
Modernisation Project) ambao ulishauri kwamba kuna haja ya
kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive Tax utekelezwe. Tungeshauri
kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara ndogo ndogo kabla
hajaanza kufanya biashara ifutwe kabisa. Uamuzi huu utapunguza
mapato ya Serikali (Shilingi 18 bilioni kwa mujibu wa Kitabu cha Bajeti
Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa ni chanzo
kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.
Ada ya Leseni za Biashara
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni inaona kurejeshwa kwa leseni kwa
biashara ndogo ndogo licha ya kuongeza mapato ya Halmashauri
za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kutarejesha ugumu wa kufanya
biashara. Madhumuni ya kuondoa leseni yaliyofanywa mwaka 2003
bado yana maana. Tunashauri uamuzi huu uangaliwe upya.
Msamaha wa Kodi kwenye Nyaya za Umeme
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inapendekeza kufutwa kwa msamaha wa kodi
kwenye orodha ya misamaha kwa nyaya za Umeme (Removal of
duty remission on electric wires and cables (as deemed capital
goods) through Tanzania Certificate of Incentive scheme
administered by TIC). Uamuzi huu utalinda viwanda vya ndani na
36
kulinda ajira za Watanzania walioajiriwa kwenye viwanda
vinavyotengeneza nyaya za umeme.
Muhtasari wa vyanzo nyongeza vya mapato kwa bajeti mbadala
2011/2012 (Shilingi)
1. Kurekebisha Kodi katika Misitu
100bn
2. Kurekebisha misamaha ya kodi
555bn
3. Mauzo ya hisa za Serikali 550bn
4. Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini 240bn
5. Kuimarisha usimamizi wa mapato ya Wanyamapori
81bn
6. Kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta Kampuni za Madini
59bn
7. Usimamizi wa Mapato katika Utalii
68bn
8. Kuimarika kwa Biashara na EAC 150bn
Jumla 1905bn
SERA YA MATUMIZI
Vipaumbele vya bajeti ya Matumizi.
(i) Ukuaji wa uchumi vijijini (rural growth) kwa kuboresha
miundo mbinu ya umeme, barabara na maji.
Tunapendekeza kutumia shilingi 450 bilioni kila mwaka
(Bilioni 150 kwa kila sekta) kwa miaka 5 mfululizo katika
sekta hizi vijijini. Ujenzi wa barabara za vijijini utatumia kwa
kiasi kikubwa nguvukazi watu (labour intensive) ili
kuongeza kipato na kukuza matumizi ya Kaya vijijini kufikia
37
lengo la kupunguza umasikini wa vijijini mpaka asilimia 20
kutoka asilimia 37 ifikapo mwaka 2015.
(ii) Ujenzi wa barabara na madaraja
(iii) Nishati (umeme na gesi asilia) kuhakikisha tunazalisha
360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya
Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano. Pia kuwekeza
katika Bomba la Gesi kutoka Mtwara, matumizi ya Gesi
kwenye nyumba za Dar es Salaam na mtambo wa
kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant).
(iv) Rasilimali watu (kuboresha Elimu na afya)
(v) Kuongeza Kima cha chini cha Mshahara kwa
Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi
na kutoa motisha kwa Walimu wanaofundisha Vijijini kwa
kuwapa Mshahara mara moja na nusu ya wenzao
wanaofundisha mijini.
(vi) Uchukuzi (reli, bandari na Shirika la ndege )
(vii) Kujenga Uwezo wa Wakandarasi wa ndani kwa
kurekebisha Sheria mbalimbali ili kuhakikisha kuwa (i)
miradi yote ya Ujenzi nchini isiyozidi shilingi 30 bilioni iwe ni
kwa ajili ya Watanzania tu na kama Mtanzania hana
uwezo ataalika mgeni kwa mapenzi yake. (ii)Miradi yote
ya Ujenzi inayozidi Shilingi 30 bilioni itakuwa wazi kwa
zabuni za ndani na nje hata hivyo Kampuni ya kigeni
itayayopata Zabuni ni lazima iwe na ushiriki wa Mtanzania
kwa angalau asilimia 30 na (iii) Vifaa vyote vya ujenzi na
hasa vile vinavyozalishwa nchini vinunuliwe nchini na
itakuwa ni marufuku kwa Kituo cha Uwekezaji kutoa
ruhusa ya msamaha wa kodi kwa makampuni ya
uwekezaji kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na hasa
Saruji. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha fedha za miradi
mikubwa ya Maendeleo ya Ujenzi zinabaki nchini na
38
kuchochea ukuaji wa Uchumi wa Watanzania, kuongeza
ajira na uzalishaji viwandani.
(viii) Pensheni ya uzeeni.
(ix) Kuondoa ada Kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari za
Kutwa na kupunguza ada kwa sekondari za Bweni kwa
kiwango cha asilimia hamsini kwa wavulana na bure kwa
wasichana. Kwa kuwa kuna wanafunzi 1.6m katika shule
za Sekondari nchini, gharama za shilingi 32 bilioni
zitakazopotea zitalipwa na Serikali kutoka vyanzo vipya
vya mapato.
(x) Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo zilizoongezewa
ubora.
(xi) Kupunguza mzigo wa Matumizi ya Magari ya Serikali kwa
kuweka mfumo wa Viongozi na watumishi ambao stahili
zao zinapaswa kupewa magari watakopeshwa magari
na kupewa posho ya mafuta. Magari kadhaa yatawekwa
‘pool’ na mengine yote yatapigwa mnada. Benki Kuu ya
Tanzania tayari inatumia mfumo huu ambapo hata
Gavana wa Benki Kuu sasa amekopeshwa gari.
Tunatumia uzoefu wa Taasisi hii ya Serikali kwa Idara zote
za Serikali, Mawizara,Mikoa,Mashirika ya Umma
yanayopata Ruzuku ya Serikali na Serikali za Mitaa
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO.
Mheshimiwa Spika,
Kama taifa tumezindua mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka
mitano 2011/2012 – 2015/2016 na jana bunge lako tukufu
limeupitisha pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na
waheshimiwa wabunge.
Mpango unahitaji wastani wa Shilingi Trilioni 8.6 kila mwaka ili
39
kuutekeleza, na fedha zote hizi za utekelezaji wa mpango huu ni
fedha za bajeti ya maendeleo. Katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa
Fedha Mh. Mkullo bajeti ya maendeleo ni Shilingi Trilioni 4.9 tu
ambayo ni sawa na asilimia 36.3 ya bajeti yote ya serikali kwa
mwaka huu.
MheshimiwaSpika, ili kuanza kutekeleza mpango wa maendeleo
kuanzia mwaka huu wa fedha, na iwapo tungesema fedha zote za
maendeleo mwaka huu zitekeleze mpango huu, ingekuwa ni
asilimia 56.9 ya fedha zinazohitajika kuutekeleza mpango kwa
mwaka. Hii inaonyesha kuwa serikali haina nia ya dhati ya
kuutekeleza mpango huu wa kitaifa. Kushindwa kutenga fedha za
kutekeleza mpango huu kwa mwaka huu, kutapeleka mzigo
mkubwa wa bajeti ya mpango huu katika mwaka ujao wa fedha.
Kambi ya upinzani inaona kuwa kuna ulazima wa kuanza kutekeleza
baadhi ya miradi ya maendeleo katika mwaka huu wa fedha.
1. Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa fedha Mhe. Mustafa Mkullo
akitaja kuwa kipaumbele cha kwanza cha bajeti ya mwaka huu
