Friday, September 27, 2013

MPANGO WA USHAURI WA BIASHARA

CPM Business Consultants imeandaa mpango kabambe wa ushauri wa biashara (Mentorship) kwa wafanyabiashara wadogo wa kati na wakubwa na wale wanaotaka kuanzisha biashara ili kuwawezesha kuwa wafanyabiashara wakubwa na wenye mafanikio. Mtu atakakayejiunga na mpango huu atapewa mbinu za hali ya juu za biashara na uwekezaji ambazo zitamuwezesha kuinuka kiuchumi na kuwa mfanyabiashara mkubwa kwa haraka. Mtu yeyote anaweza kujiunga na mpango huu ambao mkataba wake utakuwa ni wa mwaka mmoja mmoja ambao unaweza kurudiwa tena.Kwa nini uchague CPM Business consultants? Tumeweza kuwainua wajasiriamali wengi kwa ushauri wetu. Kitabu chetu cha Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri, kimewainua wajasiriamali wengi wengine ndani ya muda wa miezi 6 hadi mwaka mmoja. Pia tumefanikiwa kuuza nakala 4,000 za kitabu hicho kwa kipindi kifupi kwa sababu kinapendwa sana. Tumeweza kuandaa mpango wa biashara/michanganuo kwa wale walioomba mikopo Benki. Katika kipindi cha miaka 3 iliyopita tumewawezesha wateja wetu kupata mikopo ya sh. milioni 400 toka benki.
Manufaa ya kujiunga na mpango huu;
Utapewa mbinu za hali ya juu za biashara na uwekezaji ambazo zitakuwezesha kuinuka kiuchumi na kuwa mfanyabiashara mkubwa kwa haraka.
Utapata kitabu cha ujasiriamali kilichotungwa na Mshauri wa biashara.
Utajiunga na mafunzo maalum ya ujasiriamali kwa email kipindi chote utakachokuwa umelipia michango.
Utapata ushauri kwa kipindi cha mwaka mmoja bila kulipia gharama yoyote na unaweza kumpigia simu mshauri wakati wowote na kupatiwa ushauri.
Utapewa huduma ya kutangaza biashara yako kwenye mtandao wa Internet wenye wateja 50,000 bila gharama ya ziada.
Utapata ushauri wa kisaikolojia na matatizo ya mahusiano na maisha yanayokukabili.
Gharama ya mpango huu ni Sh. 25,000.00 Elfu ishirini na tano kwa mwaka. Ili kuomba kujiunga na mpango huu tuma sh. 25,000 kwa M PESA kwenye simu namba 0755394701, Kwa maelezo zaidi unaweza kupiga simu au kutuma email kwa cnazi2002@yahoo.com
Tumeamua kutoa bei ndogo tofauti na tangazo letu la mwanzo kutokana na maombi ya wadau wengi kuutaka mpango huu kwa gharama ambazo wanaweza kuzimudu.
CHARLES NAZI
MSHAURI WA BIASHARA
CPM BUSINESS CONSULTANTS

Thursday, September 19, 2013

RAIS KIKWETE:ACHENI KUISEMA NA KUIKEJELI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuisemea, kuijenga na kuitetea nchi yao badala ya kushiriki katika kuikejeli na kuidharaulisha.

Rais Kikwete amesema kuwa kuisemea na kuitetea Tanzania ni wajibu wa kila Mtanzania awe anaishi ndani ya nchi ana ughaibuni.

Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la ajabu kuwa kazi ya kuisemea, kuitetea na kujenga jina zuri la Tanzania inafanywa zaidi na watu wa nje kuliko baadhi ya Watanzania na hasa wale wanaoishi nje ya nchi.

Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu, Septemba 16, 2013, wakati alipokutana na kuzungumza na
Watanzania waishio katika Jimbo la California kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili katikia jimbo hilo na baadaye  katika sehemu nyingine za Marekani.

Rais Kikwete amewaambia Jumuia ya Watanzania katika Hoteli ya Embassy, San Rafael, California: “Ni wajibu wa Watanzania popote walipo kuisemea vizuri na kutetea maslahi ya nchi yao. Ni jambo lisilo na tija kushiriki katika kuilaumu na kuikejeli nchi yetu. Utasikia na kusoma kwenye mablog baadhi ya watu wakisema kuwa ‘hii nchi gani?” amesema Rais Kikwete.

Rais ameongeza: “Siyo tu kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kuisemea Tanzania lakini ni wajibu wetu kusaidia kusukuma maendeleo ya Tanzania. Hakuna mtu mwingine wa kuifanya kazi hii isipokuwa Watanzania. Hii ndiyo nchi yetu. Hakuna nchi nyingine hata kama tunailaumu kiasi gani.”

Amesisitiza: “Kama watu wa nje wako tayari kuisemea nchi yetu, nyie mnashindwaji vipi kuifanya kazi hiyo ya kuitetea nchi nzuri hii? Hivi nani tunamwachia aijenge nchi hii, aitetea nchi hii? Wengine wanathubutu kuuliza ‘Nchi nzuri? Turudi’. Hivi nani ulimwachia akujengee nchi nzuri ili uweze kurudi?”

Rais Kikwete amesema kuwa ni lazima Watanzania wajifunze kutoka kwa wenzao, wakiwemo majirani zao kuhusu namna ya kutetea maslahi ya nchi yao kwa kila jitihada.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

17 Septemba, 2013

Sunday, September 15, 2013

UWEKEZAJI KATIKA GESI NA MAFUTA,MAONI YA REGINALD MENGI

Septemba 7, 2013 nilipokea barua pepe (email) yenye kichwa cha habari kisemacho “ubinafsi/ufisadi wa MENGI na Chuki/Fitina kwenye Maendeleo”.

Aliyetuma email hiyo alijitambulisha kama “CCM TANZANIA” na email ilisambazwa kwa vyombo vya habari, waandishi na watu wengine wengi wakiwamo wanasiasa. Kabla ya hapo nilifowadiwa nakala ya ujumbe (SMS) na watu ambao walitumiwa na Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge inayosema;

“Ambieni Watanzania: Kampuni za Mengi zimeshikilia vitalu 59 vya madini vyenye ukubwa wa mita za mraba 3,752.37 (sq km) Amevishikilia, ameshindwa kuviendeleza. Watanzania wanakosa mapato na ajira! Sasa anataka vitalu vya gesi na mafuta. Je huu ndio uzawa?|

Na

“Mengi hana uzawa bali ubinafsi. Anataka kufanya udalali wa vitalu vya raslimali zetu. Waelezeni Watanzania ukweli huu.”

Vile vile Septemba 5, 2013 Profesa Muhongo akijibu swali la Mwandishi wa habari lililouliza;

“Mhe. Waziri tunataka ufafanuzi kuhusu kauli yako ya hivi karibuni kwamba waTanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika uwekezaji wa gesi asilia. Kwanza kauli hii ni kweli? Pili kauli kwamba Watanzania wanaweza kuwekeza kwenye sekta ya machungwa tu huoni kwamba si kwamba unawavunja moyo bali unadhalilisha wewekezaji wazalendo?”

Na Profesa Muhongo akajibu:

“Kila mtu alitoa mawazo ya sera ya gesi wakiwemo TPSF. Mengi na wenzake wanataka vitalu wafanye ulanguzi wa gesi na mafuta yetu. Tutatoa orodha ya vitalu vya madini vilivyoko mikononi wa Mengi ambavyo anafanya ulanguzi. Ukweli utaonyesha ubabaishaji na ulanguzi wa Mengi wa genge lake.”


