Tuesday, September 3, 2013

RWANDA YAJITETEA KUHUSU USHURU




Wakati ushuru wa magari makubwa ukiwa umeshushwa kwa wiki moja, Serikali ya Rwanda imejitetea ikisema haijafanya hujuma yoyote dhidi ya Tanzania, bali imepandisha tozo hiyo ili kuifanya ilingane na ile inayolipwa Tanzania.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake jana, Balozi wa Rwanda nchini, Ben Rugangazi alisema kuongezwa kwa ushuru huo wa forodha kisichukuliwe kama jaribio la kutaka kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Balozi Rugangazi alisema Rwanda imeamua kupandisha kiwango chake kutoka Dola za Marekani 152 (Sh240,000) kuwa Dola 500 (Sh790,000) ambazo pia hutozwa na Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu.
“Kumekuwa na majadiliano ya muda mrefu ili kuleta ulinganifu wa ushuru wa forodha kwani kwa muda mrefu wafanyabiashara Rwanda wamekuwa wakilalamika kutokana na kushindwa kushindana vizuri kwenye soko la biashara kutokana na tofauti kubwa ya ushuru wa forodha.
“Hili suala tulishawahi kuliwasilisha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tukawaomba wasaidie kurekebisha kasoro hiyo, lakini hawakufanya hivyo. Sasa tumeamua kuchukua hatua hii ili kwenda sambamba na wenzetu Tanzania.
“Pande zote Tanzania na Rwanda zilikubaliana kuwa ushuru mpya ungeanza kutumika Septemba mwaka huu na ndivyo ilivyokuwa,” alisema Balozi Rugangazi.
Siku saba
Kutokana na msongamano wa malori kwenye mpaka wa nchi hizo mbili, Serikali ya Rwanda imeshusha ushuru kwa wiki moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ushuru unaotumika ni ule wa zamani badala ya mpya.
Tizeba alisema alishauriana na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba na kukubaliana ushuru wa zamani utumike wakati Serikali hizo zikiendelea na mashauriano. Alisema Mawaziri wa Fedha wa Tanzania na Rwanda walitazamiwa kukutana ili kuzungumzia suala hilo.
Dk Tizeba alisema juzi wafanyabiashara wa Tanzania walipata usumbufu mkubwa baada ya kulazimika kulipa Dola 500 kuingiza mizigo yao Rwanda badala ya Dola 152.
Hata hivyo, alikanusha madai kuwa Rwanda imepandisha ada hizo kutokana na mgogoro wa kisiasa baina ya nchi hizo.


Hali mbaya Rusumo
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika mpaka wa nchi hizo huko Rusumo kutokana na kuwapo kwa msururu mkubwa wa magari ambao unaelezwa kuwa hadi jana ulikuwa umefikia kilometa 20.
Akizungumza kwa simu kutoka Rusumo, Ngara jana, Ofisa Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji mpakani hapo, Mahirande Samuel alisema hali hiyo inatokana na madereva wengi kutokuwa na taarifa ya ongezeko hilo.
“Hali ni mbaya, kwa sasa foleni ya magari imefika hadi Benaco ambako ni umbali wa kilometa 20… Unajua hawa madereva hawakuwa na taarifa na wengi walikuwa wakitoa ushuru wa zamani, pengine wameamua kusubiri mabosi wao wawaongezee fedha,” alisema Samuel.
Haiondoki Bandari ya Dar lakini...
Kuhusu utumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam balozi huyo alisema Serikali yake haina mpango wa kuikacha bandari hiyo, lakini akasisitiza: “Sisi tunaangalia fursa za kiuchumi, tutapenda kutumia bandari yenye ufanisi na ambayo haina usumbufu kwetu. Tutaendelea kutumia bandari zote hii ya Dar es Salaam na ile ya Mombasa lakini tungependelea zaidi kuona tunatumia ile yenye ufanisi zaidi.”

No comments:

Post a Comment