ni kumaliza tatizo la Umeme na hivyo kutamka kwamba
ametenga shilingi 537 Bilioni, upembuzi uliofanywa na Kambi ya
Upinzani kwenye vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV fungu la
58) vilivyotolewa na serikali, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na
Madini imetengewa jumla ya shilingi 402.4 bilioni. Fedha hizo
zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi ya kawaida shilingi
40
76.95 bilioni na kwa upande wa bajeti ya Maendeleo
zimetengwa shilingi 325.4 bilioni. Shilingi Bilioni 325 zilizotengwa
katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini
zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160MW, 100 Dar es
Salaam na 60 Mwanza. Hakuna mradi wowote mpya wa umeme
unaoonekana katika Bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya mpango wa kwanza wa
maendeleo wa miaka mitano, katika uzalishaji umeme ambapo
kama taifa tumepanga kuzalisha megawati 1788 za ziada kutoka
MW 1034(installed capacity) zilizopo sasa, tunahitaji kuzalisha
wastani wa MW 358 kila mwaka kwa miaka mitano. Hivyo basi,
ukiondoa mradi wa MW 160 ambao tayari umeanza na
umetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu, tunahitaji mradi
mwingine wa angalau MW 200 ndani ya mwaka huu wa fedha.
Mradi ambao unaweza ukatekelezwa kwa haraka ni mradi wa
Kiwira awamu ya kwanza MW 200.
Taasisi za NSSF na STAMICO zimeonyesha nia ya kutekeleza mradi
huo bila ya kutegemea fedha ya bajeti ya serikali. Kambi ya
Upinzani inapendekeza mradi huu kuingizwa katika utekelezaji
ndani ya mwaka huu wa fedha. Kambi ya Upinzani pia
inapendekeza kutenga fedha za ndani kutekeleza mradi wa njia
za kusafirisha umeme huu kutoka Kiwira mpaka Mbeya na
usambazaji huu utekelezwe na TANESCO.
41
Mheshimiwa Spika, miradi iliyosalia ya Mchuchuma na Ngaka
(Makaa ya Mawe), Mtwara – Somanga Fungu na Kinyerezi ( gesi
asilia) na Ruhudji (Maji) ielekezwe kwa taasisi zilizoainishwa kwa
ajili ya utekelezaji na serikali kuingia makubaliano na taasisi hizo ili
kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, madhara ya ukosefu wa umeme kwenye
Uchumi wa Taifa ni makubwa sana. Mamlaka ya Mapato
Tanzania ilinukuliwa kusema kuwa Mgawo wa Umeme uliotokea
mwanzoni mwa mwaka huu unaweza kuikosesha mapato ya
zaidi ya Shilingi 840 bilioni. Tumeona juhudi za Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini katika kutafuta ufumbuzi wa Tatizo la Umeme
lakini juhudi hizi hazionekani upande wa Serikali na hasa Wizara ya
Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, Imefikia wakati sasa kutangaza kuwa Umeme
ni janga la Taifa na kwamba Bunge lipitishe Azimio la Uzalishaji wa
Umeme kwa viwango vya Mpango wa Maendeleo na kuweka
adhabu ya kumfukuza kazi Waziri iwapo miradi hiyo haitakuwa
imekamilika kila mwaka. Kamati ya Bunge na Nishati na Madini
iwe inatoa Taarifa mara mbili kwa mwaka (Bunge la Mwezi wa
Novemba na Bunge la Mwezi Februari) kuhusu maendeleo ya
Miradi ya Umeme na kama malengo hayajafikiwa Kamati itoe
Azimio la kutokuwa na imani na Serikali.
42
Uwekezaji kwenye Gesi Asilia
Mheshimiwa Spika, Inafahamika kuwa nchi yetu imejaaliwa kuwa
na Gesi asilia nyingi sana. Tafiti zinaonyesha kuwa hivi sasa kuna
zaidi ya 12tr cf ya Gesi na utafutaji bado unaendelea. Ndani ya
Miaka michache ijayo nchi yetu itakuwa moja ya mataifa
makubwa yenye Gesi asilia nyingi sana. Hata hivyo hali hii
haionekani katika mipango ya Serikali na viongozi wa kisiasa na
hata wataalamu hawaliandai Taifa kwa hali hii. Madhara yake ni
kuwa itakapofika siku ya siku tutaingia kwenye migogoro kama
tuliyoshuhudia katika sekta ya Madini. Kambi ya Upinzani
inashangazwa na habari kwamba toka Gesi ya Mkuranga
igunduliwe mwaka 2007 mpaka sasa hakuna mradi wowote
umeanzishwa kunyonya gesi hii na kuitumia kuzalisha utajiri kwa
Taifa. Tunapendekeza kuwa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Gesi
kutoka Mtwara ambalo pia litapita Mkuranga uwe ni kipaumbele
cha juu kabisa cha nchi. Mradi huu utekelezwe kwa nguvu kama
ilivyokuwa kwa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria. Bomba hili
lijengwe kwa kushirikiana na Sekta Binafsi na lifike Tanga na
Mwanza ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo. Ni lazima
tuamua mambo makubwa na tuyafanye. Hili tunaweza kulifanya
na tulifanye.
Mheshimiwa Spika, katika suala hili la kuandaa Taifa kwa ajili ya
kuwa Taifa lenye kuzalisha Gesi na Bidhaa zitokanazo na Gesi,
43
Kambi ya Upinzani inashauri kuwa Tuanzishe Chuo Kikuu Cha
Mtwara. Chuo hiki kijikite kuwaandaa Watanzania katika
utaalamu wa utafutaji, uchimbaji na usimamizi wa sekta ya
Mafuta na Gesi.
Mheshimiwa Spika, moja ya njia ya kupunguza matumizi ya
umeme majumbani na hivyo kuhakikisha umeme wa kutosha
unabakia kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji viwandani, Kambi ya
Upinzani inapendekeza kwamba miradi miwili muhimu ya gesi
kwa ajili ya matumizi ya majumbani ianze ndani ya mwaka huu
wa fedha; nayo ni:
Mradi wa gesi ya LPG kwa ajili kujaza gesi kwenye mitungi na
Mradi wa kusambaza gesi majumbani katika jiji la Dar es salaam.
Miradi yote hii itatekelezwa na shirika la maendeleo ya gesi na
mafuta nchini TPDC. Hata hivyo Kambi ya Upinzani inakumbushia
pendekezo la kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kuhusu
kuifanyia marekebisho TPDC kwa kuigawa na kuunda mamlaka
ya mafuta na gesi ambayo itahusika na kutoa vibali na leseni na
kusimamia utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi (upstream
regulator) na kampuni itakayohusika na biashara ya mafuta na
gesi.
Ukuzaji wa Uchumi Vijijini
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kuwa Uchumi wa Nchi yetu umekuwa
ukikua kwa kasi ya kuridhisha katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Hata hivyo ukuaji huu wa uchumi haujaweza kupunguza umasikini
44
wa Watanzania kwa kiwango cha kuridhisha na cha kujivunia. Mara
mbili viongozi wetu wakuu wa nchi (Rais na Waziri Mkuu)
wamehojiwa na vyombo vya habari na kukiri kuwa hawajui kwa nini
Watanzania ni masikini. Kwa wachumi wengi na kwa kasi hii ya
ukuaji wa uchumi jibu ni hilo hilo. Kwamba unakuwaje na Uchumi
unaokua kwa wastani wa asilmia 7 kwa miaka kumi bila kuounguza
Umasikini ni kitendawili na chemsha Bongo. Nina imani kubwa
kutokana na Tafiti mbalimbali kwamba kwa miaka kumi
hatujawekeza vya kutosha katika uchumi wa vijijini na ndio maana
hatuoni faida za uchumi wetu kukua. Uwekezaji mkubwa na hasa