Nimeona ni vyema nitumie haki yangu ya kujibu (right of reply), lakini kwa wale wanaohusika kusambaza taarifa hizo kuchafua jina langu wajue kwamba kujibu kwangu hakuondoi haki yangu ya kuchukua hatua za kisheria.


Kuingizwa kwa vitalu vya madini katika hoja ya gesi

Huo ni upotoshwaji wenye lengo la kututoa kwenye hoja ya msingi ya rasilimali yetu ya gesi. Sijawahi kufanya udalali kwenye vitalu vya madini. Huu ni uongo wa hali ya juu.

Tamko la TPSF na majibu ya Profesa Muhongo

Siku ya Agosti 28, 2013 Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) ilifanya kikao chake cha Bodi na baadaye kufanya mkutano na waandishi wa habari. Mambo mengi yalizungumzwa katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa Watanzania (Economic Empowerment).

Kuhusu uwezeshaji Watanzania, mambo muhimu matatu yalijadiliwa na kutolewa mapendekezo. Mambo hayo ni 1) Manunuzi ya Umma (Public Procurement); 2) Ardhi na uvuvi; na 3) suala la gesi asilia.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, mimi nikiwa Mwenyekiti wa TPSF, niliwasilisha maoni ya TPSF kuhusiana na Manunuzi ya Umma, wakati Makamu Mwenyekiti wangu, Salum Shamte, aliwasilisha maoni yetu kuhusiana na sekta ya ardhi na uvuvi na mwishoni Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, aliwasilisha maoni TPSF kuhusiana na gesi asilia.

Katika maoni yake TPSF ilisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi na kushauri kusitishwa ugawaji wa vitalu vya gesi hadi hapo sera ya gesi itakapokua tayari. Mwisho Bwana Simbeye alisema kwamba TPSF itaomba kukutana na Profesa Muhongo kuwasilisha mawazo na mapendekezo ya taasisi hiyo.

Siku chache baada ya TPSF kutoa maoni yake mambo mawili yalitokea. Kwanza Profesa Muhongo alijibu kupitia vyombo vya habari kwamba mpango wa kugawa vitalu vya gesi na kuingia mikataba utaendelea.

Profesa Muhongo pia alisema wazi kwamba hana mpango wa kukutana TPSF, kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda. Matokeo yake Profesa Muhongo hajajibu hoja kuhusiana na barua aliyoandikiwa na TPSF. Binafsi nilishitushwa na msimamo wa Profesa Muhongo kwani Serikali ya awamu ya nne imepiga hatua kubwa katika kudhihirisha kuwa ni “serikali sikivu”. Ingemgharimu nini Profesa Muhongo kukaa na kutusikiliza? Hakuna ambacho angepoteza zaidi ya dakika chache za muda wake.

Jambo la pili ambalo lilitokea ni mimi binafsi kushambuliwa kana kwamba maoni yaliyotolewa kuhusiana na gesi ni maoni yangu binafsi na si ya TPSF. 

Mifano ya mashambulizi dhidi yangu ni kama nilivyoonyesha hapo juu katika email na ujumbe mfupi wa simu (SMS).

Msimamo wa Profesa Muhongo katika gesi ni upi?

Msimamo wa Profesa Muhongo mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ulikuwa ni kutaka kupitishwa kwanza kwa sera ya gesi asilia kabla ya kuendelea na ugawaji wa vitalu vya gesi.
Septemba 2012, Profesa Muhongo alisema;

“Some of the agreements are really shoddy and they need to be revoked” and “I can’t tolerate agreements which are not in the country’s interests but they benefit a few individuals”.
Tafsiri yake ni:

“Baadhi ya mikataba ni ya ovyo, na inahitaji kuvunjwa” na “Sitovumilia mikataba ambayo haina maslahi kwa nchi na inawanufaisha wachache”.
Tanzania orders review of all oil and gas exploration contracts

Baada ya hapo, Profesa Muhongo aliamrisha Bodi mpya ya TPDC kusitisha ugawaji wa vitalu vya gesi ambao ulipangwa kufanyika mwezi Septemba 2012 na kupitia upya mikataba yote. Profesa Muhongo alinukuliwa akisema:

‘Earlier this month, the state-run Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) delayed a licensing round for nine deep-sea oil and gas blocks previously set for this month until a parliamentary vote on a new gas policy in October. "Right now as a country, we are in the gas boom and we don't have gas policy in place.”

[…]

Recent gas strikes off east Africa's seaboard have led to predictions the region could become the third largest exporter of natural gas on the planet.

"Our country is reviewing its policy. Is that something new?" he said. "We want both the companies that are investing in the country and Tanzanians to benefit from the oil and gas projects."

[…]

"This is completely new business to us. We are learning," Muhongo said.’
Tafsiri yake ni:

‘Mwanzoni wa mwezi huu TPDC ilihairisha mchakato wa ugawaji wa vitalu tisa vya gesi asilia vilivyoko baharini hadi hapo Bunge litakapopitisha sera mpya ya gesi iliyowasilishwa bungeni mwezi Oktoba;
"Kwa sasa kama Taifa, tuko katika mazonge ya gesi na hatuna sera ya gesi. 
"Nchi yetu inaandaa sera (ya gesi). Hicho ni kitu kipya?..." 
"Tunataka kampuni zote, kampuni zinazowekeza nchini mwetu na Watanzania tunufaike na miradi ya gesi na mafuta."
"Hii ni biashara mpya kabisa kwetu. Tunajifunza."

UPDATE 2-Tanzania says will not revoke any oil and gas PSAs | Reuters
Zoezi wa la kugawa vitalu vya gesi asilia lilisitishwa lakini hadi sasa matokeo ya kupitia upya mikataba hayajatolewa hadharani.

Miezi michache baadaye, Februari 26, 2013, Profesa Muhongo alisisitiza msimamo wake wa kutaka Tanzania kuwa na sera ya gesi kabla ya kugawa vitalu zaidi. Aliyasema hayo alipokua akihutubia mkutano uliofanyika Chatham House, mjini London. Mkutano huo uliopewa jina “Tanzania: An Emerging Energy Producer”. Ulikuwa na madhumuni ya:


“Tanzania is drawing growing attention as a pivotal country in East Africa for oil and natural gas exploration, having led the region in terms of new discoveries of natural gas in 2012. With known gas reserves of approximately 7.5 billion cubic feet, the potential to transform Tanzania's international standing and domestic electricity production is considerable. However, recent protests against the construction of a pipeline to Dar es Salaam highlight the challenges that Tanzania faces in ensuring that the benefits of its natural resources are widely felt.

Tafsiri yake ni:

“Tanzania inaonyesha kuja juu katika Afrika Mashariki kwa uvumbuzi wa mafuta na gesi asilia baada ya kuongoza kwa uvumbuzi wa gesi asilia mwaka 2012. Ikiwa na wastani wa futi za ujazo bilioni 7.5, ni dhahiri itasaidia Tanzania kupaa katika anga za Kimataifa na kusaidia uzalishaji wa umeme kwa matumizi ya ndani. Hata hivyo, vurugu za hivi karibuni kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam inaashiria changamoto mpya ambazo Tanzania sasa inakabiliana nazo kuhakikisha kwamba manufaa ya gesi asilia yanawafikia watu wengi zaidi wa chini.”

