Utangulizi.
Mheshimiwa Spika, Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 99 (7) Toleo la 2007.
Mheshimiwa Spika, Nawashukuru pia viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani wakiongozwa na Kiongozi wetu wa kambi Mhe. Freeman Mbowe (MB), Naibu wake Mheshimiwa Zitto Kabwe (MB), Waheshimiwa viongozi wengine pamoja na wabunge wote wa kambi yetu, kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kuwakilisha na kutetea maslahi ya wananchi walionituma.
Mheshimiwa Spika, Kwa uzito huo huo, nakishukuru chama changu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wapiga kura wa Jimbo la Karatu kwa imani, heshima na wajibu mkubwa walionipa wa kunifanya kuwa mwakilishi wao. Naahidi nitaendelea kuwa pamoja nao wao pamoja na Watanzania wote kwa ujumla katika kusukuma mbele maendeleo ya taifa letu. Hakika, sitawaangusha.
Mheshimiwa Spika, Mwisho katika shukrani zangu, lakini kwa umuhimu mkubwa, nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote, kwa kazi mnayoifanya ya kuliongoza Bunge hili. Mungu azidi kuwatia busara na hekima katika kutekeleza wajibu wenu huo kwa haki na usawa.
Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kuwasilisha masikitiko ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na mpango huu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (3) (c)inasema kuwa majukumu ya Bunge ni “kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”; Wakati ibara ya katiba ikitamka hivyo, mpango huu tayari ulishasainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tangu tarehe 7 Juni 2011 na kuwasilishwa bungeni tarehe 8 Juni kama hati ya kuwasilisha mezani, bila kuelezwa ndani ya mpango wenyewe kama kilichowasilishwa ni rasimu.
Aidha, kwa mujibu wa mpango wenyewe, Rais ameshashukuru wadau kwa maoni yao yaliyowezesha kukamilisha mpango na ameshalishukuru bunge kwa mchango katika kukamilisha mpango husika.
Mheshimiwa Spika, Wakati Rais akisema hivyo, Kambi ya Upinzani haijawahi kushirikishwa wala kushiriki kikao chochote cha Bunge kilichojadili na kupitisha mpango huu. Kwa hiyo, Kambi ya Upinzani inamtaka waziri aeleze ni kikao kipi cha Bunge, na ni mkutano wa ngapi wa Bunge, uliowahi kujadili na na kupitisha mpango huu wa maendeleo na hata kumpelekea Mheshimiwa Rais kulishukuru Bunge kupitia dibaji yake iliyochapwa kwenye kitabu cha mpango huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalitaka Bunge lifanye kazi zake kikamilifu na serikali iwe na utamaduni wa kuheshimu hilo. Tunaitaka serikali isiwe na utamaduni wa kuamini kuwa kila jambo litakalowasilishwa hapa Bungeni basi Bunge italipitisha tu. Tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa maoni ya wabunge yanazingatiwa na kuingizwa kwenye mpango huu kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana na lugha ambayo imetumika katika kuuandaa mpango huu.Huu ni mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa miaka mitano ijayo ila haulengi kufikishwa kwa Watanzania ambao wanapaswa kuutekeleza , kwani lugha iliyotumika haifahamiki kwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wote.Tunapenda kuikumbusha serikali kuwa hakuna taifa lolote lililowahi kuendelea kwa kutumia lugha ya kukopa hapa ulimwenguni.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali baada ya mpango huu kujadiliwa na kupitishwa na Bunge basi uandikwe kwa lugha ya Kiswahili na usambazwe kwa wananchi kupitia kwa wawakilishi wao kama wenyeviti wa vijiji, mitaa, vitongoji, madiwani na wabunge ili waweze kupanga mipango yao ya maendeleo kulingana na mpango huu. Kila mwenye kuidhinisha maamuzi anapaswa kuhakikisha kuwa maamuzi yake yanaendana na mpango wa taifa wa maendeleo.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni kuwa pamoja na mpango huu kuwa na mikakati na malengo katika vipaumbele mahsusi, mpango huu hauna shabaha za ujumla za kutuwezesha kujipima kama taifa kuhusu mafanikio tunayotegemea kuyafikia baada ya kutekeleza mpango huu.
Kambi ya upinzani inapendekeza kuwa baadhi ya shabaha kuu za mpango huu ziwe kama ifuatavyo;
- Kupunguza umasikini vijijini kutoka asilimia 37% ya sasa na kufikia asilimia 20% .
- Kumaliza tatizo la umeme kabisa na kuzalisha umeme wa ziada kwa asilimia 20%.
- Kuwa Taifa linalozalisha gesi kwa wingi barani Afrika.