uliofanywa na sekta binafsi umekuwa ukifanywa katika uchumi wa
mijini. Serikali inapaswa kufanya uamuzi wa makusudi kuwekeza
katika miundombinu ya uchumi wa vijijini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani kupitia bajeti hii mbadala
imeleta mapendekezo ambayo inaamini kuwa kwa kiasi kikubwa
kwa kipindi cha miaka mitano ijayo itasaidia kujibu kitendawili hiki na
itaondoa matatizo makubwa yanayotukabili ya umasikini uliokithiri
vijijini na kusababisha vijana wengi kukimbilia mijini.
Mheshimiwa Spika, Katika mkakati wetu wa kufanikisha mpango wa
kuondoa umasikini ni kuzifanya Halmashauri zetu za Wilaya
kutayarisha kitu kinachoitwa “District Economic Development Master
Plan” yaani Mpango Mama wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Wilaya
ambapo kila halmashauri kupitia mpango wake kutengeneza ajira
zisizopungua 2000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, Mpango huu utasaidia kuondoa dhana ambayo
imeenea kwa watendaji ngazi za mikoa na wilaya kukaa mkao wa
kupokea fedha na kutumia tu toka Serikali kuu. Mikoa na wilaya
zitatumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuondoa matatizo
yanayowakabili wananchi wao kuliko kusubiri kupelekewa
wawekezaji toka kituo cha uwekezaji, ambapo Halmashauri
zingeweza kuingia ubia na mwekezaji husika.
45
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika kufanikisha mpango
huo tumeleta vipaumbele sita (6) na kila kipaumbele kitasaidia
kuinua uchumi wa wananchi waishio vijijini.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa baadhi ya vipaumbele ambavyo
tumevipanga na Serikali imeleta hivyo hivyo, tofauti iliyopo ni jinsi ya
kuvitekeleza ili viweze kuleta tofauti kwa uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, Kipaumbele chetu cha muhimu ni Kuwezesha
Ukuaji wa Sekta za Uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi wa vijijini
(rural growth). Kambi ya Upinzani inakichukulia kipaumbele hiki
kama tiba halisi ya kuwaondolea umasikini Watanzania waishio vijijini
kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaoishi vijijini maisha
yao yanaendeshwa na shughuli zinazohusiana na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Katika kutimiza azma ya kuinua maisha yao,
miundombinu ya barabara na umeme itasababisha ujenzi wa
viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani za bidhaa
zizalishwazo vijijini, ni dhahiri pia asasi za fedha zitaenda zenyewe na
pia itasaidia kupunguza uhamiaji wa kutoka vijijini kwenda mijini
(“rural urban migration”) kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kwa njia hii
tutafanikiwa kuondoa umasikini uliokithiri na pia kuiondoa nchi yetu
kwenye hatari ya kuwa taifa la wachuuzi. Pendekezo kubwa katika
kuchochea ukuaji wa uchumi wa Vijijini ni la kupeleka vijijini shilingi
450 bilioni kila mwaka kwa miaka mitano mfululizo katika sekta za
Barabara za vijijini, Umeme vijijini na Maji vijijini. Fedha hizi
zitagawiwa kwa Halmashauri za Wilaya (sio miji, manispaa na majiji)
kulingana mahitaji ya sekta husika kwa Wilaya husika ya Vijijini.
46
Tunaweza kufikiria kuanzisha Mamlaka ya Maendeleo Vijijini (Rural
Development Authority) ambayo itasimamia Mpango huu
utakaotekelezwa na Halmashauri za Wilaya chini ya Ofisi ya Waziri
Mkuu.
Bandari
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Tanzania inatumia vizuri fursa
ya jiografia yake ya kuwa na ukanda mrefu wa bahari Kambi ya
Upinzani itahakikisha upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na
Tanga kwa kutumia Ushirikiano wa Sekta Binafsi na ya Umma –
Private Public Partnership (PPP) unakamilika haraka ikiwa ni pamoja
na kuimarisha bandari ya Mtwara. Kwa njia hii tutawavutia
wafanyabiashara wa nchi ambazo hazina bandari kupitisha mizigo
yao katika bandari yetu.
Reli
Mheshimiwa Spika, Reli ya Kati ni kichocheo kikubwa sana cha
uchumi kwa wananchi wanaoishi mikoa iliyopo kando kando ya reli
hiyo, pia kuwa kiunganishi kikubwa kati ya bandari na nchi ambazo
hazina bandari, hivyo basi jambo la kwanza ni kuiboresha reli ya
sasa ili ifanye kazi kwa uwezo mkubwa kusafirisha abiria na mizigo
mpaka hapo fedha za kujenga Reli mpya yenye mataruma ya
kisasa itakapopatikana. Ili kutimiza adhima hiyo tumetenga kiasi cha
Tsh.100bn kuliwezesha shirika la Reli Tanzania kufanya kazi yake ya
msingi ya kusafirisha Mizigo na Abiria . Hata hivyo uendelezaji wa
Mradi wa Mchuchuma na Liganga unataka kuwepo kwa Reli
itakayounganisha Wilaya ya Ludewa na Bandari ya Mtwara. Kambi
ya Upinzani inapendekeza kuwa Upembuzi yakinifu wa Reli hii kama
ulivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa uanze
kufanyika mwaka huu na mchakato wa Ujenzi wa Reli hii uanze
47
sambasamba na kuanza kwa mradi wa kuchimba Chuma na
Makaa ya Mawe.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usafiri wa anga ambao ni
kiunganishi kikubwa kati ya watanzania na wale wa-ughaibuni na
kichocheo kikubwa cha utalii. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani
itahakikisha Shirika letu la Ndege linarudi tena kwenye biashara.
Tumeweka Tshs. 200bn. Kulifufua upya shirika la ndege la ATC. Hata
hivyo, tunashauri kwamba Serikali iangalie uwezekano wa
kurekebisha umiliki wa Shirika la Ndege la Taifa kwa kuhusisha Taasisi
za Umma ambazo zinafaidika na kuwepo kwa Shirika mara moja.
Kwa mfano, Shirika la Ndege linatarajiwa kukuza utalii wa nchi hivyo
Mashirika kama TANAPA na NCAA yanaweza kuelekezwa kuwekeza
mtaji katika Shirika la ATCL na kumiliki asilimia zisizozidi 30 za Shirika.
Badala ya Mashirika haya kupeleka tozo ya asilimia 10 ya mapato
yao Hazina, fedha hizi zaweza wekwa ATCL kwa kipindi cha miaka
kadhaa na hivyo kulirejesha Shirika katika Biashara. Tunashauri wazo
hili liangaliwe kiufundi kama linaweza kuleta tija.
Usimamizi wa mashirika ya umma
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na
Serikali katika hatua za kuiimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze
kusimamia vema Mashirika ya Umma. Ni wazi kwamba kuna
Mashirika ya Umma ambayo iwapo yakisimamiwa Vizuri yataweza
kufanya kazi kwa faida na hivyo kuondoa mzigo wa ruzuku za Serikali
kwenda kwa Mashirika ya Umma. Vile vile Kambi ya Upinzani
48
Bungeni inapongeza pendekezo la Kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji
wa Taifa kwa ajili ya kutoa Mitaji kwa Mashirika ya Umma. Hatua hii