Alichowasilisha Profesa Muhongo katika mkutano huo kwa ufupi kinapatikana katika tovuti hii;

Tanzania as an Emerging Energy Producer | Chatham House: Independent thinking on international affairs
Kama inavyonekana kwenye kiambatanisho, moja ya nyaraka aliyowasilisha Profesa Muhongo inaonyesha kwamba mchakato wa kuanza ugawaji wa vitalu ungeanza baada ya kupitishwa kwa sera ya gesi.
Hadi sasa hatuna sera ya gesi asilia.
Lakini jambo la kushangaza, Profesa Muhongo amebadilika na anataka vitalu vigawiwe kabla ya kuwapo kwa sera gesi.


Sababu za kubadilika kwa Profesa Muhongo hazina mashiko


Profesa Muhongo amenukuliwa na gazeti la Daily News la Agosti 31, 2013 akieleza sababu zake za kutaka vitalu vigawanywe kabla ya kupitishwa kwa sera ya gesi. Sababu kuu alizozisema ni tatu; (1) Ushindani wa soko na majirani zetu akitolea mfano wa Msumbiji (2) Sheria ya mwaka 1960 iliyoanzisha TPDC na Sheria ya Petroli ya mwaka 1980 kwamba zinatosha kusimamia ugawaji wa vitalu akimaanisha sera na sheria mpya zitafuata baada ya ugawaji wa vitalu; na (3) Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika sekta hii akimaanisha waachiwe wageni peke yao.

Maelezo kwamba tunashindana na Msumbiji haya halalishi ugawaji vitalu kabla ya sera. Utafiti wa gesi asilia ni jambo linachokua muda mrefu, ndio maana TPDC wanaingia kwenye mikataba ya muda mrefu (isiyozidi miaka 11 kwenye utafiti na miaka 25 kwenye uchimbaji). Kwa hiyo kusubiri miezi michache ili Bunge letu liidhinishe sera, haiwezi kuathiri ushindani wa kibiashara. Hata nchi Msumbiji anayoizungumzia hivi sasa inapitia upya mpango wake wa uwekezaji katika gesi asilia na kuingiza sera na sheria mpya zitakazo simamia rasilimali hiyo. Katika mahojiano yaliofanyika na jarida la Africa Report mwezi Julai mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati wa Msumbiji, Mh. Abdul Razak Noormahomed, alisema madhumuni ya mabadiliko hayo ni kuwapa kipaumbele wananchi wa Msumbiji.

Mohojiano haya yanapatikana katika anuani ifuatayo:

Extractive industry: The goal is to give an edge to Mozambicans - Noormahomed | Interview). 
Kama nilivyoeleza hapo juu, mara baada ya Profesa Muhongo kuingia wizarani alisema kinaga ubaga kwamba sheria iliyopo haikidhi mahitaji ya sekta ya gesi asilia ndiyo maana akasimamisha ugawaji wa vitalu vya gesi na kuamrisha mikataba ipitiwe upya na sera ipatikane. Leo tunashuhudia Profesa Muhongo akila matapishi yake na kusema kwamba sheria zile zile alizoziponda sasa zinafaa.

Kauli ya Profesa Muhongo kwamba wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza tu kushiriki biashara ya juisi na soda na hawana uwezo wa kushiriki katika biashara ya gesi yao ni dharau. Kigezo gani Profesa Muhongo anatumia kutoa kauli ya jumla yenye kutawaliwa na hisia? Amefanya utafiti gani kupima uwezo wa kifedha wa wafanyabiashara wa kitanzania? Kwa taarifa yake, wapo wafanyabiashara wengi ambao wanaweza kupata fedha kwa ajili ya kuchimba visima vya gesi. 
Ni dhahiri kwamba Profesa Muhongo anathamini tu kampuni za kigeni, anasahau kwamba kuna mifano ya kuwapo kampuni za kigeni ambazo zimekua zikifanya udalali hapa nchini kwa miaka mingi kwenye rasilimali za nchi yetu ikiwa ni pamoja na madini na gesi.

Uzalendo wangu:

Ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi si mzalendo Wantanzania wanafahamu ukweli. Vile vile ningependa kupuuza tuhuma kwamba mimi ni mbinafsi na sipendi maendeleo ya Watanzania wenzangu kwa hili pia Watanzania wanafahamu ukweli.

Kuhusu Kilimanjaro Hoteli na mgogoro na Yussuf Manji n.k, mtizamo wako unategemea wewe upo katika kundi lipi kati ya kundi safi la waadilifu au kundi chafu la wala rushwa. Watanzania wanafahamu msimamo wangu kwenye hili.
Mimi sipingi kuwepo kwa wawekezaje wageni katika sekta ya gesi lakini kuna mambo mawili napigania. Kwanza Watanzania wanufaike na rasilimali yao ya gesi na pili iwepo sera ya gesi inayotoa kipaumbele kwa Watanzania
Mimi napenda maendeleo ya nchi yangu; kwa hiyo hata siku moja siwezi kupinga uwekezaji ama ubia na wawekezaji. Ninachosimamia ni manufaa kwa nchi yangu.

Tuhuma kwamba nafanya kampeni dhidi ya wizara

Tuhuma kwamba nimeandaa kongamano kwa ajili ya vijana wa Chadema si za kweli. Huu ni uzushi usio na kichwa wala miguu. Vile vile madai kwamba naitumia vibaya vyombo vya habari vya IPP Media si ya kweli hata kidogo ikizingatiwa kwamba hata mahojiano ya Profesa Muhongo kwa simu akiwa Austria, yalirushwa na kituo cha redio cha Radio Stereo kinachomilikiwa na kampuni yangu ya ITV-Independent Television Limited.

Hitimisho

Julai mwaka huu, Rais wa Marekani Barack Obama, alihitimisha ziara yake ya Kiserikali nchini Tanzania, kwa kusema;

“Ultimately the goal here is for Africa to build Africa for Africans.”


Akimaanisha kwamba, Hatimaye Lengo ni Africa kujenga Africa kwaajili ya Waafrica

Profesa Muhongo asipingane na ushauri huu mzuri.
Nimalizie kwa kuwahakikishia Watanzania kwamba mashambulizi binafsi dhidi yangu yenye nia mbaya ya kunishushia heshima hayatakaa yafanikiwe.
Wenu,

Dk. Reginald A. Mengi

KAULI YA ISMAIL JUSSA KUHUSU KUMWAGIWA TINDIKALI PADRI MWANG'AMBA

KAULI YA ISMAIL JUSSA


Kwa mara nyengine tena leo hii kumetangazwa kutokea tukio la kumwagiwa acid ambapo imeelezwa jioni hii Padri Joseph Magamba amemwagiwa acid maeneo ya Sunshine Internet Cafe hapo Mlandege, mjini Zanzibar. Binafsi nalaani vikali kitendo hicho cha kinyama na cha kishenzi kabisa.

Juzi tu Jumatano nilisoma katika gazeti la Mwananchi tukio la mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi Christian Msema wa Mburahati, Dar es Salaam kumwagiwa acid na watu wasiojulikana waliokuwamo kwenye bajaj.

Matukio haya ni ya kinyama na ya kutisha na yanaonekana kushika kasi kila uchao. Bahati mbaya licha ya
 Polisi kutangaza operesheni maalum ya kutafuta kile walichokiita mtandao wa acid hakuonekani mafanikio yoyote.

Hivi uwezo wa uchunguzi wa Jeshi la Polisi umeshuka kiasi hichi? Na kwa nini hadi leo Serikali haijapiga marufuku uuzaji au upatikanaji mwengine wa acid ambao unaonekana kufanyika kiholela kiasi cha kupatikana kirahisi na kutumika kufanyia uhalifu kiasi hichi?

Yeyote au kikundi chochote kilicho nyuma ya matukio haya kinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na kusakwa ili kuchukuliwa hatua kali dhidi yao.

