Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Sadifa Juma akizungumza katika mkutano wa umoja huo mjini Zanzibar.Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi na Katibu Mkuu wa CCM, Adulrahman Kinana. Picha ya CCM
Mvutano mkubwa umeibuka ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu
kilichokuwa kikifanyika Zanzibar juzi, ambacho mgeni rasmi alikuwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ),
Balozi Seif Ali Iddi kutofikia mwisho kutokana na baadhi ya wajumbe
kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka nje ili wajadiliwe
kwa kukiuka kanuni.
Sadifa anadaiwa kukiuka Ibara ya 91 ya toleo la
nane la Kanuni za UVCCM kwa kutangaza uteuzi wa wakuu wa idara tatu za
umoja huo, kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo kimsingi
alipaswa kushirikiana nayo kuwateua, kabla ya kuidhinishwa na baraza
kuu.
Habari kutoka katika mkutano huo uliofanyika
katika Ofisi ya CCM, Kisiwandui zinasema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya
baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Inaelezwa pia kuwa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM,
Sixtus Mapunda naye alionja chungu ya mgogoro huo pale alipopingwa
vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea mwenyekiti wake.
Hata hivyo, Sadifa na Mapunda kwa nyakati tofauti
jana walisema kuwa mkutano huo ulimalizika bila tatizo na ulikuwa na
ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu Mkuu jambo ambalo lilifanyika
kama ilivyokuwa imepangwa.
“Kwa mujibu wa kanuni, mwenyekiti ndiye mwenye
mamlaka ya kufungua na kufunga kikao na vyote hivyo tulifanya, hakuna
kikao kilichovunjika,” alisema Sadifa.
Alipotakiwa kueleza kuhusu kanuni anayodaiwa
kuivunja, alikataa kuzungumzia suala hilo akitaka kwanza mwandishi
amwambie chanzo chake cha habari.
“Nani huyo aliyetaka nitoke, wewe nisikilize, kuna
watu ambao wanajua kabisa unataka kuzungumza nini hata kabla hujasema
na mmoja wa watu hao ni Sadifa kwa hiyo nilishajua kabisa ni nini
unataka,” alisema Sadifa na baada mwandishi kuendelea kumuuliza maswali
alikata simu.
Kwa upande wake, Mapunda alisema: “Mkutano
ulifanyika na kumalizika kama ulivyokuwa umepangwa. Ule ulikuwa ni
mkutano maalumu na ulikuwa na ajenda moja tu, mwenyekiti aliufungua na
kuufunga kama ilivyokuwa imepangwa. Ajenda ilikuwa ni kunithibitisha
mimi tu (kuwa katibu wa UVCCM) na baada ya hilo kufanyika nilikaribishwa
na mimi nikazungumza na nikamaliza”.
Ilikuwaje?
Habari zinasema wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM,
Mkoa wa Ruvuma, Alex Nchimbi walikuwa wakilalamika kwamba Sadifa
alikiuka kanuni katika kuteua wakuu hao wa idara hivyo uwepo wao katika
kikao cha baraza hilo haukuwa halali.
Katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa
UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, Nchimbi alimtaka Sadifa na wajumbe
wote wa Kamati ya Utekelezaji watoke nje, ili Baraza Kuu liwajadili.
“Sadifa alikataa na badala yake alimwambia Nchimbi
akae chini la sivyo angemtoa nje ya mkutano hali ambayo ilizua mvutano
mkali kwa sababu wajumbe wengine walisimama kumpinga Sadifa na wachache
walikuwa wakimtetea,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho. Kutokana
na hali hiyo, Kinana aliingilia kati na kuwaomba viongozi wa UVCCM
waende faragha kwa muda ili wakajadiliane na waliporejea aliwatangazia
wajumbe kwamba wamekubaliana kuwa kikao hicho kiahirishwe ili kiitishwe
kingine mwezi ujao kwa ajili ya kuzungumzia pamoja na mambo mengine,
uteuzi huo.