itasaidia sana.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza
kufanya Marekebisho ya Sheria zifuatazo katika Finance Bill kwa ajili
ya kuboresha ufanisi wa Mashirika ya Umma. Sheria ya Mashirika ya
Umma ya mwaka 1992 ili kuiboresha na kutamka wazi wazi mamlaka
ya Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kusimamia Mashirika ya Umma
ambayo Serikali ina hisa zaidi ya Asilimia Hamsini ikiwemo kutoa
Mamlaka kwa Msajili wa Hazina kusimamia Waraka anazotoa kwa
Mashirika na pia kutungwa kanuni zitakazopelkea kuwepo kwa
Mfumo wa Maadili ya Utawala Bora (CODE OF CORPORATE
GOVERNANCE FOR PUBLIC CORPORATIONS).
Mheshimiwa Spika, tunashauri Sheria iliyounda Consolidated
Holdings ifanyiwe Marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka
2011 ili kulipa Uhai wa moja kwa moja Shirika hili na vile vile kupewa
Majukumu ya Kusimamia Mashirika ya Umma ambayo Serikali ina
hisa chini ya asilimia 50. Lengo la pendekezo hili ni kuhakikisha kuwa
Hisa za Serikali katika Makampuni binafsi zinasimiwa ipasavyo na
kwamba CHC iwe kweli ni Holding Company ya Serikali kwa hisa hizi.
Kwa sasa hisa hizi zinasimamiwa na Msajili wa Hazina. Pendekezo
letu ni kutenganisha majukumu haya ili kuleta ufanisi na hasa
ukizingatia kuwa CHC bado itakuwa inamilikiwa na Msajili wa Hazina
49
kwa asilimia 100. Uamuzi huu ukitekelezwa utarahisisha sana Kamati
ya Bunge ya Mashirika ya Umma kuwa na jicho la kiusimamizi kwa
kwa mitaji ya Serikali kwenye Kampuni binafsi kwani CHC hutokea
mbele ya Kamati ya POAC baada ya kukaguliwa na CAG.
Pensheni kwa wazee
Mheshimiwa Spika, Tanzania ina mfumo mzuri wa pensheni kwa
wastaafu ambao unasimamiwa na Mifuko Kadhaa ya Pensheni
hapa nchini. Hata hivyo kuna changamoto kubwa kwamba Serikali
inadaiwa fedha nyingi na mifuko hii hali ambayo tunadhani
inahatarisha maisha ya wastaafu. Kwa mfano, Serikali inadaiwa na
Shirika la PSPF na iliahidi kuanza kulipa Deni la Shilingi 700 bilioni lakini
bado haijalipa. Vile vile Serikali bado haijasaini mkataba wake na
Shirika la NSSF kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Tunashauri
Serikali itemize wajibu wake huu ili kuifanya mifuko iendelee
kutumikia Taifa na kuwekeza kwenye miradi mikubwa kwa
maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Tunashauri pia kuwa Serikali iangalie uwezekano
wa kufanya marekebisho katika Mfumo wa Pensheni na
kuunganisha mifuko iliyopo na kubakia na mifuko miwili tu, mmoja
kwa ajili ya Sekta ya Umma na Mwingine kwa ajili ya Sekta Binafsi na
sekta isiyo rasmi. Hivi sasa nchini kuna jumla ya wanachama
1,073,444 kwenye mifuko ya Pensheni (NSSF – 506,218. PSPF – 298,046.
PPF – 160,068. LAPF – 73,833 na GEPF 35,279) ambayo ni sawa na
asilimia 2.4 tu ya Watanzania wote. Hiki ni kiwango kidogo sana
50
kuhudumiwa na mifuko mitano ya Hifadhi ya Jamii. Vile vile
tunapendekeza kiwango cha chini cha Pensheni kifikie Shilingi 50,000
na kwa maana hiyo Shirika la PSPF lipandishe Pensheni kutoka 20,000
za sasa. Tunawapongeza NSSF kwa kulipa 80,000 na PPF kwa kulipa
50,000.
Mheshimiwa Spika, Licha ya Udhaifu huu wa Pesheni kwa Wazee
wetu waliotumikia utumishi wa Umma kuwa kidogo pia Tanzania
haina mfumo wa Pensheni kwa Wazee bila kujali kama walikuwa
waajiriwa kwenye Serikali au Mashirika ya Umma. Wazee wakulima
ambao wamechangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi kupitia
kilimo hawamo kwenye mfumo wa Pensheni na hivyo kusababisha
kero kubwa kwa wazee wengi ambao ndio wanalea wajukuu huko
vijijini kufuatia vijana wao wengi kupoteza maisha kwa magonjwa
kama Ukimwi.
Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuanzishwa kwa Pensheni
kwa Wazee wote nchini walio na umri wa zaidi ya miaka 65 na
ambao hawamo katika mfumo wa Pensheni. Kuna Jumla ya Wazee
1,362,435 ambao ni sawa na asilimi 3.2 ya Watanzania wote. Wengi
wa Wazee hawa wapo vijijini na ndio walezi wa wajukuu zao
kufuatia janga la Ukimwi. Itatakiwa kutenga Shilingi 280 bilioni kila
mwaka kwa ajili hii. Ni fedha nyingi lakini muhimu kulinda Wazee
wetu ambao wamelitumikia Taifa letu ama kwa kulima, kufuga,
kuvua au hata kwa kutulea tu. Maelezo ya ziada kuhusiana na
51
mfumo huu wa Pensheni atayatoa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira
atakapokuwa anawasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu
Wizara husika.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Baada ya Maelezo hayo sasa napendekeza
Sura ya Bajeti ya Nchi iwe kama inavyoonekana katika Jedwali hili
hapa chini. Naomba Bunge lako tukufu lijadili Hoja ya Waziri wa
Fedha kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa
kuzingatia maoni haya ya Kambi ya Upinzani Bungeni.
SURA YA BAJETI MBADALA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012
MAPATO Tshs. Bilioni
Mapato ya Ndani 8,681.
Mapato ya Halmashauri 351.
Mikopo na Misaada ya nje 3,924.
Mikopo ya Ndani 1,204.
JUMLA YA MAPATO 14,160
MATUMIZI Tshs.Bilioni
Matumizi ya Kawaida 7,913
Matumizi ya Maendeleo
i. Fedha za Ndani:- 3,193
ii. Fedha za nje:- 3,054 6,247
JUMLA MATUMIZI 14,160
52
Mheshimiwa Spika,
Mmoja wa viongozi katika Duniani ninaowaheshimu sana ni pamoja
na Tun Dr Mahathir Mohamad, Waziri Mkuu Mkuu wa zamani wa nchi
ya Malaysia na rafiki mkubwa wa Mwalimu Nyerere. Ninapenda
kumaliza Hotuba yangu kwa kunukuu maneno yaliyopo ukurasa wa
nyuma wa Kitabu chake ‘A doctor in the house’. Nanukuu ‘……
Viongozi wachache wameweza kubadili uchumi wa nchi zao kutoka
uchumi unaotegemea kilimo tu mpaka kuwa na uchumi wa
viwanda - wachache zaidi wameweza kufanya hivi katika kipindi
cha miongo miwili tu.’
Dr Mahathir aliposhika madaraka ya nchi yake mwaka 1981,
Malaysia ilikuwa ni nchi ambayo zaidi ya nusu ya Raia wake (asilimia
56) wakiishi katika dimbwi la umasikini. Alipoachia madaraka mwaka
2003 Malaysia ikawa na asilimia 3 tu ya Raia wake wanaoishi katika
dimbwi la umasikini.
Mheshimiwa Spika,
Malaysia iliweza kwa sababu Viongozi waliweza kuwa na mwono
wa mbali, kufanya maamuzi na kuyasimamia maamuzi hayo.
Ninaamini kuwa Tanzania inaweza kufanya vizuri zaidi ya Malaysia
kama sisi sote kama viongozi tukiamua kuweka maslahi ya nchi
mbele, kuweka malengo makubwa, kufanya maamuzi na
kutekeleza maamuzi hayo.
53
Kila mtu akitimiza wajibu wake, Tunaweza.
Tukiacha kuwa Taifa la walalamikaji, Tunaweza.
Tukiendeleza Umoja wa Kitaifa, mshikamano na kulinda Haki za raia,
Tunaweza.
Ninaamini, Tunaweza!
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi

Monday, June 13, 2011

HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI-MPANGO WA UCHUMI WA MIAKA MITANO 2011--2016


Utangulizi.

Mheshimiwa Spika, Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 99 (7) Toleo la 2007.

Mheshimiwa Spika, Nawashukuru pia viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani wakiongozwa na Kiongozi wetu wa kambi Mhe. Freeman Mbowe (MB), Naibu wake Mheshimiwa Zitto Kabwe (MB), Waheshimiwa viongozi wengine pamoja na wabunge wote wa kambi yetu, kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kuwakilisha na kutetea maslahi ya wananchi walionituma.

Mheshimiwa Spika, Kwa uzito huo huo, nakishukuru chama changu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wapiga kura wa Jimbo la Karatu kwa imani, heshima na wajibu mkubwa walionipa wa kunifanya kuwa mwakilishi wao. Naahidi nitaendelea kuwa pamoja nao wao pamoja na Watanzania wote kwa ujumla katika kusukuma mbele maendeleo ya taifa letu. Hakika, sitawaangusha.

Mheshimiwa Spika, Mwisho katika shukrani zangu, lakini kwa umuhimu mkubwa, nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote, kwa kazi mnayoifanya ya kuliongoza Bunge hili. Mungu azidi kuwatia busara na hekima katika kutekeleza wajibu wenu huo kwa haki na usawa.

Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kuwasilisha masikitiko ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na mpango huu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (3) (c)inasema kuwa majukumu ya Bunge ni “kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”; Wakati ibara ya katiba ikitamka hivyo, mpango huu tayari ulishasainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tangu tarehe 7 Juni 2011 na kuwasilishwa bungeni tarehe 8 Juni kama hati ya kuwasilisha mezani, bila kuelezwa ndani ya mpango wenyewe kama kilichowasilishwa ni rasimu.

Aidha, kwa mujibu wa mpango wenyewe, Rais ameshashukuru wadau kwa maoni yao yaliyowezesha kukamilisha mpango na ameshalishukuru bunge kwa mchango katika kukamilisha mpango husika.