Ismail Jussa
Muwakilishi – Mji Mkongwe

SIMBA YAUA,YANGA YASHIKWA

Simba imekata mzizi wa fitina kwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, huku mabingwa watetezi Yanga, Azam wakilazimisha sare ugenini dhidi Mbeya City na Kagera Sugar.
Kiungo Henry Joseph na mshambuliaji Betram Mwombeki waliingia wakitokea benchi na kuifungia Simba mabao hayo mawili muhimu katika kipindi cha pili. Mabingwa watetezi Yanga, waliokolewa na bao la Didier Kavumbagu wakilazimisha sare 1-1 na Mbeya City waliopanda daraja msimu huu.
JKT Ruvu imeendelea kung’ang’ania kileleni baada ya kuichapa Ashanti United kwa bao 1-0 na kuweka rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo.
MBEYA
Mechi hiyo ilitawaliwa na vurugu na vituko vingi kabla ya kuanza kwake baada ya basi lililobeba wachezaji wa Yanga kushambuliwa kwa mawe, chupa za maji, bia na mashabiki wa Mbeya City wakati likiingia uwanjani na kusababisha kuvunja kioo cha dirisha la dereva.
Dakika chache kabla ya mechi kuanza meneja wa Uwanja wa Sokoine, Modest Mwaluka aliokota mayai matatu katikati ya uwanja.
Mwigane Yahya ndiye aliamsha shangwe za mashabiki wa Mbeya baada ya kuifungia Mbeya City bao la kuongoza katika dakika 49 akiunganisha krosi ya Mazanda.
Baada ya bao hilo Yanga, iliwapumzisha Nizar na Bahanuzi na kuwaingiza Oscar na Jerry Tegete mabadiliko yaliyozaa matunda kwani dakika ya 71 walisawazisha bao hilo kupitia Kavumbagu akimalizia krosi ya Tegete.
Dar es Salaam
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden aliwapumzisha Said Khamis, Twaha Ibrahimu na kuwaingiza Henry Joseph na Betram Mwombeki ili kuimarisha safu ya kiungo iliyoonekana kuzidiwa nguvu na vijana wa Mtibwa.
Mabadiliko hayo yalizaa faida katika dakika ya 67, pale Joseph Shindika alipoipatia Simba bao la kuongoza akiunganisha kwa kichwa krosi ya Amri Kiemba.
Dakika ya 90, Mwombeki aliwainua mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la pili akimalizia vizuri pasi ya Ramadhani Singano ambaye kabla aligongeana vyema na Joseph.


Safari ya Ashanti United kurudi ilipotoka imezidi kushika kasi baada ya jana kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu, goli pekee la Amos Mgisa.
Azam wameendelea na mwendo wa kusuasua baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Mshambuliaji Temi Felix aliwainua mashabiki wa Kagera Sugar,ambapo kiungo Hamisi Mcha aliisawazishia Azam. Katika michezo mingine Tanga, Coastal Union ilitoka sare 0-0 na Prisonsi.
Arusha wenyeji Oljoro JKT walilazimishwa sare 1 -1 na Rhino Rangers, wageni Rhino walipata bao la kuongoza kupitia Saad Kipanga kabla ya Amiry Omary kuisawazishia Oljoro katika dakika 27.
Vilevile Ruvu Shooting ilichapa Mgambo JKT kwa bao 1-0 shukrani k wa bao Elias Maguli.
Imeandaliwa na Vicky Kimaro, Jessica Nangawe (Dar), Msafiri Sanjito (Kibaha), William Paul (Kagera), Mosses Mashalla (Arusha), Doris Maliyaga (Mbeya) Salim
Mohamed (Tanga).

CHANZO  GAZETI LA MWANANCHI

Tuesday, September 10, 2013

HATIMAYE ALEX MASSAWE APANDA KIZIMBANI

Mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Massawe amefikishwa mahakamani Dubai, Falme za Kiarabu (UAE), kwa tuhuma za mauaji baada ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), kuiomba Serikali ya nchi hiyo kumkamata.
Massawe anayetarajiwa kuletwa nchini wakati wowote kuanzia sasa, alikuwa anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu na alikamatwa Dubai, mapema Julai na maofisa wa usalama wa UAE baada ya alama zake za vidole kuonyesha kuwa alikuwamo kwenye orodha ya watu waliokuwa wanasakwa na Interpol.
Baada ya kukamatwa, Mkuu wa Interpol, Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alisema Massawe alikamatwa kati ya Juni 20 na 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.
Massawe ambaye anafanya biashara zake katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba akiwa Dubai, alikutwa na pasi tatu bandia za kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za vidole zilionyesha anaitwa Alex Massawe. “Ombi la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.
Hivi karibuni, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam ilitoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa Massawe ili kukabiliana na kesi mbili ikiwamo ya madai ya kughushi nyaraka mbalimbali.
Hati hiyo ilitolewa baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha ombi la kutaka mfanyabiashara huyo arejeshwe nchini kwa kuwa tayari amefunguliwa kesi namba 150/2013.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi, Robert Manumba alisema kwa agizo hilo, polisi kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliandika barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Dubai kuangalia taratibu za kisheria za kumrudisha baada ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
“Massawe alifikishwa mahakamani Dubai kwa makosa ya kukutwa na hati bandia za kusafiria, lakini vilevile kugundulika kuwa ni kati ya watu wanaotafutwa na Polisi wa Interpol kwa tuhuma za mauaji,” alisema Manumba.
“Sheria inasema mtu akikamatwa nchi nyingine, anashtakiwa nchini humo, huku taratibu za kisheria za kumrejesha zikiendelea kwa nchi ambazo zina utaratibu wa kubadilishana wafungwa kama ilivyo Tanzania na UAE,” alisema Manumba.
Alisema ushahidi dhidi ya mtuhumiwa huyo umekamilika na tayari umewasilishwa Dubai ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria za kumrejesha Tanzania haraka kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kutajwa mahakamani
Aprili 4, mwaka huu, Massawe alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.


Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshtakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.

SERENA WILLIAMS ANYAKUWA TAJI LA U.S OPEN








Mcheza tenisi wa Marekani, Serena Williams akirudisha mpira kwa nyota wa Belarus, Victoria Azarenka wakati wa fainali ya US Open kwa wanawake iliyochezwa USTA Billie Jean King National Tennis Center, New York. Picha na AFP. 



Mchezaji namba moja kwa ubora duniani, Serena Williams ametwaa taji lake la tano la US Open kwa kumchapa Victoria Azarenka kwenye Uuwanja wa Flushing Meadows.
Mmarekani huyo mwenye miaka 32, alitumia nguvu ya ziada kushinda kwa 7-5 6-7 (6-8) 6-1 dhidi ya nyota wa Belarusian.
Williams ametwaa mataji17 Grand Slam kwa mchezaji moja moja, na kuwa pamoja na Martina Navratilova na Chris Evert, huku akiwa nyuma kwa mataji saba kwa Margaret Court anayeshikilria rekodi ya mataji 24.
Baada ya kuruhusu kupoteza seti mbili, na mara mbili akishindwa kuanzisha vizuri, Williams
alibadilika na kuonyesha mchezo wa kiwango cha juu kuliko ilivyokuwa katika fainali 16
zilizopita.
“Vika ni mpinzani bora, ameonyesha uwezo mkubwa wa kupigana wakati wote wa mchezo,
nadhani hii ni sababu iliyomfanya akatwaa mataji mengi ya Grand Slams,” alisema Williams
kuhusu mpinzani wake Azarenka.
Azarenka, 24, amefungwa mara mbili na Williams mwaka hjuu kwanza ni katika mashindano ya Cincinnati na sasa US Open

