TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa za Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kumpa Rais
Jakaya Mrisho Kikwete saa 48 kuwataja kwa majina viongozi wa dini
wanaotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya, ni kauli ya
kusikitisha na ambayo haikutegemewa kutoka kwa viongozi hao wa dini.
Viongozi wa dini ni watu wa kutumainiwa sana katika jamii yeyote,
lakini ikizingatiwa kuwa wao sio malaika ama watakatifu hapa duniani,
kwani nao wanatumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au
hali isiyo tegemewa kabisa.
Katika Hotuba yake kwenye sikukuu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa
Mhashamu Askofu John Ndimbo kuwa Askofu wa Jimbo la Mbinga, Rais
Kikwete alitoa ombi ambalo si geni kwani alishalitoa katika hafla
zingine pia zilizohusisha viongozi wa dini.
Katika sherehe hiyo Rais alitoa ombi la kuwataka viongozi wa dini
wajihusishe kwa ukamilifu katika mapambano dhidi ya biashara na
matumizi ya dawa za kulevya.
Rais Alisema, “Ni tatizo linalozidi kukua pamoja na jitihada za
Serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji
na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Athari zake kwa jamii
zinaeleweka hivyo haihitaji kuzirudia” Rais alieleza, “Hata hivyo
niruhusuni niseme tu kwamba tusipofanikiwa kulidhibiti tatizo hili,
hasara yake ni kubwa mno. Watoto wetu wengi wataharibika, uhalifu,
hasa wa wizi na mauaji utaongezeka. Taifa litaharibikiwa.” Amesema
Rais na kuendelea kueleza kuwa,
“Siku hizi kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za
kulevya. Inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, Lakini
inasikitisha sana kuona kuwa biashara hiyo sasa inawavutia hata
watumishi wa Mungu. Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana.
Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini
mnasikilizwa, Nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya
madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndiyo walengwa
wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa
za kulevya”. Rais alisema.
Kwa maneno haya, tunategemea viongozi wa dini kuchukua onyo hili la
Rais kama ishara (Clue) na kuanza kuifanyia kazi.
Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa
kuuliza kama kweli, ni wa rangi gani? Unatakiwa kushtuka na kuweka na
kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumuondosha nyumbani kwako hata ikibidi
umuue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako.
Rais ana nia njema sana katika kulielezea jambo hili na mwenye nia
njema haumbuki.
Hivi karibuni wapo viongozi wa dini wamekamatwa kwa rushwa, ngono na
kutuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kinyume na
maadili yasiyo tegemewa na jamii kwa ujumla, wapo ambao wameshakamatwa
na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, wapo wanaochunguzwa,
tumeshawashuhudia na bado wataendelea kushuhudiwa. Hili si jambo dogo
la kujitetea kwa kauli nyepesi kutoka kwa watu wanaotegemewa na jamii
kwa kumpa Rais saa 48.
Anaejishuku ajisalimishe mwenyewe, anaeshukiwa na jamii afichuliwe ili
afanyiwe uchunguzi na hatimaye sheria ichukue mkondo wake lakini
msisubiri Rais awataje hadharani ndiyo muanze kuchukua hatua.
Mnategemewa muweke mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto
hiyo, na sio kuaihirisha tatizo hili ambalo linazidi kuwa kubwa. Kazi
hii ya kupambana na madawa ya kulevya haimhusu Rais peke yake inamhusu
kila Mtanzania, popote alipo katika nafasi yake na viongozi wa dini
wananafasi kubwa sana kwa sababu wao wanasikilizwa, wanatoa ushauri na
wanategemewa kuwa na maelekezo yanayompendeza Mungu.
Mwisho.
Imetolewa na:
Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Ikulu,
Dar-Es-Salaam.
07 Juni, 2011
No comments:
Post a Comment