Sunday, September 15, 2013

SIMBA YAUA,YANGA YASHIKWA

Simba imekata mzizi wa fitina kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, huku mabingwa watetezi Yanga, Azam wakilazimisha sare ugenini dhidi Mbeya City na Kagera Sugar.
Kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki waliingia wakitokea benchi na kuifungia Simba mabao hayo mawili muhimu katika kipindi cha pili. Mabingwa watetezi Yanga, waliokolewa na bao la Didier Kavumbagu wakilazimisha sare 1-1 na Mbeya City waliopanda daraja msimu huu.
JKT Ruvu imeendelea kung’ang’ania kileleni baada ya kuichapa Ashanti United kwa bao 1-0 na kuweka rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo.
MBEYA
Mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu na vituko vingi kabla ya kuanza kwake baada ya basi lililobeba wachezaji wa Yanga kushambuliwa kwa mawe, chupa za maji, bia na mashabiki wa Mbeya City wakati likiingia uwanjani na kusababisha kuvunja kioo cha dirisha la dereva.
Dakika chache kabla ya mechi kuanza meneja wa Uwanja wa Sokoine, Modest Mwaluka aliokota mayai matatu katikati ya uwanja.
Mwigane Yahya ndiye aliamsha shangwe za mashabiki wa Mbeya baada ya kuifungia Mbeya City bao la kuongoza katika dakika 49 akiunganisha krosi ya Mazanda.
Baada ya bao hilo Yanga, iliwapumzisha Nizar na Bahanuzi na kuwaingiza Oscar na Jerry Tegete mabadiliko yaliyozaa matunda kwani dakika ya 71 walisawazisha bao hilo kupitia Kavumbagu akimalizia krosi ya Tegete.
Dar es Salaam
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden aliwapumzisha Said Khamis, Twaha Ibrahimu na kuwaingiza Henry Joseph na Betram Mwombeki ili kuimarisha safu ya kiungo iliyoonekana kuzidiwa nguvu na vijana wa Mtibwa.
Mabadiliko hayo yalizaa faida katika dakika ya 67, pale Joseph Shindika alipoipatia Simba bao la kuongoza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Amri Kiemba.
Dakika ya 90, Mwombeki aliwainua mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la pili akimalizia vizuri pasi ya Ramadhani Singano ambaye kabla aligongeana vyema na Joseph.


Safari ya Ashanti United kurudi ilipotoka imezidi kushika kasi baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu, goli pekee la Amos Mgisa.
Azam wameendelea na mwendo wa kusuasua baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Mshambuliaji Temi Felix aliwainua mashabiki wa Kagera Sugar,ambapo kiungo Hamisi Mcha aliisawazishia Azam. Katika michezo mingine Tanga, Coastal Union ilitoka sare 0-0 na Prisonsi.
Arusha wenyeji Oljoro JKT walilazimishwa sare 1 -1 na Rhino Rangers, wageni Rhino walipata bao la kuongoza kupitia Saad Kipanga kabla ya Amiry Omary kuisawazishia Oljoro katika dakika 27.
Vilevile Ruvu Shooting ilichapa Mgambo JKT kwa bao 1-0 shukrani k wa bao Elias Maguli.
Imeandaliwa na Vicky Kimaro, Jessica Nangawe (Dar), Msafiri Sanjito (Kibaha), William Paul (Kagera), Mosses Mashalla (Arusha), Doris Maliyaga (Mbeya) Salim
Mohamed (Tanga).

CHANZO  GAZETI LA MWANANCHI

Tuesday, September 10, 2013

HATIMAYE ALEX MASSAWE APANDA KIZIMBANI

Mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Massawe amefikishwa mahakamani Dubai, Falme za Kiarabu (UAE), kwa tuhuma za mauaji baada ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali ya nchi hiyo kumkamata.
Massawe anayetarajiwa kuletwa nchini wakati wowote kuanzia sasa, alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu na alikamatwa Dubai, mapema Julai na maofisa wa usalama wa UAE baada ya alama zake za vidole kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Baada ya kukamatwa, Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema Massawe alikamatwa kati ya Juni 20 na 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Massawe ambaye anafanya biashara zake katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba akiwa Dubai, alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe. “Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam ilitoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa Massawe ili kukabiliana na kesi mbili ikiwamo ya madai ya kughushi nyaraka mbalimbali.
Hati hiyo ilitolewa baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha ombi la kutaka mfanyabiashara huyo arejeshwe nchini kwa kuwa tayari amefunguliwa kesi namba 150/2013.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba alisema kwa agizo hilo, polisi kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliandika barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Dubai kuangalia taratibu za kisheria za kumrudisha baada ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
“Massawe alifikishwa mahakamani Dubai kwa makosa ya kukutwa na hati bandia za kusafiria, lakini vilevile kugundulika kuwa ni kati ya watu wanaotafutwa na Polisi wa Interpol kwa tuhuma za mauaji,” alisema Manumba.
“Sheria inasema mtu akikamatwa nchi nyingine, anashtakiwa nchini humo, huku taratibu za kisheria za kumrejesha zikiendelea kwa nchi ambazo zina utaratibu wa kubadilishana wafungwa kama ilivyo Tanzania na UAE,” alisema Manumba.
Alisema ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo umekamilika na tayari umewasilishwa Dubai ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria za kumrejesha Tanzania haraka kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kutajwa mahakamani
Aprili 4, mwaka huu, Massawe alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.


Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshtakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.

SERENA WILLIAMS ANYAKUWA TAJI LA U.S OPEN








Mcheza tenisi wa Marekani, Serena Williams akirudisha mpira kwa nyota wa Belarus, Victoria Azarenka wakati wa fainali ya US Open kwa wanawake iliyochezwa USTA Billie Jean King National Tennis Center, New York. Picha na AFP. 



Mchezaji namba moja kwa ubora duniani, Serena Williams ametwaa taji lake la tano la US Open kwa kumchapa Victoria Azarenka kwenye Uuwanja wa Flushing Meadows.
Mmarekani huyo mwenye miaka 32, alitumia nguvu ya ziada kushinda kwa 7-5 6-7 (6-8) 6-1 dhidi ya nyota wa Belarusian.
Williams ametwaa mataji17 Grand Slam kwa mchezaji moja moja, na kuwa pamoja na Martina Navratilova na Chris Evert, huku akiwa nyuma kwa mataji saba kwa Margaret Court anayeshikilria rekodi ya mataji 24.
Baada ya kuruhusu kupoteza seti mbili, na mara mbili akishindwa kuanzisha vizuri, Williams
alibadilika na kuonyesha mchezo wa kiwango cha juu kuliko ilivyokuwa katika fainali 16
zilizopita.
“Vika ni mpinzani bora, ameonyesha uwezo mkubwa wa kupigana wakati wote wa mchezo,
nadhani hii ni sababu iliyomfanya akatwaa mataji mengi ya Grand Slams,” alisema Williams
kuhusu mpinzani wake Azarenka.
Azarenka, 24, amefungwa mara mbili na Williams mwaka hjuu kwanza ni katika mashindano ya Cincinnati na sasa US Open

PANGA PANGUA UVCCM

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI



Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya mkutano wa Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji hao na kwamba kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa na Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita lakini kwa kuwa tulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba suala hili lisogezwe mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji hao walikuwa wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya, wameona ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni inayotoa mamlaka kwa Kamati ya Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo inabidi sasa tuweke kwanza mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa watathibishwa,” alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao, kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini, shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu wengine,” alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya, Mapunda ambaye mara baada ya kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika taasisi ambayo yeye ni mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha majina ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya kuthibitishwa.
Vikao vya Siri


Habari kutoka katika mkutano wa Zanzibar zilisema kuwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Kinana alinukuliwa akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara hivyo alishauri suala hilo lipangwe kuzungumzwa katika mkutano wa Oktoba utakaofanyika Dodoma.
Baada ya mkutano wa Baraza Kuu, baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa, waliripotiwa kuendesha vikao vya siri katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku kundi kubwa likitajwa kupanga mikakati ya kuhakikisha Sadifa anang’oka.
Miongoni mwa hoja zinazojengwa dhidi ya mwenyekiti huyo ni pamoja na hiyo ya ukiukwaji wa kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara, hasa Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za Umoja huo kwa kuwatangaza kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo alipaswa kushirikiana nayo, kabla ya kuridhiwa na Baraza Kuu.
Wajumbe wengi watatumia kusimama kazi kwa watumishi hao kama hoja ya kuthibitisha kuwapo kwa makosa ya kiutendaji, hivyo watahoji iwapo kuna sababu za UVCCM “kuendelea kuwa na mwenyekiti ambaye hawezi kuzingatia kanuni na miongozo katika utendaji wake”.
Tuhuma nyingine ambazo zimekuwa zikizungumzwa dhidi ya Sadifa ni matumizi mabaya ya fedha za Umoja huo pamoja na kukodi walinzi binafsi watano; wawili Tanzania Bara na watatu Zanzibar, ambao wamekuwa wakilipwa na UVCCM.
Jana Sadifa alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo mpya alisema: “Hayo masuala mimi bwana siyataki, chochote unachopewa wewe andika unavyojua”.
Aliongeza:“Ukiwa na issue (suala) yoyote inayohusu Umoja wa Vijana, wewe mtafute Katibu Mkuu, hata kama hayo mambo yananihusu mimi, wewe usinitafute mimi, mtafute Katibu Mkuu yeye nimempa mamlaka ya kuwa msemaji mkuu.”
Naye Mapunda alipoulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya bosi wake alisema hawezi kuzungumzia matumizi mabaya ya fedha kwani hana taarifa.
“Tangu niteuliwe sijamaliza hata siku saba, kwa hiyo niwe muwazi tu kuwa sina taarifa nayo na sasa siwezi kusema fedha zilivyotumika,” alisema Mapunda.
Kuhusu suala la walinzi (mabaunsa),Mapunda alisema hao si sehemu ya watumishi aliokabidhiwa na kwamba jumuiya hiyo haina waajiriwa wa aina hiyo.