PANGA PANGUA UVCCM

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI



Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), huku jumuiya hiyo ikitengua uteuzi wa wakuu watatu wa idara zake ambao walikataliwa na Baraza Kuu la chombo hicho lililokutana hivi karibuni, Visiwani Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kuna na taarifa kwamba kumekuwa na mwendelezo wa harakati za kuandaa mkakati wa kumwondoa madarakani mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sadifa Juma Khamis na kwamba vikao vya kupanga mkakati huo vilianza mara tu baada ya mkutano wa Zanzibar.
Watendaji waliosimamishwa ni Wakuu wa Idara za Oganaizesheni, Tumaini Mwakasege, Fedha na Uchumi, Omary Suleiman na yule wa Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji, Omary Justus.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda alilithibitishia gazeti hili kung’olewa kwa watendaji hao na kwamba kuendelea kwao na majukumu yao kutategemea iwapo watathibitishwa na Baraza Kuu la jumuiya hiyo linalokutana mjini Dodoma Oktoba mwaka huu.
“Sisi tuliomba hawa wathibitishwe kwenye kikao kijacho kwa kuwa kulitokea kidogo mkanganyiko wajumbe wakataka tujadili suala hili kwenye Baraza Kuu lililopita lakini kwa kuwa tulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu tukaomba suala hili lisogezwe mbele,” alisema Mapunda.
Mapunda alisema tayari watendaji hao walikuwa wameanza kazi lakini kutokana na baadhi ya kanuni kujikanganya, wameona ni vyema waache suala hilo mpaka kwenye mkutano ujao.
“Kuna kanuni inayotoa mamlaka kwa Kamati ya Utekelezaji na vilevile Baraza Kuu, kwa hiyo inabidi sasa tuweke kwanza mambo sawa kisha kwenye Baraza Kuu la Oktoba, hawa watathibishwa,” alisema.
Hata hivyo habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema si rahisi kwa wakuu hao wa idara kurejea kwenye nafasi zao, kwani kitendo cha wajumbe kuwakataa katika kikao cha Zanzibar kinathibitisha kwamba hawana imani nao.
“Kama wajumbe wa Baraza Kuu wangekuwa wanawaamini, shinikizo lingekuwa ni kuwathibitisha, lakini sisi wajumbe ni kwamba hatuwataki. Inabidi Sadifa na kamati yake ya utekelezaji watuteulie watu wengine,” alisema mmoja wa viongozi wa UVCCM wa mikoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Suala la uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM pia ni mtihani wa kwanza kwa Katibu Mkuu mpya, Mapunda ambaye mara baada ya kuthibitishwa alionja chungu ya mgogoro katika taasisi ambayo yeye ni mtendaji mkuu wake, pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea Sadifa.
Katika mazingira hayo, Mapunda anaweza kujikuta katika mgogoro mkubwa zaidi na wajumbe wa Baraza Kuu, ikiwa atawasilisha majina ya watu walewale waliong’olewa ili wapigiwe kura kwa ajili ya kuthibitishwa.
Vikao vya Siri


Habari kutoka katika mkutano wa Zanzibar zilisema kuwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Kinana alinukuliwa akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara hivyo alishauri suala hilo lipangwe kuzungumzwa katika mkutano wa Oktoba utakaofanyika Dodoma.
Baada ya mkutano wa Baraza Kuu, baadhi ya wenyeviti wa UVCCM wa mikoa, waliripotiwa kuendesha vikao vya siri katika sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku kundi kubwa likitajwa kupanga mikakati ya kuhakikisha Sadifa anang’oka.
Miongoni mwa hoja zinazojengwa dhidi ya mwenyekiti huyo ni pamoja na hiyo ya ukiukwaji wa kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara, hasa Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za Umoja huo kwa kuwatangaza kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo alipaswa kushirikiana nayo, kabla ya kuridhiwa na Baraza Kuu.
Wajumbe wengi watatumia kusimama kazi kwa watumishi hao kama hoja ya kuthibitisha kuwapo kwa makosa ya kiutendaji, hivyo watahoji iwapo kuna sababu za UVCCM “kuendelea kuwa na mwenyekiti ambaye hawezi kuzingatia kanuni na miongozo katika utendaji wake”.
Tuhuma nyingine ambazo zimekuwa zikizungumzwa dhidi ya Sadifa ni matumizi mabaya ya fedha za Umoja huo pamoja na kukodi walinzi binafsi watano; wawili Tanzania Bara na watatu Zanzibar, ambao wamekuwa wakilipwa na UVCCM.
Jana Sadifa alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo mpya alisema: “Hayo masuala mimi bwana siyataki, chochote unachopewa wewe andika unavyojua”.
Aliongeza:“Ukiwa na issue (suala) yoyote inayohusu Umoja wa Vijana, wewe mtafute Katibu Mkuu, hata kama hayo mambo yananihusu mimi, wewe usinitafute mimi, mtafute Katibu Mkuu yeye nimempa mamlaka ya kuwa msemaji mkuu.”
Naye Mapunda alipoulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya bosi wake alisema hawezi kuzungumzia matumizi mabaya ya fedha kwani hana taarifa.
“Tangu niteuliwe sijamaliza hata siku saba, kwa hiyo niwe muwazi tu kuwa sina taarifa nayo na sasa siwezi kusema fedha zilivyotumika,” alisema Mapunda.
Kuhusu suala la walinzi (mabaunsa),Mapunda alisema hao si sehemu ya watumishi aliokabidhiwa na kwamba jumuiya hiyo haina waajiriwa wa aina hiyo.

WANASWA NA DAWA ZA KULEVYA ETHIOPIA

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI


Mshambuliaji wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6bilioni.
Aidha, hilo limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125 bilioni).
Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo alithibitisha jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki akidaiwa kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa kifungo cha miaka tisa hadi 15.
Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.
“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa na mtu mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya yeye ni kuubeba tu. Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndipo warudi Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndipo hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa tena Jumanne (leo) na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado unaendelea.”
Wanamichezo hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za kupandia ndege baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi.


“Kilichotokea ni jambo la aibu kwa nchi na hata wachezaji wenyewe wanajuta. Kwa mfano, Kaniki anasema alikuwa aende England kucheza mpira Desemba lakini sisi tukamwambia hatuwezi kumsaidia inabidi akabiliane na kesi iliyoko mbele yake. Mkwanda yeye ametuambia kwamba anaishi Sweden hatuna maelezo yake zaidi,” alisema Shelukindo na kuongeza kuwa wamewapelekea wanamichezo hao msaada wa mablanketi kwa vile bado wako mahabusu na Ethiopia kwa sasa kuna baridi kali.
Shelukindo alisema wachezaji hao wapo mahabusu kwenye Kituo cha Polisi cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (Federal Police Crime Investigation) na hawana chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa.
Watanzania wengine kuachiwa leo
Shelukindo alisema kuna Watanzania wanne wanaotazamiwa kuachia leo baada ya kumaliza vifungo vyao baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.
“Kuna Watanzania wengine walinaswa hapa miaka ya nyuma wao walikuwa wamemeza wakapasuliwa dawa zikatolewa na baadhi yao walifariki. Hata hivyo, wanne ambao wamemaliza vifungo vyao vya miaka minne wanaweza kurudishwa Tanzania,” alisema Shelukindo.

