Massawe anayetarajiwa kuletwa nchini wakati wowote
kuanzia sasa, alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu
na alikamatwa Dubai, mapema Julai na maofisa wa usalama wa UAE baada ya
alama zake za vidole kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu
waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Baada ya kukamatwa, Mkuu wa Interpol, Tawi la
Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema
Massawe alikamatwa kati ya Juni 20 na 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Massawe ambaye anafanya biashara zake katika Miji
ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba akiwa Dubai, alikutwa
na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati
alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe. “Ombi la kuleta
mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina hatua
ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima
Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo
ili aletwe,” alisema Babile.
Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu
Dar es Salaam ilitoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa Massawe
ili kukabiliana na kesi mbili ikiwamo ya madai ya kughushi nyaraka
mbalimbali.
Hati hiyo ilitolewa baada ya Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha ombi la kutaka mfanyabiashara huyo
arejeshwe nchini kwa kuwa tayari amefunguliwa kesi namba 150/2013.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba alisema kwa
agizo hilo, polisi kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliandika
barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Dubai kuangalia taratibu za kisheria za
kumrudisha baada ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
“Massawe alifikishwa mahakamani Dubai kwa makosa
ya kukutwa na hati bandia za kusafiria, lakini vilevile kugundulika kuwa
ni kati ya watu wanaotafutwa na Polisi wa Interpol kwa tuhuma za
mauaji,” alisema Manumba.
“Sheria inasema mtu akikamatwa nchi nyingine,
anashtakiwa nchini humo, huku taratibu za kisheria za kumrejesha
zikiendelea kwa nchi ambazo zina utaratibu wa kubadilishana wafungwa
kama ilivyo Tanzania na UAE,” alisema Manumba.
Alisema ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo
umekamilika na tayari umewasilishwa Dubai ili kuendelea na taratibu
nyingine za kisheria za kumrejesha Tanzania haraka kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kutajwa mahakamani
Aprili 4, mwaka huu, Massawe alitajwa mahakamani
katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa
katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake
Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara
maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshtakiwa mwingine, Makongoro
Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome
mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa
kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao
lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa
ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe
akamatwe.
No comments:
Post a Comment