Mheshimiwa Spika, Wakati Rais akisema hivyo, Kambi ya Upinzani haijawahi kushirikishwa wala kushiriki kikao chochote cha Bunge kilichojadili na kupitisha mpango huu. Kwa hiyo, Kambi ya Upinzani inamtaka waziri aeleze ni kikao kipi cha Bunge, na ni mkutano wa ngapi wa Bunge, uliowahi kujadili na na kupitisha mpango huu wa maendeleo na hata kumpelekea Mheshimiwa Rais kulishukuru Bunge kupitia dibaji yake iliyochapwa kwenye kitabu cha mpango huu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalitaka Bunge lifanye kazi zake kikamilifu na serikali iwe na utamaduni wa kuheshimu hilo. Tunaitaka serikali isiwe na utamaduni wa kuamini kuwa kila jambo litakalowasilishwa hapa Bungeni basi Bunge italipitisha tu. Tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa maoni ya wabunge yanazingatiwa na kuingizwa kwenye mpango huu kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana na lugha ambayo imetumika katika kuuandaa mpango huu.Huu ni mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa miaka mitano ijayo ila haulengi kufikishwa kwa Watanzania ambao wanapaswa kuutekeleza , kwani lugha iliyotumika haifahamiki kwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote.Tunapenda kuikumbusha serikali kuwa hakuna taifa lolote lililowahi kuendelea kwa kutumia lugha ya kukopa hapa ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali baada ya mpango huu kujadiliwa na kupitishwa na Bunge basi uandikwe kwa lugha ya Kiswahili na usambazwe kwa wananchi kupitia kwa wawakilishi wao kama wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji, madiwani na wabunge ili waweze kupanga mipango yao ya maendeleo kulingana na mpango huu. Kila mwenye kuidhinisha maamuzi anapaswa kuhakikisha kuwa maamuzi yake yanaendana na mpango wa taifa wa maendeleo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni kuwa pamoja na mpango huu kuwa na mikakati na malengo katika vipaumbele mahsusi, mpango huu hauna shabaha za ujumla za kutuwezesha kujipima kama taifa kuhusu mafanikio tunayotegemea kuyafikia baada ya kutekeleza mpango huu.

Kambi ya upinzani inapendekeza kuwa baadhi ya shabaha kuu za mpango huu ziwe kama ifuatavyo;


  1. Kupunguza umasikini vijijini kutoka asilimia 37% ya sasa na kufikia asilimia 20% .
  2. Kumaliza tatizo la umeme kabisa na kuzalisha umeme wa ziada kwa asilimia 20%.
  3. Kuwa Taifa linalozalisha gesi kwa wingi barani Afrika.
  4. Kuhakikisha kuwa asilimia 80% ya watanzania wanapata maji safi na salama.
  5. Kuhakikisha kuwa barabara za vijijini zinapitika kwa wakati wote wa mwaka.
  6. Kupunguza vifo vya akina mama na watoto.



KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO WA 2011/2012 -2015/2016

  1. Utawala bora na uwajibikaji

Mheshimiwa Spika, Upembuzi wa kina uliofanywa na Kambi ya Upinzani, umebaini kuwepo kwa mapungufu mengi na dosari kadhaa nzito zinazoweza kuathiri utekelezaji wake au kukwama kabisa.

Mheshimiwa Spika, Mipango ya aina hii si mipya katika nchi yetu. Tumeshakuwa na mipango ya maendeleo ya miaka mitano-mitano tangu mwanzoni mwa miaka ya 60, lakini hatimaye mingi ilisuasua au kukwama kabisa, kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni kutokuwepo kwa uwajibikaji wa kutosha ndani na baina ya taasisi za serikali.

[h=1]Mheshimiwa Spika, Mathalan, wakati wananchi wakishinikiza kuanza mapema kwa mchakato shirikishi wa kuandikwa kwa katiba mpya ili, pamoja na mambo mengine, wapate haki ya kuweka mifumo thabiti ya kusimamia uwajibikaji wa utawala kwa umma; Lakini kwa masikitiko makubwa kilio chao hicho hakionekani kuzingatiwa kwa uzito unaostahili.
[/h][h=1][/h][h=1]Kambi ya Upinzani, tumeshangazwa na mpango huu wa maendeleo wa miaka mitano (2011/2012 - 2015/2016) kutolipa kipaumbele hata kidogo hitaji la katiba mpya wala kutenga fedha maalum kwa ajili ya mchakato huo nyeti, katika kuamua hatma mpya ya mwelekeo wa taifa letu.
[/h]
Mheshimiwa Spika, Nguzo kuu ya utekelezaji wa mipango na malengo yote mazuri ni uwepo wa utawala bora na wenye kuwajibika kikamilifu. Kambi ya Upinzani inatambua kuwa mpango huu umetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuchochea demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora kwa kufanya mambo yafuatayo;

  1. Kuzijengea uwezo wa kiutendaji taasisi za kiserikali na watendaji wake.
  2. Kukabiliana na tatizo la rushwa,
  3. Kuchochea uwazi, uwajibikaji na maadili kwa watumishi wa umma.
  4. Kukamilisha mradi wote wa mfumo wa vitambulisho vya taifa na kuhakikisha vinatumika ifikapo mwaka 2015.
  5. Kuchochea ushiriki mpana wa wananchi na usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa mpango wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na shughuli zote hizo zilizoainishwa kwa ajili ya kuboresha uongozi bora na utawala wa sheria, kama moja ya mikakati ya utekelezaji wa mpango wenyewe, bado Kambi ya Upinzani inaona kuwa mchakato wa katiba mpya ulipaswa kupewa uzito mkubwa kwa upekee wake, kama nguzo kuu ya maboresho yote ya ndani ya mfumo wa utawala yanayokusudiwa kufanywa.

Mheshimiwa spika,
Hata kama serikali itasema kuwa kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya tume ya kurekebisha sheria kiasi cha shilingi 945 milioni, bado kambi ya upinzani inataka kuona fedha za mchakato wa katiba mpya zikitengwa. Kwa mujibu wa maelezo ya mpango huu fedha hizo za kurekebisha sheria zinatarajiwa kutoka nje ya nchi. Kambi ya upinzani inaona ni aibu kubwa kwa taifa kufikia hatua ya kuomba fedha za kurekebisha sheria kutoka nje ya nchi.

  1. Tatizo la umaskini na mwelekeo wa mpango.

Mheshimiwa Spika, Moja ya matatizo makubwa ya kiuchumi yanayoikabili nchi yetu katika zama hizi, ni kuwa na uchumi mpana (macro-economy) unaokua bila kupunguza umaskini wala kuwanufaisha wananchi walio wengi. Katika kipindi cha mwaka 2001 - 2010 uchumi wetu umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7. Kwa mfano, kipimo cha umaskini (Head Count Index) kinaonyesha kuwa umaskini ulipungua kidogo sana kutoka asilimia 35.7 mwaka 2001 hadi kufikia asilimia 33.6 mwaka 2007, ingawa uchumi umeelezwa kuwa ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 ndani ya kipindi hicho.

Mheshimiwa Spika, Ili kukabiliana na tatizo hilo la uchumi kukua huku umaskini ukiendelea, mpango huu umejieleza kuwa utajikita katika kutekeleza nadharia kuu mbili; Mosi ni kuvutia uwekezaji mkubwa, hususani kupitia maeneo au sekta zinazogusa zaidi maskini; Pili, kudumisha na kuendeleza ukuaji wa uchumi mpana kwa kuhakikisha pato la taifa linakua kwa wastani wa asilimia 8 kwa miaka mitano ijayo, na kwamba mpango utakaofuatia utaiwezesha nchi kulenga ukuaji wa pato la taifa kwa wastani wa takribani asilimia 10 kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na shabaha hizo, Kambi ya Upinzani inaona kuwa mpango huu umeshindwa kuweka bayana jinsi utakavyoinua uchumi wa vijijini (rural economic growth), ambao kimsingi ndio utakaoweza kupunguza moja kwa moja umaskini wa wananchi walio wengi. Mpango umejikita katika kushughulikia vipaumbele vilivyoainishwa kwa ujumla wake kwa kuanzia juu kwenda chini, bila kuzifanyia uwekezaji wa moja ya fursa nyingi za kiuchumi zilizopo katika ngazi za chini za utawala, kama wilayani na vijijini, ambako ndiko wengi wanaweza kukombolewa.