- Kuhakikisha kuwa asilimia 80% ya watanzania wanapata maji safi na salama.
- Kuhakikisha kuwa barabara za vijijini zinapitika kwa wakati wote wa mwaka.
- Kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
KUHUSU MPANGO WA MAENDELEO WA 2011/2012 -2015/2016
- Utawala bora na uwajibikaji
Mheshimiwa Spika, Upembuzi wa kina uliofanywa na Kambi ya Upinzani, umebaini kuwepo kwa mapungufu mengi na dosari kadhaa nzito zinazoweza kuathiri utekelezaji wake au kukwama kabisa.
Mheshimiwa Spika, Mipango ya aina hii si mipya katika nchi yetu. Tumeshakuwa na mipango ya maendeleo ya miaka mitano-mitano tangu mwanzoni mwa miaka ya 60, lakini hatimaye mingi ilisuasua au kukwama kabisa, kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni kutokuwepo kwa uwajibikaji wa kutosha ndani na baina ya taasisi za serikali.
[h=1]Mheshimiwa Spika, Mathalan, wakati wananchi wakishinikiza kuanza mapema kwa mchakato shirikishi wa kuandikwa kwa katiba mpya ili, pamoja na mambo mengine, wapate haki ya kuweka mifumo thabiti ya kusimamia uwajibikaji wa utawala kwa umma; Lakini kwa masikitiko makubwa kilio chao hicho hakionekani kuzingatiwa kwa uzito unaostahili.
[/h][h=1][/h][h=1]Kambi ya Upinzani, tumeshangazwa na mpango huu wa maendeleo wa miaka mitano (2011/2012 - 2015/2016) kutolipa kipaumbele hata kidogo hitaji la katiba mpya wala kutenga fedha maalum kwa ajili ya mchakato huo nyeti, katika kuamua hatma mpya ya mwelekeo wa taifa letu.
[/h]
Mheshimiwa Spika, Nguzo kuu ya utekelezaji wa mipango na malengo yote mazuri ni uwepo wa utawala bora na wenye kuwajibika kikamilifu. Kambi ya Upinzani inatambua kuwa mpango huu umetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuchochea demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora kwa kufanya mambo yafuatayo;
- Kuzijengea uwezo wa kiutendaji taasisi za kiserikali na watendaji wake.
- Kukabiliana na tatizo la rushwa,
- Kuchochea uwazi, uwajibikaji na maadili kwa watumishi wa umma.
- Kukamilisha mradi wote wa mfumo wa vitambulisho vya taifa na kuhakikisha vinatumika ifikapo mwaka 2015.
- Kuchochea ushiriki mpana wa wananchi na usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa mpango wenyewe.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na shughuli zote hizo zilizoainishwa kwa ajili ya kuboresha uongozi bora na utawala wa sheria, kama moja ya mikakati ya utekelezaji wa mpango wenyewe, bado Kambi ya Upinzani inaona kuwa mchakato wa katiba mpya ulipaswa kupewa uzito mkubwa kwa upekee wake, kama nguzo kuu ya maboresho yote ya ndani ya mfumo wa utawala yanayokusudiwa kufanywa.
Mheshimiwa spika,
Hata kama serikali itasema kuwa kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya tume ya kurekebisha sheria kiasi cha shilingi 945 milioni, bado kambi ya upinzani inataka kuona fedha za mchakato wa katiba mpya zikitengwa. Kwa mujibu wa maelezo ya mpango huu fedha hizo za kurekebisha sheria zinatarajiwa kutoka nje ya nchi. Kambi ya upinzani inaona ni aibu kubwa kwa taifa kufikia hatua ya kuomba fedha za kurekebisha sheria kutoka nje ya nchi.
- Tatizo la umaskini na mwelekeo wa mpango.
