Dawa za Sh8 bilioni zaoza mikononi mwa MSD |
Saturday, 04 June 2011 09:44 |
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), jana ilikakataa kupitisha hesabu za Bohari Kuu ya Dawa ya Serikali (MSD)kutokana na kuharibika kwa dawa zenye thamani ya Sh8 bilioni. Sambamba na hatua hiyo, Makamu Mwenyekiti wa POAC, Deo Filikunjombe aliwatoa nje viongozi wa MSD waliofika mbele ya kamati hiyo kutetea hesabu zao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Tecla Shangali na Mkurugenzi Mkuu, Joseph Mgaya. Filikunjombe alisema kamati imesikitishwa na hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo zimeonyesha kuwapo kwa upungufu mkubwa. “Wakati Watanzania wengi wanakufa kwa kukosa dawa, ripoti hii inaonyesha kwamba dawa za mabilioni ya fedha ziliharibika zikiwa mikononi mwa MSD,” alisema Filikunjombe na kuongeza: “Huu ni uharibifu mkubwa wa fedha za walipakodi, hali hii hatuwezi kuiacha iendelee, lazima tuchukue hatua. Makamu mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe (CCM), alisema kiasi cha Sh5.2 bilioni hakijulikani kimetumika vipi hali ambayo inazidi kuzua maswali. Filikunjombe aliagiza CAG kufanya ukaguzi maalum wa MSD ili hatimaye kamati hiyo iweze kupitia hesabu hizo. “Hesabu zenu hatuwezi kuzipitisha, tunaomba muondoke hadi CAG atakapofanya ukaguzi maalumu ndipo tunaweza kuwaita mbele ya kamati,” alisema Filikunjombe. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa nje, Mgaya alikiri kuharibika kwa dawa hizo akisema hiyo inatokana na MSD kununua dawa zinazotosheleza mahitaji ya nchi wakati huohuo, serikali nayo kupata misaada ya dawa kutoka kwa wahisani mbalimbali. “Ikumbukwe kwamba tunaweza kuagiza dawa zinazotosheleza mahitaji lakini serikali inaweza kupewa pia msaada wa dawa zilezile, matokeo yake dawa zinakuwa nyingi kuliko mahitaji,” alisema Mgaya. Aidha, Mgaya alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), linaruhusu kiwango fulani cha dawa kuharibika zikiwaa katika taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na utunzaji wa dawa. “Viwango vya WHO vinaruhusu asilimia tatu za dawa kwamba zinaweza kuharibika na hilo ni jambo la kawaida na dawa zilizoharibika ni chini ya asilimia tatu jambo ambalo ni la kawaida,” alisema CHANZO CHA HABARI GAZETI LA MWANANCHI |
No comments:
Post a Comment