WANASWA NA DAWA ZA KULEVYA ETHIOPIA

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI


Mshambuliaji wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6bilioni.
Aidha, hilo limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125 bilioni).
Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo alithibitisha jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki akidaiwa kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa kifungo cha miaka tisa hadi 15.
Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.
“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa na mtu mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya yeye ni kuubeba tu. Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndipo warudi Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndipo hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa tena Jumanne (leo) na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado unaendelea.”
Wanamichezo hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za kupandia ndege baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi.


“Kilichotokea ni jambo la aibu kwa nchi na hata wachezaji wenyewe wanajuta. Kwa mfano, Kaniki anasema alikuwa aende England kucheza mpira Desemba lakini sisi tukamwambia hatuwezi kumsaidia inabidi akabiliane na kesi iliyoko mbele yake. Mkwanda yeye ametuambia kwamba anaishi Sweden hatuna maelezo yake zaidi,” alisema Shelukindo na kuongeza kuwa wamewapelekea wanamichezo hao msaada wa mablanketi kwa vile bado wako mahabusu na Ethiopia kwa sasa kuna baridi kali.
Shelukindo alisema wachezaji hao wapo mahabusu kwenye Kituo cha Polisi cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (Federal Police Crime Investigation) na hawana chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa.
Watanzania wengine kuachiwa leo
Shelukindo alisema kuna Watanzania wanne wanaotazamiwa kuachia leo baada ya kumaliza vifungo vyao baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.
“Kuna Watanzania wengine walinaswa hapa miaka ya nyuma wao walikuwa wamemeza wakapasuliwa dawa zikatolewa na baadhi yao walifariki. Hata hivyo, wanne ambao wamemaliza vifungo vyao vya miaka minne wanaweza kurudishwa Tanzania,” alisema Shelukindo.

Tuesday, September 3, 2013

RWANDA YAJITETEA KUHUSU USHURU




Wakati ushuru wa magari makubwa ukiwa umeshushwa kwa wiki moja, Serikali ya Rwanda imejitetea ikisema haijafanya hujuma yoyote dhidi ya Tanzania, bali imepandisha tozo hiyo ili kuifanya ilingane na ile inayolipwa Tanzania.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake jana, Balozi wa Rwanda nchini, Ben Rugangazi alisema kuongezwa kwa ushuru huo wa forodha kisichukuliwe kama jaribio la kutaka kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Balozi Rugangazi alisema Rwanda imeamua kupandisha kiwango chake kutoka Dola za Marekani 152 (Sh240,000) kuwa Dola 500 (Sh790,000) ambazo pia hutozwa na Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu.
“Kumekuwa na majadiliano ya muda mrefu ili kuleta ulinganifu wa ushuru wa forodha kwani kwa muda mrefu wafanyabiashara Rwanda wamekuwa wakilalamika kutokana na kushindwa kushindana vizuri kwenye soko la biashara kutokana na tofauti kubwa ya ushuru wa forodha.
“Hili suala tulishawahi kuliwasilisha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tukawaomba wasaidie kurekebisha kasoro hiyo, lakini hawakufanya hivyo. Sasa tumeamua kuchukua hatua hii ili kwenda sambamba na wenzetu Tanzania.
“Pande zote Tanzania na Rwanda zilikubaliana kuwa ushuru mpya ungeanza kutumika Septemba mwaka huu na ndivyo ilivyokuwa,” alisema Balozi Rugangazi.
Siku saba
Kutokana na msongamano wa malori kwenye mpaka wa nchi hizo mbili, Serikali ya Rwanda imeshusha ushuru kwa wiki moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ushuru unaotumika ni ule wa zamani badala ya mpya.
Tizeba alisema alishauriana na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba na kukubaliana ushuru wa zamani utumike wakati Serikali hizo zikiendelea na mashauriano. Alisema Mawaziri wa Fedha wa Tanzania na Rwanda walitazamiwa kukutana ili kuzungumzia suala hilo.
Dk Tizeba alisema juzi wafanyabiashara wa Tanzania walipata usumbufu mkubwa baada ya kulazimika kulipa Dola 500 kuingiza mizigo yao Rwanda badala ya Dola 152.
Hata hivyo, alikanusha madai kuwa Rwanda imepandisha ada hizo kutokana na mgogoro wa kisiasa baina ya nchi hizo.