Mheshimiwa Spika, Moja ya matatizo makubwa ya kiuchumi yanayoikabili nchi yetu katika zama hizi, ni kuwa na uchumi mpana (macro-economy) unaokua bila kupunguza umaskini wala kuwanufaisha wananchi walio wengi. Katika kipindi cha mwaka 2001 - 2010 uchumi wetu umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7. Kwa mfano, kipimo cha umaskini (Head Count Index) kinaonyesha kuwa umaskini ulipungua kidogo sana kutoka asilimia 35.7 mwaka 2001 hadi kufikia asilimia 33.6 mwaka 2007, ingawa uchumi umeelezwa kuwa ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 ndani ya kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika, Ili kukabiliana na tatizo hilo la uchumi kukua huku umaskini ukiendelea, mpango huu umejieleza kuwa utajikita katika kutekeleza nadharia kuu mbili; Mosi ni kuvutia uwekezaji mkubwa, hususani kupitia maeneo au sekta zinazogusa zaidi maskini; Pili, kudumisha na kuendeleza ukuaji wa uchumi mpana kwa kuhakikisha pato la taifa linakua kwa wastani wa asilimia 8 kwa miaka mitano ijayo, na kwamba mpango utakaofuatia utaiwezesha nchi kulenga ukuaji wa pato la taifa kwa wastani wa takribani asilimia 10 kuanzia mwaka 2016 hadi 2025.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na shabaha hizo, Kambi ya Upinzani inaona kuwa mpango huu umeshindwa kuweka bayana jinsi utakavyoinua uchumi wa vijijini (rural economic growth), ambao kimsingi ndio utakaoweza kupunguza moja kwa moja umaskini wa wananchi walio wengi. Mpango umejikita katika kushughulikia vipaumbele vilivyoainishwa kwa ujumla wake kwa kuanzia juu kwenda chini, bila kuzifanyia uwekezaji wa moja ya fursa nyingi za kiuchumi zilizopo katika ngazi za chini za utawala, kama wilayani na vijijini, ambako ndiko wengi wanaweza kukombolewa.
Mheshimiwa Spika, Mpango umetenga fedha za utekelezaji wa vipaumbele kadhaa vya kisekta kwa ujumla wake, lakini haujaweka mfumo mzuri wa mgawanyo wa raslimali za kimaendeleo kati ya halmashauri na serikali kuu, jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ni changamoto katika utekelezaji wa mipango na mikakati mingi ya kimaendeleo, hivyo kusababisha mikakati hiyo kukwama inapofikia kwenye utekelezaji wake.
Kambi ya upinzani inaelewa kuwa pamoja na machapisho na maandiko mazuri ya mpango wenyewe kasoro kubwa ni kuwa yanatayarishiwa Dar Es Salaam maofisini na kuwanyima wananchi fursa katika kuumiliki mpango huu ili waweze kuutekeleza kikamilifu.
- Mpango unaanza kwa kushindwa
[/h]
Mheshimiwa Spika, Wakati utekelezaji wa mpango huu ukiwa umepangwa kuanza mwaka wa fedha wa 2011/2012, mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2011/2012 yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha wiki iliyopita, yanaonyesha kuwa hakuna fedha zilizotengwa za jumla ya Sh trilioni 8.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Jumla ya bajeti yote inayopendekezwa na serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ni Sh trilioni 13. 5. Katika hizo fedha za matumizi ya kawaida ni Sh trilioni 8.6 na matumizi ya maendeleo yametengewa Sh trilioni 4.9. Na hata kama fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo (Sh trilioni 4.9) zitashughulikia pia vipaumbele vya mpango wa maendeleo kama vilivyowekwa, bado utekelezaji wa mpango huu kwa mwaka wa fedha 2011/2012 utakuwa umepungukiwa Sh trilioni 3.7, sawa na upungufu wa asilimia 43% ya fedha zote zinazohitajika kwa mpango huu kuanza kutekelezwa .
Mheshimiwa Spika, Kwa mahesabu hayo ya kibajeti, utekelezaji wa mpango huu utakwama kwa asilimia 43 katika mwaka wa kwanza wa kuanza kwake. Kauli kwamba, mwaka wa fedha wa 2011/2012 utakuwa ni kipindi cha mpito katika utekelezaji wa mpango huu, hazina mashiko.
Kambi ya Upinzani inaona kuwa kufanya hivyo ni kupoteza muda wa utekelezaji ambao tayari umo ndani ya mpango wenyewe – kwamba utatekelezwa kwa miaka mitano na sio miaka minne. Hii ni dalili kuwa mpango huu umeanza kufeli kabla hata ya kuanza utekelezaji wake.
- Ukadiriaji wa gharama
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imebaini kuwapo dosari kadhaa kuhusiana na gharama zilizokadiriwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu wa miaka mitano. Moja ya dosari hizo ni gharama za jumla za kutekeleza mpango huu ambazo ni Sh trilioni 42.98, kutowiana na uwezo halisi wa serikali kujipatia mapato yake. Ili mpango huu utekelezeke serikali itapaswa kuwa na bajeti ya maendeleo inayozidi au isiyopungua Sh trilioni 8.6 kila mwaka ndani ya kipindi chote cha miaka mitano cha utekelezaji wa mpango huu.
