Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba
kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa
madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba
vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya mkutano wa
Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za
Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na
yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda
alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji hao na kwamba
kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa na
Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao
kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili
suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita lakini kwa kuwa tulikuwa na
ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba suala hili lisogezwe
mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji hao walikuwa
wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya, wameona
ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni inayotoa mamlaka kwa Kamati ya
Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo inabidi sasa tuweke kwanza
mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa watathibishwa,”
alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili
zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao,
kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar
kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini,
shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba
hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu
wengine,” alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka
kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni
mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya, Mapunda ambaye mara baada ya
kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika taasisi ambayo yeye ni
mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu
kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta
katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha
majina ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya
kuthibitishwa.
Vikao vya Siri
Habari kutoka katika mkutano wa Zanzibar zilisema kuwa, Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya
kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Kinana alinukuliwa akikiri kufanyika kwa makosa
katika uteuzi wa wakuu wa idara hivyo alishauri suala hilo lipangwe
kuzungumzwa katika mkutano wa Oktoba utakaofanyika Dodoma.
Baada ya mkutano wa Baraza Kuu, baadhi ya
wenyeviti wa UVCCM wa mikoa, waliripotiwa kuendesha vikao vya siri
katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku kundi kubwa
likitajwa kupanga mikakati ya kuhakikisha Sadifa anang’oka.
Miongoni mwa hoja zinazojengwa dhidi ya mwenyekiti
huyo ni pamoja na hiyo ya ukiukwaji wa kanuni za uteuzi wa wakuu wa
idara, hasa Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za Umoja huo kwa
kuwatangaza kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo alipaswa
kushirikiana nayo, kabla ya kuridhiwa na Baraza Kuu.
Wajumbe wengi watatumia kusimama kazi kwa
watumishi hao kama hoja ya kuthibitisha kuwapo kwa makosa ya kiutendaji,
hivyo watahoji iwapo kuna sababu za UVCCM “kuendelea kuwa na mwenyekiti
ambaye hawezi kuzingatia kanuni na miongozo katika utendaji wake”.
Tuhuma nyingine ambazo zimekuwa zikizungumzwa
dhidi ya Sadifa ni matumizi mabaya ya fedha za Umoja huo pamoja na
kukodi walinzi binafsi watano; wawili Tanzania Bara na watatu Zanzibar,
ambao wamekuwa wakilipwa na UVCCM.
Jana Sadifa alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo
mpya alisema: “Hayo masuala mimi bwana siyataki, chochote unachopewa
wewe andika unavyojua”.
Aliongeza:“Ukiwa na issue (suala) yoyote inayohusu
Umoja wa Vijana, wewe mtafute Katibu Mkuu, hata kama hayo mambo
yananihusu mimi, wewe usinitafute mimi, mtafute Katibu Mkuu yeye nimempa
mamlaka ya kuwa msemaji mkuu.”
Naye Mapunda alipoulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya
bosi wake alisema hawezi kuzungumzia matumizi mabaya ya fedha kwani hana
taarifa.
“Tangu niteuliwe sijamaliza hata siku saba, kwa
hiyo niwe muwazi tu kuwa sina taarifa nayo na sasa siwezi kusema fedha
zilivyotumika,” alisema Mapunda.
Kuhusu suala la walinzi (mabaunsa),Mapunda alisema
hao si sehemu ya watumishi aliokabidhiwa na kwamba jumuiya hiyo haina
waajiriwa wa aina hiyo.
No comments:
Post a Comment