Tuesday, September 3, 2013

RWANDA YAJITETEA KUHUSU USHURU




Wakati ushuru wa magari makubwa ukiwa umeshushwa kwa wiki moja, Serikali ya Rwanda imejitetea ikisema haijafanya hujuma yoyote dhidi ya Tanzania, bali imepandisha tozo hiyo ili kuifanya ilingane na ile inayolipwa Tanzania.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake jana, Balozi wa Rwanda nchini, Ben Rugangazi alisema kuongezwa kwa ushuru huo wa forodha kisichukuliwe kama jaribio la kutaka kuvuruga uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Balozi Rugangazi alisema Rwanda imeamua kupandisha kiwango chake kutoka Dola za Marekani 152 (Sh240,000) kuwa Dola 500 (Sh790,000) ambazo pia hutozwa na Serikali ya Tanzania kwa muda mrefu.
“Kumekuwa na majadiliano ya muda mrefu ili kuleta ulinganifu wa ushuru wa forodha kwani kwa muda mrefu wafanyabiashara Rwanda wamekuwa wakilalamika kutokana na kushindwa kushindana vizuri kwenye soko la biashara kutokana na tofauti kubwa ya ushuru wa forodha.
“Hili suala tulishawahi kuliwasilisha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tukawaomba wasaidie kurekebisha kasoro hiyo, lakini hawakufanya hivyo. Sasa tumeamua kuchukua hatua hii ili kwenda sambamba na wenzetu Tanzania.
“Pande zote Tanzania na Rwanda zilikubaliana kuwa ushuru mpya ungeanza kutumika Septemba mwaka huu na ndivyo ilivyokuwa,” alisema Balozi Rugangazi.
Siku saba
Kutokana na msongamano wa malori kwenye mpaka wa nchi hizo mbili, Serikali ya Rwanda imeshusha ushuru kwa wiki moja.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema ushuru unaotumika ni ule wa zamani badala ya mpya.
Tizeba alisema alishauriana na Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba na kukubaliana ushuru wa zamani utumike wakati Serikali hizo zikiendelea na mashauriano. Alisema Mawaziri wa Fedha wa Tanzania na Rwanda walitazamiwa kukutana ili kuzungumzia suala hilo.
Dk Tizeba alisema juzi wafanyabiashara wa Tanzania walipata usumbufu mkubwa baada ya kulazimika kulipa Dola 500 kuingiza mizigo yao Rwanda badala ya Dola 152.
Hata hivyo, alikanusha madai kuwa Rwanda imepandisha ada hizo kutokana na mgogoro wa kisiasa baina ya nchi hizo.


Hali mbaya Rusumo
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa msaada mkubwa katika mpaka wa nchi hizo huko Rusumo kutokana na kuwapo kwa msururu mkubwa wa magari ambao unaelezwa kuwa hadi jana ulikuwa umefikia kilometa 20.
Akizungumza kwa simu kutoka Rusumo, Ngara jana, Ofisa Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji mpakani hapo, Mahirande Samuel alisema hali hiyo inatokana na madereva wengi kutokuwa na taarifa ya ongezeko hilo.
“Hali ni mbaya, kwa sasa foleni ya magari imefika hadi Benaco ambako ni umbali wa kilometa 20… Unajua hawa madereva hawakuwa na taarifa na wengi walikuwa wakitoa ushuru wa zamani, pengine wameamua kusubiri mabosi wao wawaongezee fedha,” alisema Samuel.
Haiondoki Bandari ya Dar lakini...
Kuhusu utumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam balozi huyo alisema Serikali yake haina mpango wa kuikacha bandari hiyo, lakini akasisitiza: “Sisi tunaangalia fursa za kiuchumi, tutapenda kutumia bandari yenye ufanisi na ambayo haina usumbufu kwetu. Tutaendelea kutumia bandari zote hii ya Dar es Salaam na ile ya Mombasa lakini tungependelea zaidi kuona tunatumia ile yenye ufanisi zaidi.”

UVCCM KWACHAFUKA

CHANZO CHA HABARI NI GAZETI LA MWANANCHI








Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Sadifa Juma akizungumza katika mkutano wa umoja huo mjini Zanzibar.Wengine ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Iddi na Katibu Mkuu wa CCM, Adulrahman Kinana. Picha ya CCM



Mvutano mkubwa umeibuka ndani ya Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kutokana na baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la umoja huo kudhamiria kumng’oa madarakani mwenyekiti wao, Sadifa Juma Khamis.
Mgogoro huo ulisababisha kikao cha Baraza Kuu kilichokuwa kikifanyika Zanzibar juzi, ambacho mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi kutofikia mwisho kutokana na baadhi ya wajumbe kumtaka Sadifa na Kamati yake ya Utekelezaji kutoka nje ili wajadiliwe kwa kukiuka kanuni.
Sadifa anadaiwa kukiuka Ibara ya 91 ya toleo la nane la Kanuni za UVCCM kwa kutangaza uteuzi wa wakuu wa idara tatu za umoja huo, kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Utekelezaji ambayo kimsingi alipaswa kushirikiana nayo kuwateua, kabla ya kuidhinishwa na baraza kuu.
Habari kutoka katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi ya CCM, Kisiwandui zinasema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kuingilia kati mvutano baina ya baadhi ya wajumbe na Sadifa.
Inaelezwa pia kuwa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM, Sixtus Mapunda naye alionja chungu ya mgogoro huo pale alipopingwa vikali na wajumbe, alipojaribu kumtetea mwenyekiti wake.
Hata hivyo, Sadifa na Mapunda kwa nyakati tofauti jana walisema kuwa mkutano huo ulimalizika bila tatizo na ulikuwa na ajenda moja tu ya kumthibitisha Katibu Mkuu jambo ambalo lilifanyika kama ilivyokuwa imepangwa.
“Kwa mujibu wa kanuni, mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka ya kufungua na kufunga kikao na vyote hivyo tulifanya, hakuna kikao kilichovunjika,” alisema Sadifa.
Alipotakiwa kueleza kuhusu kanuni anayodaiwa kuivunja, alikataa kuzungumzia suala hilo akitaka kwanza mwandishi amwambie chanzo chake cha habari.
“Nani huyo aliyetaka nitoke, wewe nisikilize, kuna watu ambao wanajua kabisa unataka kuzungumza nini hata kabla hujasema na mmoja wa watu hao ni Sadifa kwa hiyo nilishajua kabisa ni nini unataka,” alisema Sadifa na baada mwandishi kuendelea kumuuliza maswali alikata simu.
Kwa upande wake, Mapunda alisema: “Mkutano ulifanyika na kumalizika kama ulivyokuwa umepangwa. Ule ulikuwa ni mkutano maalumu na ulikuwa na ajenda moja tu, mwenyekiti aliufungua na kuufunga kama ilivyokuwa imepangwa. Ajenda ilikuwa ni kunithibitisha mimi tu (kuwa katibu wa UVCCM) na baada ya hilo kufanyika nilikaribishwa na mimi nikazungumza na nikamaliza”.
Ilikuwaje?