Mheshimiwa Spika, Wakati serikali ikipaswa kuwa na Sh trilioni 8.6 za maendeleo kila mwaka ili kutekeleza mpango huu, uzoefu unaonyesha kuwa imekuwa vigumu kwa serikali kuweza kukusanya fedha za kutosha ili bajeti ya maendeleo iwe kubwa. Kambi ya Upinzani inahoji ni miujiza gani ambayo serikali hii (yenye uwezo mdogo wa kukusanya mapato), itafanya hadi kuwa na bajeti ya maendeleo ya Sh trilioni 8.6, ikiwa imekuwa ikishindwa kufanya hivyo.
Mheshimiwa spika, Ipo mipango mingi ambayo ilikwishapangwa lakini haikuonesha matokeo ambayo yalitarajiwa, kwa mfano ni utekelazaji wa MKUKUTA I ambapo ni programu ambayo hata ushirikishwaji wa wananchi ulikuwa ni mdogo sana na hivyo kutojenga msingi na matarajio yaliyokuwa yakitegemewa.
Kambi ya Upinzani inahoji ni kwa kiasi gani wananchi wameshirikishwa kwenye kutayarisha na kuandaa mpango huu? Au tumeendelea na utamaduni ule ule wa kutowashirikisha wananchi katika hatua za matayarisho na badala yake tunataka washiriki kwenye utekelezaji? Mipango mingi inakwama kwa sababu wananchi wanaachwa kwenye hatua za utayarishaji na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, Fedha zinazotarajiwa kutumika ni kiasi kikubwa sana kuliko vyanzo vya mapato vilivyoainishwa. Jumla ya fedha zinazotarajiwa kutumika ni trilioni 42.9 milioni za kitanzania, ambapo kati ya hizo, serikali inategemea kuchangia kiasi cha shilingi milioni 7.8 tu. Kwa uwezo wa sasa wa serikali wa kukusanya mapato yake na fedha zinazotengwa kwenye miradi ya maendeleo ni vigumu sana kufika lengo hilo kwa muda uliowekwa.
Kambi ya Upinzani inahoji, Je nakisi hii ya mapato itazibwa na vyanzo gani vya uhakika vya kuuwezesha mpango huu kutekelezek ili tusiendelee kuwa mabingwa wa kutengeneza mipango mizuri inayoishia kufungiwa kwenye makabati ya serikali.
Mheshimiwa Spika, Ukisoma Mpango huu utaona kuwa hakuna ufafanuzi wa Wadau wa Maendeleo ambao serikali imewaainisha kuwa watachangia katika kutekeleza mpango huu. Hili litaleta shida ikiwa wadau wengi watashindwa kutekeleza ahadi zao au kutekeleza wakiwa wamechelewa.
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuweka bayana orodha ya wadau ambao wameonyesha nia ya kuuchangia mpango huu ili wajulikane na kiasi cha ahadi walizoahidi.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona haja ya mpango huu kutekelezwa kuanzia ngazi ya Halmashauri huku jukumu la serikali kuu likibakia kuwa ni la kuratibu utekelezaji. Kwa kufanya hivyo, utekelezaji wa mpango huu utaweza kugusa wananchi moja kwa moja kuliko kuweka mamlaka ya utekelezaji kwenye ngazi ya serikali kuu pekee. Utekelezaji wa ushauri wetu huu utaufanya ile dhana nzima ya serikali ya ugatuaji wa madaraka itekelezeke.
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali ya mwaka 2009/2010 inaeleza kuwa Deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 38% . Kambi ya Upinzani imestushwa na hali hii kwani kwa mujibu wa taarifa za serikali, hadi kufikia Disemba 2010 deni la taifa lilikuwa limefikia dola milioni 11,948.0 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi trilioni 17 za kitanzania .
Malipo ya deni la taifa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka ulioishia Machi 2011 yalikuwa shilingi bilioni 803.64. Malipo ya deni la nje kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi 73.66 bilioni na kati ya hizo shilingi 29.06 zilikuwa ni malipo ya mtaji na shilingi bilioni 44.6 zilikuwa ni malipo ya riba. Swali la kujiuliza hapa ni, Je ikiwa tunalipa riba kubwa kiasi hicho, yako wapi masharti nafuu ambayo serikali mara zote imekuwa ikiyasema?
Mheshimiwa Spika, Hali hii ya kulipa riba kubwa ipo pia kwenye ulipaji wa madeni ya ndani, kwani kwa kipindi hicho hicho kinachoishia mwezi machi 2011, deni la ndani lilipiwa kiasi cha shilingi 730.3 bilioni na kati ya hizo, shilingi bilioni 556.7 zilitumika kulipia dhamana za serikali zilizoiva na riba ilikuwa jumla ya shilingi 173.6 bilioni.