Mheshimiwa Spika, Mpango umetenga fedha za utekelezaji wa vipaumbele kadhaa vya kisekta kwa ujumla wake, lakini haujaweka mfumo mzuri wa mgawanyo wa raslimali za kimaendeleo kati ya halmashauri na serikali kuu, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ni changamoto katika utekelezaji wa mipango na mikakati mingi ya kimaendeleo, hivyo kusababisha mikakati hiyo kukwama inapofikia kwenye utekelezaji wake.

Kambi ya upinzani inaelewa kuwa pamoja na machapisho na maandiko mazuri ya mpango wenyewe kasoro kubwa ni kuwa yanatayarishiwa Dar Es Salaam maofisini na kuwanyima wananchi fursa katika kuumiliki mpango huu ili waweze kuutekeleza kikamilifu.


  1. Mpango unaanza kwa kushindwa
[h=1][/h][h=1]Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) kama lilivyo jina na malengo yake unapaswa kuanza kufanyiwa utekelezaji kwa kutengewa fedha za bajeti kuanzia mwaka wa fedha wa 2011/2012, ili ifikapo mwaka 2016 uwe umetimiza miaka mitano. Ukurasa wa 71 wa kitabu cha mpango huu (chapisho la Kiingereza) unaonyesha kupitia jedwali, kuwa zinahitajika jumla ya Shs trilioni 8.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012 tunaokwenda kuuanza siku si nyingi.
[/h]
Mheshimiwa Spika, Wakati utekelezaji wa mpango huu ukiwa umepangwa kuanza mwaka wa fedha wa 2011/2012, mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2011/2012 yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha wiki iliyopita, yanaonyesha kuwa hakuna fedha zilizotengwa za jumla ya Sh trilioni 8.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Jumla ya bajeti yote inayopendekezwa na serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ni Sh trilioni 13. 5. Katika hizo fedha za matumizi ya kawaida ni Sh trilioni 8.6 na matumizi ya maendeleo yametengewa Sh trilioni 4.9. Na hata kama fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo (Sh trilioni 4.9) zitashughulikia pia vipaumbele vya mpango wa maendeleo kama vilivyowekwa, bado utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka wa fedha 2011/2012 utakuwa umepungukiwa Sh trilioni 3.7, sawa na upungufu wa asilimia 43% ya fedha zote zinazohitajika kwa mpango huu kuanza kutekelezwa .

Mheshimiwa Spika, Kwa mahesabu hayo ya kibajeti, utekelezaji wa mpango huu utakwama kwa asilimia 43 katika mwaka wa kwanza wa kuanza kwake. Kauli kwamba, mwaka wa fedha wa 2011/2012 utakuwa ni kipindi cha mpito katika utekelezaji wa mpango huu, hazina mashiko.

Kambi ya Upinzani inaona kuwa kufanya hivyo ni kupoteza muda wa utekelezaji ambao tayari umo ndani ya mpango wenyewe – kwamba utatekelezwa kwa miaka mitano na sio miaka minne. Hii ni dalili kuwa mpango huu umeanza kufeli kabla hata ya kuanza utekelezaji wake.



  1. Ukadiriaji wa gharama

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imebaini kuwapo dosari kadhaa kuhusiana na gharama zilizokadiriwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu wa miaka mitano. Moja ya dosari hizo ni gharama za jumla za kutekeleza mpango huu ambazo ni Sh trilioni 42.98, kutowiana na uwezo halisi wa serikali kujipatia mapato yake. Ili mpango huu utekelezeke serikali itapaswa kuwa na bajeti ya maendeleo inayozidi au isiyopungua Sh trilioni 8.6 kila mwaka ndani ya kipindi chote cha miaka mitano cha utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Spika, Wakati serikali ikipaswa kuwa na Sh trilioni 8.6 za maendeleo kila mwaka ili kutekeleza mpango huu, uzoefu unaonyesha kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kuweza kukusanya fedha za kutosha ili bajeti ya maendeleo iwe kubwa. Kambi ya Upinzani inahoji ni miujiza gani ambayo serikali hii (yenye uwezo mdogo wa kukusanya mapato), itafanya hadi kuwa na bajeti ya maendeleo ya Sh trilioni 8.6, ikiwa imekuwa ikishindwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa spika, Ipo mipango mingi ambayo ilikwishapangwa lakini haikuonesha matokeo ambayo yalitarajiwa, kwa mfano ni utekelazaji wa MKUKUTA I ambapo ni programu ambayo hata ushirikishwaji wa wananchi ulikuwa ni mdogo sana na hivyo kutojenga msingi na matarajio yaliyokuwa yakitegemewa.

Kambi ya Upinzani inahoji ni kwa kiasi gani wananchi wameshirikishwa kwenye kutayarisha na kuandaa mpango huu? Au tumeendelea na utamaduni ule ule wa kutowashirikisha wananchi katika hatua za matayarisho na badala yake tunataka washiriki kwenye utekelezaji? Mipango mingi inakwama kwa sababu wananchi wanaachwa kwenye hatua za utayarishaji na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, Fedha zinazotarajiwa kutumika ni kiasi kikubwa sana kuliko vyanzo vya mapato vilivyoainishwa. Jumla ya fedha zinazotarajiwa kutumika ni trilioni 42.9 milioni za kitanzania, ambapo kati ya hizo, serikali inategemea kuchangia kiasi cha shilingi milioni 7.8 tu. Kwa uwezo wa sasa wa serikali wa kukusanya mapato yake na fedha zinazotengwa kwenye miradi ya maendeleo ni vigumu sana kufika lengo hilo kwa muda uliowekwa.

Kambi ya Upinzani inahoji, Je nakisi hii ya mapato itazibwa na vyanzo gani vya uhakika vya kuuwezesha mpango huu kutekelezek ili tusiendelee kuwa mabingwa wa kutengeneza mipango mizuri inayoishia kufungiwa kwenye makabati ya serikali.

Mheshimiwa Spika, Ukisoma Mpango huu utaona kuwa hakuna ufafanuzi wa Wadau wa Maendeleo ambao serikali imewaainisha kuwa watachangia katika kutekeleza mpango huu. Hili litaleta shida ikiwa wadau wengi watashindwa kutekeleza ahadi zao au kutekeleza wakiwa wamechelewa.

Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuweka bayana orodha ya wadau ambao wameonyesha nia ya kuuchangia mpango huu ili wajulikane na kiasi cha ahadi walizoahidi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona haja ya mpango huu kutekelezwa kuanzia ngazi ya Halmashauri huku jukumu la serikali kuu likibakia kuwa ni la kuratibu utekelezaji. Kwa kufanya hivyo, utekelezaji wa mpango huu utaweza kugusa wananchi moja kwa moja kuliko kuweka mamlaka ya utekelezaji kwenye ngazi ya serikali kuu pekee. Utekelezaji wa ushauri wetu huu utaufanya ile dhana nzima ya serikali ya ugatuaji wa madaraka itekelezeke.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali ya mwaka 2009/2010 inaeleza kuwa Deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 38% . Kambi ya Upinzani imestushwa na hali hii kwani kwa mujibu wa taarifa za serikali, hadi kufikia Disemba 2010 deni la taifa lilikuwa limefikia dola milioni 11,948.0 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi trilioni 17 za kitanzania .

Malipo ya deni la taifa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka ulioishia Machi 2011 yalikuwa shilingi bilioni 803.64. Malipo ya deni la nje kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi 73.66 bilioni na kati ya hizo shilingi 29.06 zilikuwa ni malipo ya mtaji na shilingi bilioni 44.6 zilikuwa ni malipo ya riba. Swali la kujiuliza hapa ni, Je ikiwa tunalipa riba kubwa kiasi hicho, yako wapi masharti nafuu ambayo serikali mara zote imekuwa ikiyasema?

Mheshimiwa Spika, Hali hii ya kulipa riba kubwa ipo pia kwenye ulipaji wa madeni ya ndani, kwani kwa kipindi hicho hicho kinachoishia mwezi machi 2011, deni la ndani lilipiwa kiasi cha shilingi 730.3 bilioni na kati ya hizo, shilingi bilioni 556.7 zilitumika kulipia dhamana za serikali zilizoiva na riba ilikuwa jumla ya shilingi 173.6 bilioni.

Kambi ya Upinzani inashauri kuwa huu ni wakati muafaka wa kuhakikisha kuwa inatungwa sheria itakayoliwezesha Bunge kuidhinisha Mikopo yote ambayo serikali inakopa kwenye taasisi za ndani na nje ya nchi.Hii itasaidia kupata taarifa juu ya lengo la mikopo hiyo na itadhibiti kuhakikisha kuwa tunakopa kwa ajili ya Maendeleo na sio vinginevyo.Na huu ndio utakuwa wajibu wa Bunge katika kuisimamia serikali kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa bei umezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka huku ukigusa bidhaa muhimu hasa chakula. Serikali bado inasuasua kuchukua hatua thabiti za kuzidbiti hali hiyo. Tusipochukua hatua za kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unadhibitiwa kikamilifu, utekelezaji wa mpango huu utakuwa ni ndoto.

Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza kwa kina kuna mkakati gani wa kudhibiti mfumuko wa bei hapa nchini, hasa ikitiliwa maanani kuwa mfumuko huu kwa kiasi kikubwa umesababishwa na kupanda bei kwa bidhaa za nishati hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Thamani ya shilingi yetu kwa mwaka 2010 ilishuka kwa asilimia 8.5 kulinganisha na dola ya Kimarekani. Ili kutekeleza mpango huu na kufikia lengo la kutumia shilingi trilioni 8.2 kwa mwaka wa kwanza, tutajikuta katika mwaka wa tatu wa utekelezaji wa mpango huu unafika kiasi cha fedha kinachotarajiwa kitakuwa sio Sh trilioni 9.1 tena kama kilivyopangwa sasa. Hii itavuruga kabisa utekelezaji wa mpango huu.

Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali ieleze kwa kina ina makakati gani ya kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya nchi ili kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kikamilifu ndani ya miaka 5 kwa makadirio ya fedha yaliyowekwa sasa. Vinginevyo, mpango huu utakuwa hautekelezeki, na tutajikuta tukilazimika kuufanyia duruso/mapitio (review) ili kuweza kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi. Vinginevyo, kiasi cha pesa kilichotengwa kwa utekelezaji wa mpango huu si kiasi halisi kinachoweza kutegemewa katika kuutekeleza mpango huu, ikiwa anguko hili la thamani ya shilingi litatokea.

Tunaitaka serikali iwe inakokotoa makadirio yake ya thamani ya mipango yake kwa kutumia shilingi za kitanzania na pia kwa kutumia dola ya kimarekani, ili iwe rahisi kuweza kupima thamani halisi ya mpango kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha yetu.

  1. Uboreshaji rasilimali watu.
Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa vipaumbele vya mpango wa maendeleo wa miaka mitano ni uboreshaji wa rasilimali watu. Kwenye hili mkazo umewekwa kwenye kuboresha shule zilizopo, kujenga nyumba za waalimu nakadhalika.

Kambi ya upinzani inataka mpango uweke wazi kuwa kipaumbele cha kwanza ni elimu bora ili kuhakikisha kuwa rasilimali watu inaandaliwa kukidhi haja ya kuwa na taifa lenye watu walioelimika. Na hili litaendana sambamba na kuifumua mitaala yetu ya elimu ili ikidhi haja ya wakati uliopo na ujao katika nchi yetu.

Tunaitaka serikali ihakikishe kuwa kama taifa tunakuwa na mkakati maalum wa kuandaa wataalamu kwenye sekta nyeti katika kukuza uchumi na hasa turejee kwenye utamaduni wetu wa kupeleka vijana wetu nje ya nchi na kuwapatia utalaam kuhusu madini, gesi, mafuta, lugha hasa Kichina, Kihindi, Kihispaniola. Lengo ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na wataalamu wa kutosha na ambao watashiriki moja kwa moja katika kuvuna rasilimali za taifa letu kwa manufaa ya taifa.

Kambi ya Upinzani, inataka mpango huu uainishe ndani ya miaka mitano tunataka kuwa na wataalamu wangapi na kwenye sekta gani. Na hili lifanywe na Balozi zetu kufanya tafiti kwenye nchi ambazo wametumwa kujua ni vyuo gani vinavyotoa taaluma adhimu. Kwa hiyo tunaitaka serikali iwe inawatuma vijana wetu kusoma nje na hatimaye kuweza kulikomboa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, mpango huu ni wa miaka mitano, ila haujazingatia popote kuhusiana na changamoto ya kuhakikisha kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaandaliwa kikamilifu katika kukabiliana na changamoto mpya na za kisasa.

Kambi ya Upinzani, inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inazingatia katika kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo na zijazo ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huu.


Mheshimiwa Spika,

Naomba kuwasilisha .



………………………

Mchungaji Israel Y. Natse.

Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani.
13-06-2011.