Habari hizo zilimnukuu Kinana akikiri kufanyika
kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara aliowatangaza katika kikao
cha Baraza Kuu cha Februari Mjini Dodoma.
“Kitaitishwa kikao kingine Dodoma mwezi wa 10
(Oktoba) ili tuweze kukamilisha taratibu hizo, lakini wewe subiri utaona
tutakamilisha uteuzi halafu yeye naye (Sadifa) atang’oka maana hatuwezi
kukaa na mwenyekiti ambaye hajui kanuni,” alisema mjumbe mwingine.
Kwa uamuzi huo, sasa ni dhahiri kwamba Baraza Kuu
la UVCCM, limetengua uteuzi wa watendaji hao wa Idara za Oganaizesheni,
Fedha na Uchumi na ile ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Habari zaidi zinasema kulikuwa na ulinzi mkali wa
polisi katika kikao hicho na kila mjumbe alifanyiwa ukaguzi wa hali ya
juu ikidaiwa kwamba ilikuwa ni kuwabaini wajumbe ambao walikuwa
wamepanga kuingia na silaha.
Fedha na simu
Kada wa CCM ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza
Kuu la UVCCM lililopita, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kugawa kwa
kificho fedha kiasi cha Sh100,000 kwa kila mjumbe wa wa mkutano huo
lengo likiwa ni kumwokoa Sadifa.
Inadaiwa kwamba mbali na fedha hizo, pia wajumbe
walikodiwa usafiri wa boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam na baadhi
yao kulipiwa gharama za vyumba vya kulala na chakula.
Kadhalika, wajumbe wote wa kikao hicho
walizawadiwa simu aina ya Samsung Galax na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba ili ‘kurahisiaha mawasiliano’
miongoni mwao, kitendo ambacho pia kinapewa tafsiri kwamba huenda kuna
ajenda nyuma ya simu hizo.
Makamba alikiri kugawa simu hizo lakini akasema ilikuwa sehemu
ya kutekeleza ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM
uliofanyika Dodoma Februari 16, mwaka huu ambao wajumbe hao waliomba
kupewa simu hizo.
Alisema katika mkutano huo, alialikwa kutoa mada
na alizungumzia suala la matumizi ya mitandao ya kijamii katika
kukijenga chama na baadhi ya wajumbe walisema wanashindwa kutumia njia
hiyo kwa kuwa wapo mbali na maeneo ya mijini.
Alisema kabla ya kutoa simu hizo, umoja huo
ulimkumbusha kuhusu ahadi yake kutokana na barua yenye kumbukumbu namba
VMM/M.30/39/Vol.17/35 ambayo pia ilimwalika kuhudhuria kwenye mkutano wa
juzi.
Makamba alisema ili kutimiza ahadi hiyo, alizungumza na baadhi ya makada wenzake na kuwaomba wamsaidie.
“Nilifanya kaharambee kadogo, mtu ukiombwa na wewe
unahangaika huku na huko, walinipa na jana (juzi) tuligawa simu 138,”
alisema.
Mgogoro UVCCM
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge, aliwahi
kulalamika kuhusu kuwapo kwa kundi la vijana wapatao 10 kutoka mikoa
mbalimbali ambao wamekuwa wakimpiga vita na kuingilia utendaji wa kazi
zake kinyume cha katiba ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Sadifa amekuwa akilaumiwa na baadhi ya
wanachama wa UVCCM kwamba ameshindwa kazi na badala yake amekuwa akitoa
lugha chafu mbele ya vikao dhidi ya wajumbe ambao wamekuwa wakihoji
mambo yanavyokwenda.
Baada ya kuchaguliwa, Sadifa na Makamu wake, Mboni
Mhita walipingwa kwa mabango mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye
pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na madai kwamba
uchaguzi uliowaweka madarakani uligubikwa na rushwa.
No comments:
Post a Comment