Habari zinasema wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Ruvuma, Alex Nchimbi walikuwa wakilalamika kwamba Sadifa alikiuka kanuni katika kuteua wakuu hao wa idara hivyo uwepo wao katika kikao cha baraza hilo haukuwa halali.
Katika hoja hiyo iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna, Nchimbi alimtaka Sadifa na wajumbe wote wa Kamati ya Utekelezaji watoke nje, ili Baraza Kuu liwajadili.
“Sadifa alikataa na badala yake alimwambia Nchimbi akae chini la sivyo angemtoa nje ya mkutano hali ambayo ilizua mvutano mkali kwa sababu wajumbe wengine walisimama kumpinga Sadifa na wachache walikuwa wakimtetea,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho. Kutokana na hali hiyo, Kinana aliingilia kati na kuwaomba viongozi wa UVCCM waende faragha kwa muda ili wakajadiliane na waliporejea aliwatangazia wajumbe kwamba wamekubaliana kuwa kikao hicho kiahirishwe ili kiitishwe kingine mwezi ujao kwa ajili ya kuzungumzia pamoja na mambo mengine, uteuzi huo.
Habari hizo zilimnukuu Kinana akikiri kufanyika kwa makosa katika uteuzi wa wakuu wa idara aliowatangaza katika kikao cha Baraza Kuu cha Februari Mjini Dodoma.
“Kitaitishwa kikao kingine Dodoma mwezi wa 10 (Oktoba) ili tuweze kukamilisha taratibu hizo, lakini wewe subiri utaona tutakamilisha uteuzi halafu yeye naye (Sadifa) atang’oka maana hatuwezi kukaa na mwenyekiti ambaye hajui kanuni,” alisema mjumbe mwingine.
Kwa uamuzi huo, sasa ni dhahiri kwamba Baraza Kuu la UVCCM, limetengua uteuzi wa watendaji hao wa Idara za Oganaizesheni, Fedha na Uchumi na ile ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Habari zaidi zinasema kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi katika kikao hicho na kila mjumbe alifanyiwa ukaguzi wa hali ya juu ikidaiwa kwamba ilikuwa ni kuwabaini wajumbe ambao walikuwa wamepanga kuingia na silaha.
Fedha na simu
Kada wa CCM ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM lililopita, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kugawa kwa kificho fedha kiasi cha Sh100,000 kwa kila mjumbe wa wa mkutano huo lengo likiwa ni kumwokoa Sadifa.
Inadaiwa kwamba mbali na fedha hizo, pia wajumbe walikodiwa usafiri wa boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam na baadhi yao kulipiwa gharama za vyumba vya kulala na chakula.
Kadhalika, wajumbe wote wa kikao hicho walizawadiwa simu aina ya Samsung Galax na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ili ‘kurahisiaha mawasiliano’ miongoni mwao, kitendo ambacho pia kinapewa tafsiri kwamba huenda kuna ajenda nyuma ya simu hizo.

Makamba alikiri kugawa simu hizo lakini akasema ilikuwa sehemu ya kutekeleza ahadi aliyoitoa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM uliofanyika Dodoma Februari 16, mwaka huu ambao wajumbe hao waliomba kupewa simu hizo.
Alisema katika mkutano huo, alialikwa kutoa mada na alizungumzia suala la matumizi ya mitandao ya kijamii katika kukijenga chama na baadhi ya wajumbe walisema wanashindwa kutumia njia hiyo kwa kuwa wapo mbali na maeneo ya mijini.
Alisema kabla ya kutoa simu hizo, umoja huo ulimkumbusha kuhusu ahadi yake kutokana na barua yenye kumbukumbu namba VMM/M.30/39/Vol.17/35 ambayo pia ilimwalika kuhudhuria kwenye mkutano wa juzi.
Makamba alisema ili kutimiza ahadi hiyo, alizungumza na baadhi ya makada wenzake na kuwaomba wamsaidie.
“Nilifanya kaharambee kadogo, mtu ukiombwa na wewe unahangaika huku na huko, walinipa na jana (juzi) tuligawa simu 138,” alisema.
Mgogoro UVCCM
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge, aliwahi kulalamika kuhusu kuwapo kwa kundi la vijana wapatao 10 kutoka mikoa mbalimbali ambao wamekuwa wakimpiga vita na kuingilia utendaji wa kazi zake kinyume cha katiba ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Sadifa amekuwa akilaumiwa na baadhi ya wanachama wa UVCCM kwamba ameshindwa kazi na badala yake amekuwa akitoa lugha chafu mbele ya vikao dhidi ya wajumbe ambao wamekuwa wakihoji mambo yanavyokwenda.
Baada ya kuchaguliwa, Sadifa na Makamu wake, Mboni Mhita walipingwa kwa mabango mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na madai kwamba uchaguzi uliowaweka madarakani uligubikwa na rushwa.


Monday, September 2, 2013

MGOGORO WA TANZANIA NA RWANDA

CHANZO CHA HABARI HII NI WANABIDII, (MWANDISHI ELISA MUHINGO)


Mgogoro wa Rwanda na Tanzania: Vyama vya upinzani vinapwaya katika sera za Mambo ya nje:
Watanzania tumo katika kujifunza mfumo wa Vyama vingi. Huku nyuma tumefanya uchaguzi si kwa kuzisikiliza sera za chama ila kwa ushabiki au kupewa hela. Kidogo kidogo tunaelimika na si mbali tutaanza kuchagua kwa kuzipima sera za chama za kutekeleza vipaumbele vya Taifa letu.
 
Hivi karibuni kwa bahati nzuri umejitokeza mgogoro unaoelekea kuuharibu uhusiano wetu na jirani yetu Rwanda. Wala sijakosea kusema bahati nzuri. Nina maana hiyohiyo. Unajua kama kumefunikwa tatizo, kwa hiyo halionekani usiseme uko salama. Likifunuka likawa wazi shukuru. Naachia hapo.
 
Mgogoro huu unaangaliwa kwa namna tofauti. Wapo wanaouangalia kuanzia Rais wetu alipozishauri nchi zenye mogogoro na vikundi vilivyo msituni kujadiliana. Baada ua ushauri huo Rwanda si ilikataa ushauri tu bali iliamua kumshambulia Rais wetu. Wanaouangalia mgogoro huo kuanzia hapo wengine wanamlaumu Rais kwa nini alisema hivyo. Wanaouangalia mgogoro huu kuanzia nyuma wanamuelewa Rais wetu na wanaishtuka Rwanda na mikakati yake inayoileta katika kutaka kuidhoofisha Tanzania.
 
Katika jambo hili Watanzazania wengi tumekuwa na misimamo tofauti. Lakini kitu kimoja mimi nafikiri nimekipata ni misimamo ya Vyama vya upinzani kuhusu jambo hili. Nasikitika ku conclude kuwa vyama hivi vimeonyesha kupwaya au labda havina msimamo na vyenyewe vinaangalia namna ya kuing’oa CCM hivyo kazi ni kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali yake. Nitatumia vyeo ua vyama badala ya majina ya wahusika. Chadema walimkosoa Rais kwa kuishauri Rwanda kuzungumza na FDLR wakati yeye hajaongea na wapinzani wake. Mtu au chama kulinganisha hali hizi mbili ni dalili ya kupwaya kukubwa. Wapinzani wa Tanzania wanatumia majukwaa wanalindwa na polisi katika mikutano hata kama polisi hao wametumiwa vibaya. Huwezi kulinganisha hali hii ya Rwanda ambako wapinzani wa Rais wake wako gerezani na wengine wako misitu ya nchi jirani. Kumlaumu Kikwete kwa kutowakutanisha ni dalili ya utata katika kufikiri. Kikwete ameshauri viongozi wa nchi hizi wazungumze. Bila shaka nchi hizo zingeonyesha dalili ya kuukubali ushauri Kikwete angekwenda mbele kuandaa mazingira. Utamlaumuje kwa kutowakutanisha wakati aliposhauliwa jibu la kwanza ni kumuita mpuuzi?
 