Hali mbaya Rusumo
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika mpaka wa nchi hizo huko Rusumo kutokana na kuwapo kwa msururu mkubwa wa magari ambao unaelezwa kuwa hadi jana ulikuwa umefikia kilometa 20.
Akizungumza kwa simu kutoka Rusumo, Ngara jana, Ofisa Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji mpakani hapo, Mahirande Samuel alisema hali hiyo inatokana na madereva wengi kutokuwa na taarifa ya ongezeko hilo.
“Hali ni mbaya, kwa sasa foleni ya magari imefika hadi Benaco ambako ni umbali wa kilometa 20… Unajua hawa madereva hawakuwa na taarifa na wengi walikuwa wakitoa ushuru wa zamani, pengine wameamua kusubiri mabosi wao wawaongezee fedha,” alisema Samuel.
Haiondoki Bandari ya Dar lakini...
Kuhusu utumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam balozi huyo alisema Serikali yake haina mpango wa kuikacha bandari hiyo, lakini akasisitiza: “Sisi tunaangalia fursa za kiuchumi, tutapenda kutumia bandari yenye ufanisi na ambayo haina usumbufu kwetu. Tutaendelea kutumia bandari zote hii ya Dar es Salaam na ile ya Mombasa lakini tungependelea zaidi kuona tunatumia ile yenye ufanisi zaidi.”

UVCCM KWACHAFUKA

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI








Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Sadifa Juma akizungumza katika mkutano wa umoja huo mjini Zanzibar.Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi na Katibu Mkuu wa CCM, Adulrahman Kinana. Picha ya CCM



Mvutano mkubwa umeibuka ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu kilichokuwa kikifanyika Zanzibar juzi, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi kutofikia mwisho kutokana na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Sadifa anadaiwa kukiuka Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za UVCCM kwa kutangaza uteuzi wa wakuu wa idara tatu za umoja huo, kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo kimsingi alipaswa kushirikiana nayo kuwateua, kabla ya kuidhinishwa na baraza kuu.
Habari kutoka katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi ya CCM, Kisiwandui zinasema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Inaelezwa pia kuwa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM, Sixtus Mapunda naye alionja chungu ya mgogoro huo pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea mwenyekiti wake.
Hata hivyo, Sadifa na Mapunda kwa nyakati tofauti jana walisema kuwa mkutano huo ulimalizika bila tatizo na ulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu Mkuu jambo ambalo lilifanyika kama ilivyokuwa imepangwa.
“Kwa mujibu wa kanuni, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kufungua na kufunga kikao na vyote hivyo tulifanya, hakuna kikao kilichovunjika,” alisema Sadifa.
Alipotakiwa kueleza kuhusu kanuni anayodaiwa kuivunja, alikataa kuzungumzia suala hilo akitaka kwanza mwandishi amwambie chanzo chake cha habari.
“Nani huyo aliyetaka nitoke, wewe nisikilize, kuna watu ambao wanajua kabisa unataka kuzungumza nini hata kabla hujasema na mmoja wa watu hao ni Sadifa kwa hiyo nilishajua kabisa ni nini unataka,” alisema Sadifa na baada mwandishi kuendelea kumuuliza maswali alikata simu.
Kwa upande wake, Mapunda alisema: “Mkutano ulifanyika na kumalizika kama ulivyokuwa umepangwa. Ule ulikuwa ni mkutano maalumu na ulikuwa na ajenda moja tu, mwenyekiti aliufungua na kuufunga kama ilivyokuwa imepangwa. Ajenda ilikuwa ni kunithibitisha mimi tu (kuwa katibu wa UVCCM) na baada ya hilo kufanyika nilikaribishwa na mimi nikazungumza na nikamaliza”.
Ilikuwaje?


