Monday, September 2, 2013

MGOGORO WA TANZANIA NA RWANDA

CHANZO CHA HABARI HII NI WANABIDII, (MWANDISHI ELISA MUHINGO)


Mgogoro wa Rwanda na Tanzania: Vyama vya upinzani vinapwaya katika sera za Mambo ya nje:
Watanzania tumo katika kujifunza mfumo wa Vyama vingi. Huku nyuma tumefanya uchaguzi si kwa kuzisikiliza sera za chama ila kwa ushabiki au kupewa hela. Kidogo kidogo tunaelimika na si mbali tutaanza kuchagua kwa kuzipima sera za chama za kutekeleza vipaumbele vya Taifa letu.
 
Hivi karibuni kwa bahati nzuri umejitokeza mgogoro unaoelekea kuuharibu uhusiano wetu na jirani yetu Rwanda. Wala sijakosea kusema bahati nzuri. Nina maana hiyohiyo. Unajua kama kumefunikwa tatizo, kwa hiyo halionekani usiseme uko salama. Likifunuka likawa wazi shukuru. Naachia hapo.
 
Mgogoro huu unaangaliwa kwa namna tofauti. Wapo wanaouangalia kuanzia Rais wetu alipozishauri nchi zenye mogogoro na vikundi vilivyo msituni kujadiliana. Baada ua ushauri huo Rwanda si ilikataa ushauri tu bali iliamua kumshambulia Rais wetu. Wanaouangalia mgogoro huo kuanzia hapo wengine wanamlaumu Rais kwa nini alisema hivyo. Wanaouangalia mgogoro huu kuanzia nyuma wanamuelewa Rais wetu na wanaishtuka Rwanda na mikakati yake inayoileta katika kutaka kuidhoofisha Tanzania.
 
Katika jambo hili Watanzazania wengi tumekuwa na misimamo tofauti. Lakini kitu kimoja mimi nafikiri nimekipata ni misimamo ya Vyama vya upinzani kuhusu jambo hili. Nasikitika ku conclude kuwa vyama hivi vimeonyesha kupwaya au labda havina msimamo na vyenyewe vinaangalia namna ya kuing’oa CCM hivyo kazi ni kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali yake. Nitatumia vyeo ua vyama badala ya majina ya wahusika. Chadema walimkosoa Rais kwa kuishauri Rwanda kuzungumza na FDLR wakati yeye hajaongea na wapinzani wake. Mtu au chama kulinganisha hali hizi mbili ni dalili ya kupwaya kukubwa. Wapinzani wa Tanzania wanatumia majukwaa wanalindwa na polisi katika mikutano hata kama polisi hao wametumiwa vibaya. Huwezi kulinganisha hali hii ya Rwanda ambako wapinzani wa Rais wake wako gerezani na wengine wako misitu ya nchi jirani. Kumlaumu Kikwete kwa kutowakutanisha ni dalili ya utata katika kufikiri. Kikwete ameshauri viongozi wa nchi hizi wazungumze. Bila shaka nchi hizo zingeonyesha dalili ya kuukubali ushauri Kikwete angekwenda mbele kuandaa mazingira. Utamlaumuje kwa kutowakutanisha wakati aliposhauliwa jibu la kwanza ni kumuita mpuuzi?
 
Nimemsikia Kiongozi wa Upinzani Bungeni akimuuliza Waziri Mkuu kuhusu mgogoro huu. Anashauri utafutwe usuruhishi kwa sababu sera ya nchi hii sio kugombana na majirani. Nimekuwa na mashaka na hoja yake. Sijui ana maana gani kusema si sera ya nchi yetu kutogombana na majirani. Ana maana hata Idi Amin alipotuvamia haikuwa sahihi kumfukuza maana si sera yetu kugombana? Huenda anamlaumu na baba wa taifa kugombana na wareno Mozambique na Smith Rhodeshia.
 
Mtu yeyote wa Kawaida anayeona kinachoendelea DRC hasa eneo la mashariki mwa nchi hiyo atamlaumu Rais wetu kwa kwenda polepole. Mtu yeyote atajua asipochukua hatua mapema kitu kama hicho kitakuja tokea Tanzania miaka mingi ijayo. Lazima Kiongozi mwenye Vision atataka kuisaidia DRC kuondokana na mgogoro huo ili kuifundisha nchi jirani isije ichezea Tanzania huko mbele. Kutaka Tanzania isitengwe namajirani kwa maana ya kuuacha mgogoro miaka mingi ijayo ni kupwaya kwa vyama vyetu katika kuyashughulikia mambo ya nje. Nilitegemea katika hili watanzania wote kuungana na Rais wetu na kuangalia anachukua hatua gani. Vyama vyetu kuliangalia jambo hili kwa umbali wa futi tatu ni kutufanya tuwe na mashaka navyo. Hata kama kwa mfano vyama hivyo vimetuonyesha uwezekano wa kulikomboa taifa letu kuondokana na uongozi ulioshindwa kuudhibiti ufisadi. Unatumia kodi zetu kuendesha serikali kubwa kuliko uwezo wetu. Wananchi wanazidi kuwa maskini huku viongozi wakiwa na mrupurupu kibao. (Na kwa kweli katika hili nawapongeza wapinzani hasa CHADEMA). Lakini kutoonyesha watalindaje heshima ya taifa letu ni sababu tosha ya kuwafaya watanzania wawaimarishe kuwa wapinzani lakini sio kuliongoza Taifa. Tena kama katiba ijayo itampunguzia madaraka Rais kuamua mambo basi kwangu heri kuendelea na uongozi uliopo kuliko kuweka madarakani chama kutakachoharibu sera za nje. Kumbuka sasa Tanzania inatengwa kwa sababu imemwambia Kagame apatane na wanyarwanda wenzake. Tukisema Kikwete aombe msamaha ili wasitutenge, siku tukisema tudhibiti Tanzanite. Kenya wakasema tuwatenge tumwambie rais aombe radhi aseme basi endelea kuchimba. Nina uvumi kuwa Tin bora duniani inatoka wilayani Kyerwa, Mkoani Kagera. Inapochimbwa inauzwa Rwanda kimagendo na Rwanda inaiuza nje. Nje inajulikana Tin bora inatoka Rwanda. Habari za maandalizi ya Bahima Empire hazikuwahi kukanushwa kikamilifu. Rwanda iliwahi kudai sehemu ya Karagwe kuwa ni yake. Sababu wakazi wengi wa eneo hilo ni wanyarwanda. Banyamulenge wanapigana magaribi mwa DRC kutetea maslahi ya watutsi. Kiongozi wa Upinzani alipoibaha serikali kutaka kuacha kugombana na Rwanada aliyafikiria hayo? Anaiwazia Tanzania hadi miaka kumi akiwa rais? Kwanini kiongozi wa upinzani hakumuelewa Waziri Mkuu aliposema jambo hili linahitaji busara? Ni dalili ya kupwaya kwa vyama hivi katika jambo hili. Wasipoangalia CCM itawapiku maana ni jambo nyeti. Wasipoangalia majirani zetu wanafikiri nini juu ya nchi yetu, badala yake wakashikilia wanachosema, ipo siku watalitumbukiza taifa katika mgogoro mkubwa zaidi ya uharibifu wa ufisadi. Hatutawapa nchi. Wajiangalie na watuonyeshe kuwa wamepaona.


No comments:

Post a Comment