Nimemsikia Kiongozi wa Upinzani Bungeni akimuuliza Waziri Mkuu kuhusu mgogoro huu. Anashauri utafutwe usuruhishi kwa sababu sera ya nchi hii sio kugombana na majirani. Nimekuwa na mashaka na hoja yake. Sijui ana maana gani kusema si sera ya nchi yetu kutogombana na majirani. Ana maana hata Idi Amin alipotuvamia haikuwa sahihi kumfukuza maana si sera yetu kugombana? Huenda anamlaumu na baba wa taifa kugombana na wareno Mozambique na Smith Rhodeshia.
 
Mtu yeyote wa Kawaida anayeona kinachoendelea DRC hasa eneo la mashariki mwa nchi hiyo atamlaumu Rais wetu kwa kwenda polepole. Mtu yeyote atajua asipochukua hatua mapema kitu kama hicho kitakuja tokea Tanzania miaka mingi ijayo. Lazima Kiongozi mwenye Vision atataka kuisaidia DRC kuondokana na mgogoro huo ili kuifundisha nchi jirani isije ichezea Tanzania huko mbele. Kutaka Tanzania isitengwe namajirani kwa maana ya kuuacha mgogoro miaka mingi ijayo ni kupwaya kwa vyama vyetu katika kuyashughulikia mambo ya nje. Nilitegemea katika hili watanzania wote kuungana na Rais wetu na kuangalia anachukua hatua gani. Vyama vyetu kuliangalia jambo hili kwa umbali wa futi tatu ni kutufanya tuwe na mashaka navyo. Hata kama kwa mfano vyama hivyo vimetuonyesha uwezekano wa kulikomboa taifa letu kuondokana na uongozi ulioshindwa kuudhibiti ufisadi. Unatumia kodi zetu kuendesha serikali kubwa kuliko uwezo wetu. Wananchi wanazidi kuwa maskini huku viongozi wakiwa na mrupurupu kibao. (Na kwa kweli katika hili nawapongeza wapinzani hasa CHADEMA). Lakini kutoonyesha watalindaje heshima ya taifa letu ni sababu tosha ya kuwafaya watanzania wawaimarishe kuwa wapinzani lakini sio kuliongoza Taifa. Tena kama katiba ijayo itampunguzia madaraka Rais kuamua mambo basi kwangu heri kuendelea na uongozi uliopo kuliko kuweka madarakani chama kutakachoharibu sera za nje. Kumbuka sasa Tanzania inatengwa kwa sababu imemwambia Kagame apatane na wanyarwanda wenzake. Tukisema Kikwete aombe msamaha ili wasitutenge, siku tukisema tudhibiti Tanzanite. Kenya wakasema tuwatenge tumwambie rais aombe radhi aseme basi endelea kuchimba. Nina uvumi kuwa Tin bora duniani inatoka wilayani Kyerwa, Mkoani Kagera. Inapochimbwa inauzwa Rwanda kimagendo na Rwanda inaiuza nje. Nje inajulikana Tin bora inatoka Rwanda. Habari za maandalizi ya Bahima Empire hazikuwahi kukanushwa kikamilifu. Rwanda iliwahi kudai sehemu ya Karagwe kuwa ni yake. Sababu wakazi wengi wa eneo hilo ni wanyarwanda. Banyamulenge wanapigana magaribi mwa DRC kutetea maslahi ya watutsi. Kiongozi wa Upinzani alipoibaha serikali kutaka kuacha kugombana na Rwanada aliyafikiria hayo? Anaiwazia Tanzania hadi miaka kumi akiwa rais? Kwanini kiongozi wa upinzani hakumuelewa Waziri Mkuu aliposema jambo hili linahitaji busara? Ni dalili ya kupwaya kwa vyama hivi katika jambo hili. Wasipoangalia CCM itawapiku maana ni jambo nyeti. Wasipoangalia majirani zetu wanafikiri nini juu ya nchi yetu, badala yake wakashikilia wanachosema, ipo siku watalitumbukiza taifa katika mgogoro mkubwa zaidi ya uharibifu wa ufisadi. Hatutawapa nchi. Wajiangalie na watuonyeshe kuwa wamepaona.


Sunday, September 1, 2013

MABADILIKO YA MAKATIBU WAKUU

Mabadiliko yaliyofanywa kwa upande wa Makatibu Wakuu ni kama ifuatavyo:

  • Dk Florens Turuka amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

  • Joyce Mapunjo amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, awali alikuwa Katibu Mkuu Wizara  ya Viwanda, Biashara na Masoko.

  • Jumanne Sagini amekuwa Katibu  Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) awali alikuwa Naibu Katibu  Ofisi wa Waziri Mkuu - TAMISEMI.

  • Dk Servacius Likwalile amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, awali alikuwa Naibu Katibu Wizara ya
Fedha.

  • Dk Patrick Makungu amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, awali alikuwa  Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo.

  • Alphayo Kitanda amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, awali alikuwa Naibu Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.

  • Dk Shaaban Mwinjaka amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara  ya Viwanda, Biashara na Masoko.

  • Dk Uledi Mussa amekuwa Katibu Mkuu Wizara  ya Viwanda, Biashara na Masoko, awali alikuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

  • Profesa Sifuni Mchome amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya  Elimu na Mafunzo ya Ufundi, awali alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.

  • Charles Pallangyo amekuwa Katibu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri.

  • Anna Maembe amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, awali  alikuwa Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo.

  • Sihaba Nkinga amekuwa Katibu  Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo.

  • Sophia Kaduma amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Balozi Sefue aliongeza kwamba:

  • Katibu Mkuu aliyepewa uhamisho ni  Peniel  Lyimo ambaye anahamia Ofisi ya Rais - Ikulu  kwenye “Presidential’s Delivery Bureau” kama Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo mwanzoni alikuwa  Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu.

Makatibu wakuu watakaopangiwa kazi nyingine ni:-
  • Sethi Kamuhanda aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
  • Kijakazi Mtengwa aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto
  • Injinia Omari  Chambo aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi

Katibu anayestaafu ni Patrick Rutabanzibwa ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye sasa amestaafu kwa hiari.

Aidha, Balozi Sefue alisema Rais Kikwete pia amefanya uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu wapya na kuwapa uhamisho baadhi yao.  Aliiwataja Naibu Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa kuwa ni:-

  • Angelina  Madete amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais  Mazingira

  • Regina Kikuli amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu

  • Zuberi Sumataba amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, anayeshughulikia  suala la elimu katika ngazi za Serikali za Mitaa

  • Edwin Kiliba amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI

  • Deodatus Mtasiwa amekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ambaye atashughulikia saula la afya  upande wa  Serikali za Mitaa.

  • Dk Yamungu Kayandabila amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika

  • Profesa Adolf Mkenda amekuwa Naibu Katibu Mkuu ya Fedha anayeshughulikia sera

  • Dorothy Mwanyika amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Fedha anayeshughulikia Fedha za Nje na Madeni

  • Rose Shelukindo amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

  • Dk Selassie Mayunga amekuwa Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

  • Monica Mwamunyange amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi

  • Consolata Mgimba amekuwa  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Elimu na Mafunzo ya Ufundi

  • Profesa Elisante ole Gabriel Laizer amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

  • Armantius Msole amekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Balozi Sefue aliwataja Naibu Makatibu Wakuu waliopewa uhamisho kuwa ni:-

  • John Mngondo ambaye amehamishiwa Wizara ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ametoka Wizara ya Uchukuzi katika nafasi hiyo

  • Selestine Gesimba amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii, anatoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi

  • Injinia Ngosi Mwihava anahamia Wizara ya Nishati na Madini kutokea Ofisi ya Makamu wa Rais

  • Maria Bilia amehamia Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

  • Nuru Milao anahamia  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.