Habari zinasema wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Ruvuma, Alex Nchimbi walikuwa wakilalamika kwamba Sadifa alikiuka kanuni katika kuteua wakuu hao wa idara hivyo uwepo wao katika kikao cha baraza hilo haukuwa halali.
Katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, Nchimbi alimtaka Sadifa na wajumbe wote wa Kamati ya Utekelezaji watoke nje, ili Baraza Kuu liwajadili.
“Sadifa alikataa na badala yake alimwambia Nchimbi akae chini la sivyo angemtoa nje ya mkutano hali ambayo ilizua mvutano mkali kwa sababu wajumbe wengine walisimama kumpinga Sadifa na wachache walikuwa wakimtetea,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho. Kutokana na hali hiyo, Kinana aliingilia kati na kuwaomba viongozi wa UVCCM waende faragha kwa muda ili wakajadiliane na waliporejea aliwatangazia wajumbe kwamba wamekubaliana kuwa kikao hicho kiahirishwe ili kiitishwe kingine mwezi ujao kwa ajili ya kuzungumzia pamoja na mambo mengine, uteuzi huo.
Habari hizo zilimnukuu Kinana akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara aliowatangaza katika kikao cha Baraza Kuu cha Februari Mjini Dodoma.
“Kitaitishwa kikao kingine Dodoma mwezi wa 10 (Oktoba) ili tuweze kukamilisha taratibu hizo, lakini wewe subiri utaona tutakamilisha uteuzi halafu yeye naye (Sadifa) atang’oka maana hatuwezi kukaa na mwenyekiti ambaye hajui kanuni,” alisema mjumbe mwingine.
Kwa uamuzi huo, sasa ni dhahiri kwamba Baraza Kuu la UVCCM, limetengua uteuzi wa watendaji hao wa Idara za Oganaizesheni, Fedha na Uchumi na ile ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Habari zaidi zinasema kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi katika kikao hicho na kila mjumbe alifanyiwa ukaguzi wa hali ya juu ikidaiwa kwamba ilikuwa ni kuwabaini wajumbe ambao walikuwa wamepanga kuingia na silaha.
Fedha na simu
Kada wa CCM ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM lililopita, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kugawa kwa kificho fedha kiasi cha Sh100,000 kwa kila mjumbe wa wa mkutano huo lengo likiwa ni kumwokoa Sadifa.
Inadaiwa kwamba mbali na fedha hizo, pia wajumbe walikodiwa usafiri wa boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam na baadhi yao kulipiwa gharama za vyumba vya kulala na chakula.
Kadhalika, wajumbe wote wa kikao hicho walizawadiwa simu aina ya Samsung Galax na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ili ‘kurahisiaha mawasiliano’ miongoni mwao, kitendo ambacho pia kinapewa tafsiri kwamba huenda kuna ajenda nyuma ya simu hizo.

Makamba alikiri kugawa simu hizo lakini akasema ilikuwa sehemu ya kutekeleza ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM uliofanyika Dodoma Februari 16, mwaka huu ambao wajumbe hao waliomba kupewa simu hizo.
Alisema katika mkutano huo, alialikwa kutoa mada na alizungumzia suala la matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukijenga chama na baadhi ya wajumbe walisema wanashindwa kutumia njia hiyo kwa kuwa wapo mbali na maeneo ya mijini.
Alisema kabla ya kutoa simu hizo, umoja huo ulimkumbusha kuhusu ahadi yake kutokana na barua yenye kumbukumbu namba VMM/M.30/39/Vol.17/35 ambayo pia ilimwalika kuhudhuria kwenye mkutano wa juzi.
Makamba alisema ili kutimiza ahadi hiyo, alizungumza na baadhi ya makada wenzake na kuwaomba wamsaidie.
“Nilifanya kaharambee kadogo, mtu ukiombwa na wewe unahangaika huku na huko, walinipa na jana (juzi) tuligawa simu 138,” alisema.
Mgogoro UVCCM
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge, aliwahi kulalamika kuhusu kuwapo kwa kundi la vijana wapatao 10 kutoka mikoa mbalimbali ambao wamekuwa wakimpiga vita na kuingilia utendaji wa kazi zake kinyume cha katiba ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Sadifa amekuwa akilaumiwa na baadhi ya wanachama wa UVCCM kwamba ameshindwa kazi na badala yake amekuwa akitoa lugha chafu mbele ya vikao dhidi ya wajumbe ambao wamekuwa wakihoji mambo yanavyokwenda.
Baada ya kuchaguliwa, Sadifa na Makamu wake, Mboni Mhita walipingwa kwa mabango mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na madai kwamba uchaguzi uliowaweka madarakani uligubikwa na rushwa.