Kambi ya Upinzani inashauri kuwa huu ni wakati muafaka wa kuhakikisha kuwa inatungwa sheria itakayoliwezesha Bunge kuidhinisha Mikopo yote ambayo serikali inakopa kwenye taasisi za ndani na nje ya nchi.Hii itasaidia kupata taarifa juu ya lengo la mikopo hiyo na itadhibiti kuhakikisha kuwa tunakopa kwa ajili ya Maendeleo na sio vinginevyo.Na huu ndio utakuwa wajibu wa Bunge katika kuisimamia serikali kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa bei umezidi kuongezeka mwaka hadi mwaka huku ukigusa bidhaa muhimu hasa chakula. Serikali bado inasuasua kuchukua hatua thabiti za kuzidbiti hali hiyo. Tusipochukua hatua za kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unadhibitiwa kikamilifu, utekelezaji wa mpango huu utakuwa ni ndoto.
Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza kwa kina kuna mkakati gani wa kudhibiti mfumuko wa bei hapa nchini, hasa ikitiliwa maanani kuwa mfumuko huu kwa kiasi kikubwa umesababishwa na kupanda bei kwa bidhaa za nishati hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Thamani ya shilingi yetu kwa mwaka 2010 ilishuka kwa asilimia 8.5 kulinganisha na dola ya Kimarekani. Ili kutekeleza mpango huu na kufikia lengo la kutumia shilingi trilioni 8.2 kwa mwaka wa kwanza, tutajikuta katika mwaka wa tatu wa utekelezaji wa mpango huu unafika kiasi cha fedha kinachotarajiwa kitakuwa sio Sh trilioni 9.1 tena kama kilivyopangwa sasa. Hii itavuruga kabisa utekelezaji wa mpango huu.
Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali ieleze kwa kina ina makakati gani ya kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya nchi ili kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kikamilifu ndani ya miaka 5 kwa makadirio ya fedha yaliyowekwa sasa. Vinginevyo, mpango huu utakuwa hautekelezeki, na tutajikuta tukilazimika kuufanyia duruso/mapitio (review) ili kuweza kukabiliana na kushuka kwa thamani ya shilingi. Vinginevyo, kiasi cha pesa kilichotengwa kwa utekelezaji wa mpango huu si kiasi halisi kinachoweza kutegemewa katika kuutekeleza mpango huu, ikiwa anguko hili la thamani ya shilingi litatokea.
Tunaitaka serikali iwe inakokotoa makadirio yake ya thamani ya mipango yake kwa kutumia shilingi za kitanzania na pia kwa kutumia dola ya kimarekani, ili iwe rahisi kuweza kupima thamani halisi ya mpango kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha yetu.
- Uboreshaji rasilimali watu.
Kambi ya upinzani inataka mpango uweke wazi kuwa kipaumbele cha kwanza ni elimu bora ili kuhakikisha kuwa rasilimali watu inaandaliwa kukidhi haja ya kuwa na taifa lenye watu walioelimika. Na hili litaendana sambamba na kuifumua mitaala yetu ya elimu ili ikidhi haja ya wakati uliopo na ujao katika nchi yetu.
Tunaitaka serikali ihakikishe kuwa kama taifa tunakuwa na mkakati maalum wa kuandaa wataalamu kwenye sekta nyeti katika kukuza uchumi na hasa turejee kwenye utamaduni wetu wa kupeleka vijana wetu nje ya nchi na kuwapatia utalaam kuhusu madini, gesi, mafuta, lugha hasa Kichina, Kihindi, Kihispaniola. Lengo ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na wataalamu wa kutosha na ambao watashiriki moja kwa moja katika kuvuna rasilimali za taifa letu kwa manufaa ya taifa.
Kambi ya Upinzani, inataka mpango huu uainishe ndani ya miaka mitano tunataka kuwa na wataalamu wangapi na kwenye sekta gani. Na hili lifanywe na Balozi zetu kufanya tafiti kwenye nchi ambazo wametumwa kujua ni vyuo gani vinavyotoa taaluma adhimu. Kwa hiyo tunaitaka serikali iwe inawatuma vijana wetu kusoma nje na hatimaye kuweza kulikomboa taifa letu.
Mheshimiwa Spika, mpango huu ni wa miaka mitano, ila haujazingatia popote kuhusiana na changamoto ya kuhakikisha kuwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaandaliwa kikamilifu katika kukabiliana na changamoto mpya na za kisasa.
Kambi ya Upinzani, inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inazingatia katika kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo na zijazo ndani ya miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huu.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha .
………………………
Mchungaji Israel Y. Natse.
Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani.
13-06-2011.
No comments:
Post a Comment